Na Seif Mangwangi, Dodoma
SERIKALI imevitaka vyombo vya habari nchini kuendelea kutoa elimu ya kupinga ukatili dhidi ya watoto na wanawake katika jamii ili kukomesha vitendo hivyo na kujenga jamii bora, usawa na Taifa lenye amani na utulivu.

Wito huo umetolewa leo Februari 28, 2025 Jijini Dodoma na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, jinsia, wanawake na makundi Maalum, Dkt Doroth Gwajima alipokuwa akifungua mafunzo ya Waandishi wa habari wanaoshiriki katika utekelezaji wa programu jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na maendeleo ya Mtoto (PJT – MMMAM)kupitia mradi wa Mtoto kwanza.
” Napenda kuchukua nafasi hii kuwaomba waandishi wa habari mtoe taarifa za hali ya unyanyasaji wa watoto na changamoto zinazokwamisha jitihada za kulinda haki zao, na hamasisheni jamii na wadau wote kuendelea kuwekeza katika utoaji wa huduma bora za malezi ya watoto,” amesema Dkt Doroth.
Amesema Serikali inaamini baada ya mafunzo hayo, waandishi wa habari watakuwa na mbinu bora zaidi za kutoa habari zenye athari chanya kwa jamii na kuchochea mabadiliko yanayohitajika.

Aidha amevitaka vyombo vya habari kutoa elimu ya lishe kwa jamii, ili kuendelea kupunguza changamoto ya udumavu kwa watoto ikiwa ni pamoja na kuhamasisha utoaji wa chakula shuleni hususani katika madarasa ya elimu ya awali ili kuendelea kuchochea ukuaji bora na ujifunzaji wenye tija.
“Kuhamasisha watoto kupata chanjo na huduma za afya, ikiwa ni pamoja na wajawazito na wenza wao kuhudhuria kliniki kabla na baada ya kujifungua, hii itasaidia kushirikishana na kuchochea ukuaji sahihi wa mtoto katika familia”, amesema na kuongeza:
“Vyombo vya habari vitumike kuhamasisha jamii yetu kuandikisha watoto wote wenye umri wa miaka mitano kwenye darasa la elimu ya awali kama sera ya elimu inavyoelekeza hii itatoa fursa ya kipekee kwa watoto wetu kujengewa utayari wa shule na kuwa na mwanzo bora kwenye elimu yao,”. Amesema.

Aidha amevitaka vyombo vya habari kuendelea kutoa elimu ya kupinga ukatili dhidi ya watoto na wanawake katika jamii.
” Toeni taarifa za hali ya unyanyasaji wa watoto na changamoto zinazokwamisha jitihada za kulinda haki zao, na hamasisheni jamii na wadau wote kuendelea kuwekeza katika utoaji wa huduma bora za malezi ya watoto,” amesema.
Amesema ni matumaini ya Serikali kuwa baada ya mafunzo hayo, waandishi wa habari watakuwa na mbinu bora zaidi za kutoa habari zenye athari chanya kwa jamii na kuchochea mabadiliko yanayohitajika.

Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto inalenga kuhakikisha kuwa kila mtoto mwenye umri wa miaka 0 hadi chini ya miaka 8 nchini anapata malezi yanayozingatia afya bora kwa mtoto, lishe toshelevu, ulinzi na usalama wa mtoto, malezi yenye kuitikia hisia za mtoto na kutoa fursa za uchangamshi na ujifunzaji wa awali wa mtoto.
Inaelezwa kuwa uwekezaji katika umri wa miaka 0 hadi8 kwa mtoto, ndio msingi wa kuwa Taifa imara lenye raslimali watu wenye tija katika kipindi cha sasa, siku za usoni na baadaye.
