Wabunge wanne chadema wanusurika kwenda gerezani….mahakama yawapa onyo

Mbunge
wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter
Msigwa, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya
wamenusurika kwenda gerezani baada ya mahakama kuridhia ombi la
kutowafutia dhamana zao.


Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba leo
Jumatano Novemba 20, saa saba mchana imetoa uamuzi kuhusu maombi ya
Jamhuri ya kutaka washtakiwa hao wafutiwe dhamana kwa kushindwa kufika
Mahakamani Novemba 15 mwaka huu.

“Baada
ya kupitia hoja za pande zote mbili na hoja za washtakiwa mahakama
inaona kwamba maelezo yao hayana mashiko na kuwafutia dhamana ni hatua
kali sana badala yake mahakama inawapa onyo kali wasirudie tena,”
amesema Hakimu Simba.

Hakimu Simba amesema walifanya makusudi na kwamba hatua ya kujisalimisha polisi ni uoga wa jambo ambalo lingewatokea.

Kutokana
na hali hiyo, amesema mahakama imewaachia kwa dhamana zao za awali na
kuwataka wafuate masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili.

Katika
kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Februari Mosi na
Februari 16, mwaka huu Mbowe na wenzake wakiwa Kinondoni, Dar es Salaam
kwa pamoja walikula njama na  wengine ambao hawapo mahakamani ya kutenda
kosa la jinai ikiwamo kuendelea na mkusanyiko isivyo halali na
kusababisha chuki na uchochezi wa uasi.