Viwanda kuondoa umasikini wa wafugaji na wavuvi

 

Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa pili kutoka kushoto), akiwa
na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul (wa pili kutoka
kulia) pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia
Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah (wa kwanza kutoka kushoto), wakati Waziri
Ndaki alipofanya ziara ya kikazi katika kiwanda cha kuchakata samaki cha
Nile Perch kilichopo kata ya Nyakato, Wilaya ya Nyamagana jijini
Mwanza. 



Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kutoka
kushoto), akiwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul
(anayemfuata) pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi
anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah (wa kwanza kutoka kulia),
wakati Waziri Ndaki alipofanya ziara ya kikazi katika kiwanda cha
kukausha mabondo ya samaki cha Hong Lin International Ltd kilichopo
Wilaya ya Ilemela, jijini Mwanza. 


Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki na Naibu Waziri wa wizara hiyo
Mhe. Pauline Gekul wakiangalia mabondo ya samaki baada ya kukaushwa
tayari kwa ajili ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi, wakati walipofanya
ziara ya kikazi katika kiwanda cha kukausha mabondo ya samaki cha Hong
Lin International Ltd kilichopo Wilaya ya Ilemela, jijini Mwanza. 
Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiwa na Naibu Waziri wa Mifugo
na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul wakati walipofanya ziara ya kikazi katika
Maabara ya Taifa ya Uvuvi iliyopo Kata ya Nyegezi Wilaya ya Nyamagana
Mkoani Mwanza na kushuhudia namna maabara hiyo inayofanya kazi kwa
kufanyia uchunguzi sampuli za samaki kutoka viwandani. Wa kwanza kushoto
ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt.
Rashid Tamatamah.


**********************************************


Na. Edward Kondela


Serikali
imesema itahakikisha sekta za mifugo na uvuvi zinawaondoa wananchi
katika umasikini, kupata ajira na nchi iweze kuuza bidhaa bora za mazao
ya mifugo na uvuvi ndani na nje ya nchi.


Akizungumza
jana (28.12.2020) katika siku yake ya kwanza ya ziara ya kikazi ya siku
mbili Mkoani mwanza, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki
wakati akihitimisha ziara hiyo kwenye kiwanda cha kuchinja na kuchakata
nyama cha Chobo kilichopo Kata ya Usagara Wilaya ya Misungwi amesema
wizara imekuwa ikichukulia kwa uzito mkubwa suala la viwanda ambalo
litaweza kubadilisha fikra za wafugaji na wavuvi.


“Wananchi
wetu waondoe umasikini, wananchi wetu wapate ajira na sisi tuuze bidhaa
za mazao haya ya mifugo na uvuvi yaliyo bora hapa ndani na kule kwa
wenzetu nje, sasa mimi nikikuta hali ya mkwamo kwa kitu ambacho
kinatusaidia kuelekea huko napata shida.”
Amesema Mhe. Ndaki


Waziri
Ndaki akifuatana na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul
katika ziara hiyo amefafanua kuwa haridhishwi na baadhi ya changamoto
wanazokutana nazo wawekezaji ambao wamejikita katika kuyaongezea thamani
mazao ya mifugo na uvuvi na kumuagiza Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama
nchini Bw. Iman Sichalwe kumpatia taarifa ya hali ya viwanda vya nyama
nchini ili apate tathmini halisi ya utendaji kazi wa viwanda hivyo,
baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha Chobo, Bw. John Chobo
kubainisha baadhi ya changamoto ambazo Waziri Ndaki amesema wizara
itahakikisha inafuatilia changamoto zinazoihusu wizara hiyo ili
kuzipatia majibu.


Kwa
upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho Bw. John Chobo amesema
kwa sasa kiwanda chake kimesimamisha uzalishaji na kinatarajia kuanza
kurejea katika shughuli zake Mwezi Januari Mwaka 2021 baada ya ugonjwa
wa Covid 19 kuathiri shughuli za kiwanda hicho ambacho kimekuwa
kikisambaza nyama katika nchi za falme za kiarabu.


Bw.
Chobo amesema kutopatikana kwa taarifa sahihi za mifugo kumekuwa
kukichangia kwa kiasi kikubwa soko la nyama kutoka Tanzania kwenda nje
ya nchi kuwekwa katika daraja la chini kwa kuwa mifugo mingi ambayo
inachakatwa viwandani haina taarifa sahihi juu ya ukuaji wake, magonjwa
na chanjo mbalimbali ambazo mfugo huo umepatiwa.


Akiwa
katika Kiwanda cha kuchakata samaki Nile Perch kilichopo eneo la
viwanda katika Kata ya Nyakato Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza, Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiambatana na Naibu Waziri Mhe.
Pauline Gekul amewataka wawekezaji wa viwanda vya samaki vilivyopo
Mkoani Mwanza kuhakikisha wanatumia usafiri wa ndege kutoka katika
kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Mwanza kusafirisha minofu ya samaki
ili kutangaza bidhaa zinazotengezwa hapa Tanzania.


“Tungependa
kuona usafirishaji wa minofu ya samaki unafanyika hapa nchini kwetu,
badala ya nchi jirani kwa kusafirisha kwa malori kwenda nchi za jirani,
kuna uwekezekano kabisa wa kutoa minofu ya samaki kutoka kiwanja cha
ndege cha Mwanza kwenda nje ya nchi badala ya kutumia nchi za jirani.”
Amefafanua Mhe. Ndaki


Aidha,
amewataka wawekezaji wa viwanda vya samaki kuangalia namna ya kuongeza
bei ya kununulia samaki kwa wavuvi wanaopeleka samaki katika viwanda
hivyo ili wavuvi hao waweze kubadilisha maisha yao na kunufaika kupitia
Sekta ya Uvuvi.


Waziri
Ndaki amebainisha hayo baada ya Meneja Mkuu wa Kiwanda cha kuchakata
samaki cha Nile Perch Bw. Rupesh Mohan kumueleza Waziri Ndaki na Naibu
Waziri Gekul kuwa viwanda vya samaki vimekuwa vikikosa malighafi ya
kutosha kutokana na soko la ndani kukua na wakati mwingine kupata samaki
kwa bei ya juu, hali iliyomlazimu Waziri Ndaki kubainisha kuwa kama bei
ya soko la ndani imepanda ni dhahiri wavuvi watauza samaki katika soko
hilo badala ya kupeleka viwandani ambapo wanauza kwa bei ndogo.


Hivyo
amevitaka viwanda vya kuchakata samaki kuangalia upya bei ya samaki
wanayonunua ili wavuvi nao waweze kunufaika na kuboresha maisha yao na
viwanda pia viweze kupata malighafi za kutosha.


Pia,
Waziri Ndaki ametembelea kiwanda cha kukausha mabondo ya samaki cha
Hong Lin International Ltd kilichopo Wilaya ya Ilemela jijini Mwanza na
kufurahishwa na kiwanda hicho kwa kutumia kiwanja cha ndege cha
kimataifa cha Mwanza kusafirisha bidhaa zake kwenda nchi za nje.


Naye
Mkurugenzi wa kiwanda hicho Bi. Wang Shenghong ameishukuru Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji
hali inayomuwezesha kufanya shughuli zake bila matatizo huku akiomba
pia baadhi ya tozo zipunguzwe.


Katika
siku ya kwanza ya ziara yake Mkoani Mwanza, Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki akiwa na Naibu Waziri Mhe. Pauline Gekul
wametembelea pia Maabara ya Taifa ya Uvuvi, Wakala ya Elimu na Mafunzo
ya Uvuvi nchini (FETA) na Kituo cha Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi (FRP).