Viziwi wawezeshwa kufanya kazi kwa usalama

 

  Mkuu
wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika, akifungua mafunzo ya Usalama na Afya
mahali pa kazi yaliyotolewa na OSHA kwa watu wenye changamoto ya kusikia
(Viziwi) mkoani Mbeya. Kulia kwake ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA,
Khadija Mwenda na kushoto ni Katibu wa Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi
Tanzania (TAMAVITA), Kelvin Nyema.
Kaimu
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, akifunga mafunzo ya Usalama na
Afya kwa watu wenye changamoto ya kutosikia wa Mkoa wa Mbeya.
Alioambatana nao ni Kaimu Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini,
Faston Uswege (Wa kwanza kushoto) na viongozi wa Taasisi ya Maendeleo ya
Viziwi Tanzania.
Mwezeshaji
kutoka OSHA, Simon Lwaho, akizielezea picha kuhusu usalama wa umeme
zilizochapishwa katika bango wakati wa mafunzo ya Usalama na Afya mahali
pa kazi yalitolewa kwa viziwi mkoani Mbeya.

 Baadhi
ya washiriki wa mafunzo ya Usalama na Afya mahali pa kazi kwa watu
wenye changamoto ya kutosikia wa Mkoa wa Mbeya wakifuatilia moja ya mada
zilizokuwa zikiwasilishwa na wawezeshaji kutoka OSHA.
  Mwezeshaji
kutoka OSHA, Renatus Qaqal, akionyesha matumizi sahihi ya kofia ngumu
katika sehemu ya kazi alipokuwa akiwasilisha mada wakati wa mafunzo ya
Usalama na Afya mahali pa kazi yalitolewa kwa viziwi mkoani Mbeya.

Na Mwandishi Wetu


Kufuatia
mchango mkubwa wa watu wenye ulemavu katika shughuli za uzalishaji
nchini, serikali imesema kuna umuhimu wa kuwawezesha kupitia mafunzo ya
usalama na afya kazini pamoja na kuwapa mitaji ili wawaze kuboresha
shughuli zao za kiuchumi.


Kauli
hiyo ya serikali imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika,
ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa kwenye ufunguzi wa mafunzo ya kukuza
uelewa wa masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi yaliyoandaliwa na
Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kwa kushirikiana na
Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi Tanzania (TAMAVITA) Mkoa wa Mbeya.


Mafunzo
hayo ya siku moja yalijikita katika kuainisha na kushauri mbinu mahsusi
za kudhibiti vihatarishi vya usalama na afya ambavyo huambatana na
shughuli mbali mbali za uzalishaji ikiwemo ujenzi, kilimo, useremala,
kilimo, ufugaji, biashara ndogo ndogo pamoja na kazi za maofisini.


Miongoni
mwa vihatarishi vilivyoainishwa na watalaam wa OSHA katika mafunzo hayo
ni pamoja na; vumbi, kelele, kemikali, umeme, mitambo na zana mbali
mbali za kazi.


Katika
hotuba yake ya ufunguzi wa mafunzo, Mkuu wa Wilaya amesema: “Pamoja na
serikali kutenga fungu maalum la fedha kwa ajili ya kutoa mikopo isiyo
na riba kwa makundi mbali mbali katika jamii ambapo asilimia mbili (2%)
ya fedha hizo ni kwa ajili ya watu wenye ulemavu, kama serikali tunaona
kuna umuhimu wa kutoa mafunzo ya Usalama na Afya kwa makundi lengwa ili
waweze kuepuka madhara yanaweza kusababishwa na kutozingatia kanuni za
usalama na afya kazini.”


Aidha,
Mkuu huyo wa Wilaya aliipongeza Taasisi ya OSHA kwa kutekeleza ipasavyo
wajibu wake ikiwemo kufanya kaguzi za Usalama na Afya katika sehemu
nyingi za kazi pamoja na kuwaelimisha wananchi kuhusiana na masuala ya
Afya na Usalama kazini na kuitaka kuongeza jitihada zaidi ili kuweza
kuwafikia wananchi wengi zaidi.


Kaimu
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema mafunzo hayo yamekuwa
yakitolewa kwa makundi mbali mbali ya kijamii wakiwemo watu wenye
ulemavu katika mikoa mbali mbali na kusisitiza kwamba mafunzo hayo ni
endelevu.


“Kama
Taasisi yenye dhamana ya Usalama na Afya kwa mfanyakazi, tumeona kuna
umuhimu wa kuyafikia makundi haya ya watu wenye ulemavu kwakuwa
tunatambua kwamba ulemavu ni hali tu na haupaswi kuwa kikwazo kwa mtu
kushiriki katika shughuli kiuzalishaji.


“Tumeshayafikia
makundi mbali mbali ya watu wenye ulemavu katika mikoa kadhaa ikiwemo
Kagera, Dar es Salaam, Pwani na sasa Mbeya na tutaendelea kutoa mafunzo
haya katika mikoa mingine,” alieleza Kiongozi huyo Mkuu wa Taasisi.


Alisema
baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Renatha Exsavery ambaye ni
mwanafunzi wa ufundi katika Chuo cha VETA Mbeya na Queen Majembe
wameeleza kufurahishwa kwao na mafunzo waliyoyapata ambapo wamesema
mafunzo hayo yatawawezesha kujilinda dhidi ya vihatarishi mbali mbali
vilivyopo katika sehemu zao za kazi.


“Mafunzo
haya tuliyoyapata leo tumeyaona yanafaida nyingi kwani yatatusaidia
kulinda afya zetu na kupitia mafunzo haya tutakuwa waangalifu zaidi
katika kazi mbali mbali ambazo ni hatarishi hususan kuzingatia matumizi
sahihi ya vifaa kinga muhimu,” alisema Renatha Exsavery, Mshiriki wa
Mafunzo.