Wabadhilifu, wezi wa dawa za serikali wapewa onyo tena

Na. Atley Kuni- TAMISEMI

Naibu
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dkt.
Dorothy Gwajima, ameapa kwamba moto dhidi ya wabadhilifu wa dawa
aliouwasha katika zoezi la ufuatiliaji hautazimika wala kupoa, huku
akiwaomba wananchi kutoa ushirikiano wa karibu kwa kuwafichua watu/mtu
yeyote atakayebainika kuhujumu jitihada za serikali.


Gwajima
ametoa kauli hiyo ikiwa ni mara ya pili kurudia wito huo mbele ya
Makatibu Tawala wa Mikoa, wataalamu Wafamasia kutoka mikoa 13 na wadau
wa maendeleo Global Supply chain, waliokutana mjini Dodoma kwenye ukumbi
wa Mikutano wa OR-TAMISEMI katika kikao kazi cha tathmini ya mbinu mpya
ya kuimarisha takwimu za bidhaa za afya.

Akizungumza
katika kikao hicho Gwajima amesema, vita hiyo wataweza kuishinda kwa
kuunganisha nguvu na wananchi kutoka maeneo yote nchini.

“Niwaombe
wanachi kuwa mstari wa mbele kufichua wale wote mtakaowabaini
wanahujumu suala la dawa kwani vita hiyo siyo ya mtu mmoja mmoja wala
serikali peke yake bali ni ya jamii nzima” alisema Gwajima na kuongeza
kuwa, “wapo watu wanaotambua nani ni adui wao katika vita hivi ndiyo
maana jana nimeona kwenye Jamiiforum wakinipa pole na kunipongeza,
lakini nasema lazima tutembee na wananchi katika hili.” alisisitiza
kiongozi huyo.

Gwajima
alisema inashangaza unafika kwenye kituo ambacho kina wafamasia
wasiopungua sita (6) lakini unakuta kitabu cha kupokelea dawa (ledger)
hakijahuishwa kwa zaidi ya miezi 5, hii ni hali ya hatari sana, suala
hilo halivumiki na wala hawezi kukubaliana nalo.

“Viongozi
wangu Makatibu Tawala, mnaelewa tunatekeleza ilani ya Chama Cha
Mapinduzi ya 2015-2020, hivyo fuatilieni hili hadi kwenye stoo za
kutunzia dawa lakini pia ombeni taarifa na ingieni kwenye mikutano yao
muone kile wanachokijadili maana humo hakuna zuio lolote kwa kuwa
taarifa zinazojadiliwa humo sio siri za mgonjwa, sasa wasije
wakajifichia kwenye mwamvuli wa taarifa za kitabibu kwa kuwahadaa eti
siri za Mgonjwa?” Alihoji na alikemea  

Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Global Supply Chain Tukay Mavere
aliwataka wachumi, watawala wa fedha pamoja na watumiaji wa mfumo wa
eLMIS kukaa pamoja na kuja na mbinu mbadala za kudhibiti hali ya dawa na
upatikanaji wake na kutoa mrejesho wa kile ambacho serikali imewekeza.

“Lengo
la mfumo huu tunataka tuwe tunachukua jambo, tunalichakata na kisha
tunalitolea majibu kwa wakati sio kungoja muda uende, aidha hii inakuwa
ni zoezi endelevu katika utendaji wa siku kwa siku kama mfumo ulivyo,
hivyo tumeitana ili tuwe na uwelewa wa pamoja juu ya hili tunalokusudia
kulifanikisha” alisema Mavere.

Kwa
upande wao washiriki wa warsha hiyo wameipongeza serikali na wadau kuja
na mfumo huo, kwani ni matumaini yao utakuwa suluhu ya yale
wanayofanyia kazi kila siku.

“Kama
Naibu Katibu Mkuu alivyosema, mfumo huu utasaidia kuondoa ziada ya dawa
inayosababisha upotevu wa pesa kutokana na kuchina kwa Bidhaa
zilizoingizwa bila takwimu sahihi, vema sasa kila mmoja wetu akitoka
hapa awe mstari wa mbele katika kuutumia mfumo kwenye utendaji wake.”
alisema, Msalika Makungu Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora.

Katika
kikao hicho cha siku mbili pamoja na mambo mengine yatakayojitokeza,
wataalam watajifunza kupata takwimu sahihi kwa ajili ya kufanyia maoteo
kwa kuwa mfumo unaanzia chini kwenye huduma kwenda juu, hivyo itakuwa ni
fursa ya kuwajengea uwezo timu za uratibu wa afya za Mikoa na Wilaya,
kupata taarifa sahihi na kufanya ugawaji wa dawa kulingana na mahitaji
na kuondokana na tatizo la dawa kwenye maeneo yenye dawa nyingi.

Mambo
mengine ni kufanya bajeti kulingana na rasilimali zilizopo lakini pia
kuwezesha kufanya usimamizi kwa njia ya mtandao Online Supervision.

Katika
kikao hicho, Wataalamu hao walikumbushwa juu ya viapo vyao kwa
kuongozwa na kiapo mbele ya Naibu Katibu Mkuu huku wakiwa wamenyoosha
mikono juu na kuapa kwamba, watakuwa chachu ya mapambano dhidi ya
ubadhilifu wa dawa na endapo wakishindwa basi wawe tayari kuachia
nyadhifa zao hata kwa kutuma ujumbe wa maandishi kwenye mtandao wa kundi
sogozi (WhatsApp) kuhusu  kuachia madaraka waliyonayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *