Vijiji 8,641 vyafikiwa na umeme wa rea


Na Mwandishi Wetu

Jumla ya vijiji 8,641 kati ya vijiji 12,268 vya Tanzania Bara
vimeunganishwa  na umeme kupitia Mradi ya
Usambazaji Umeme Vijijini (REA)
sawa na asilimia 70.4.

Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na
Mipango, Dkt. Philip Mpango wakati akitoa Tathmini ya Utekelezaji wa Mpango wa
mwaka 2019/20 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2020/21.

“Katika
kipindi cha Julai 2015 hadi Januari 2020, jumla ya shilingi trilioni 1.53
zimetumika katika utekelezaji wa mradi huu ikijumuisha shilingi bilioni 207.2
zilizotolewa katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020.” Alisema Dkt.
Mpango.

Katika hatua
nyingine, Dkt. Mpango alisema kuwa thamani
ya shilingi ya Tanzania dhidi ya sarafu nyingine kubwa duniani imeendelea kuwa
tulivu kwa kipindi chote cha mwaka 2019.

Ameeleza kuwa utulivu wa sarafu ya Tanzania dhidi ya sarafu kubwa duniani
umetokana na utekelezaji mzuri wa sera ya fedha na ya kibajeti, pamoja na
kupungua kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho mali
nchi za nje.

Kwa upande wa afya, Waziri Mpango ameeleza kuwa kuwa
Serikali ya Awamu ya Tano
imeendelea kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa kugharamia ujenzi na
uboreshaji wa miundombinu ya vituo 540 vituo vya afya 361, hospitali za
halmashauri za wilaya 71, hospitali za zamani tisa na zahanati 99 ambapo
watumishi  477 wameajiriwa na kupangwa
kwenye vituo hivyo.

Dkt. Mpango  alifafanua kuwa katika
kipindi cha Julai 2015 hadi Januari 2020 jumla ya shilingi trilioni 3.01
zimetumika kugharamia huduma za afya ikijumuisha shilingi bilioni 14.5
zilizotumika kununua mashine ya Positron Emmission Tomography (PET scan) kwa ajili
ya hospitali ya Ocean Road.

Akiongelea kuhusu mkakati wa
uwezeshaji wa kaya maskini kiuchumi, amesema kuwa kwa sasa Serikali inatekeleza
Awamu ya III ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF III), ambapo jumla ya kaya
1,067,041 zenye wanakaya 5,130,001 zimetambuliwa na kuandikishwa katika vijiji
na mitaa 9,627 kwenye Halmashauri 159 Tanzania Bara na kaya 32,248 zenye
wanakaya 169,999 katika shehia 204 za Zanzibar na ruzuku ya fedha shilingi
bilioni 968.73 imehawilishwa katika kaya hizo.

Amesema kati ya fedha hizo,
shilingi bilioni 935.94 ni kwa ajili ya kuhudumia Kaya zilizopo Tanzania Bara
na shilingi bilioni 32.79 ni kwa ajili ya Kaya zilizopo Zanzibar.

Aidha, katika kipindi cha Julai
2019 hadi Januari 2020, ufanisi wa kukusanya mapato ya kodi umeimarika na
kufikia asilimia 96.9 ya lengo ikilinganishwa na ufanisi wa asilimia 88.6 katika
kipindi cha Julai 2018 hadi Januari 2019, sawa na ukuaji wa asilimia 16.6.