Urasimishaji ardhi ushirikishe halmashauri, wizara ya ardhi na jamii ili kuepuka migogoro

Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akisalimiana 
na baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe alipowasili
katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Christopher Ole Sendeka
Mnufaika
wa MKURABITA, Bw. Heri Nahala akitoa ushuhuda wa namna alivyonufaika na MKURABITA
wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri 
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt.
Mary Mwanjelwa (Mb) kutembelea utekelezaji wa miradi ya MKURABITA katika
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe .
Mkuu wa
Mkoa wa Njombe, Mhe. Christopher Ole Sendeka akimkaribisha Naibu Waziri, Ofisi
ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary
Mwanjelwa (Mb) alipowasili ofisini kwake kabla ya kuanza ziara ya kikazi
kukagua miradi ya MKURABITA. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Ruth Msafiri.

Na Aaron Mrikaria –
Njombe

Naibu Waziri, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa
(Mb) amezishauri Halmashauri nchini kushirikiana na Wizara ya ardhi na walengwa
wa MKURABITA katika zoezi la kurasimisha rasilimali ardhi za wanyonge ili
kuepuka migogoro inayojitokeza.
Dkt. Mwanjelwa ameyasema
hayo leo wakati wa ziara yake ya kikazi Mkoani Njombe alipokuwa akizungumza na
wanufaika wa MKURABITA Wilayani Njombe. 
Mhe. Mwanjelwa ametoa
maagizo hayo baada ya wananchi kuwasilisha kero zao kuhusu kutokushirikishwa
wakati wa zoezi la upimaji ardhi lililofanywa na kampuni binafsi kwa niaba ya
Wizara ya Ardhi jambo lililosababisha kumegwa kwa maeneo yao.
“Jambo lililonishtua ni
hili la Makampuni kurasimisha ardhi, bila kushirikisha wananchi wa eneo husika
hivyo kuna umuhimu mkubwa sasa kwa MKURABITA kuzungumza na Wizara ya Ardhi ili
changamoto hii isijitokeza tena kwasababu serikali ni moja” Dkt. Mwanjelwa
amesisitiza.
Mhe. Dkt,. Mwanjelwa
amefafanua kuwa ushirikishwaji wa wananchi katika zoezi la upimaji ardhi
utasaidia kuondoa migogoro katika kaya na jamii kwa ujumla.
Aidha, Mhe. Dkt.
Mwanjelwa ameridhishwa na zoezi la urasimishaji ardhi wilayani humo kutokana na
ushuhuda uliotolewa na baadhi ya wanufaika waliofanikiwa kiuchumi baada ya
kurasimishiwa ardhi zao ambapo wameweza kuzitumia hatimiliki zao kama dhamana ya
kuombea mikopo katika taasisi za fedha.
 Katika zoezi la urasimishaji ardhi wilayani
humo, jumla ya hatimiliki za kimila
elfu kumi na tatu na arobaini na saba zimeshatolewa kwa wanufaika huku
wanufaika mianne sitini na tatu wakiwa tayari wamenufaika na mikopo ya zaidi ya
shilingi bilioni mbili.
Akitoa ushuhuda, Mmoja wa
Wanufaika wa MKURABITA, Bi. Lucy Mhavile amesema kuwa kabla ya kupata hati
miliki za kimila kiwango chake cha kukopa kilikuwa ni shilingi laki mbili tu,
lakini mara baada ya kupata hatimiliki ya kimila  ameweza kukopa hadi shilingi milioni mia tano
na kwamba ameweza kujenga kiwanda kikubwa cha kusaga nafaka Wilayani Njombe.
Dkt. Mwanjelwa
amehitimisha ziara yake ya kikazi Mkoani Mbeya na Njombe ambapo amekagua miradi
ya MKURABITA na kusisitiza ushirikiano baina ya wadau wote wanaohusika katika
suala la urasimishaji ardhi ili kupunguza umasikini kwa wanufaika.