Wahamiaji haramu tanzania kusakwa nyumba za wageni,stesheni za mabasi, stesheni za reli na mahotelini

Na Mwandishi Wetu

Serikali
imetangaza kuanza operesheni, doria na misako  maalumu ya kuwasaka na
kuwakamata wahamiaji haramu katika sehemu mbalimbali ikiwemo  katika 
nyumba za kulala wageni, stesheni za mabasi, stesheni za reli, mahoteli,
mialo ya uvuvi pamoja na maeneo yenye muingiliano wa shughuli za
kibiashara hasa vijiji vinavyojishughulisha na shughuli za
kilimo,makampuni binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali.

Hayo
yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad
Masauni, mkoani Kigoma baada ya kikao cha ndani na   Wakuu wa Vyombo
vilivyopo chini ya wizara yake ikiwemo Jeshi la Polisi, Uhamiaji,
Zimamoto na Uokoaji, Magereza, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa(NIDA)
na Idara ya Wakimbizi.

“Nchi
yetu inaelekea katika Uchaguzi Mkuu,kama vyombo vya ulinzi na usalama
lazima tutimize majukumu yetu na sasa tunaanza msako nchi nzima hasa
katika mikoa iliyopo mipakani,tutaimarisha vizuizi vyetu vya barabarani
nchi nzima,tutatoa elimu kwa wananchi wetu jinsi ya kuwatambua watu
wasio raia ambao wameingia nchini bila kufuata utaratibu na kubwa zaidi
tutafanya ukaguzi katika makampuni binafsi na mashirika yasiyo ya
kiserikali” alisema Masauni

“Kumekuwepo
na wimbi kubwa la watu kuingia nchini bila kufuata utaratibu,sisi kama
serikali hatukatazi mtu kuingia nchini basi wafuate utaratibu,kila mtu
kwa kada yake anaetaka kuingia nchini kuna utaratibu wake wa kufuata na
serikali haijawahi kumnyima raia yoyote yule wa kigeni fursa ya kuingia
nchini.

Masauni
pia aliwataka wananchi kutowahifadhi au kuwasafirisha  watu wasio raia
kwani ni kinyume na sheria na adhabu yake ni kifungo cha muda wa miaka
ishirini au faini ya milioni ishirini  au vyote kwa pamoja ikienda
sambamba na kutaifishwa kwa chombo cha usafiri kilichohusika
kuwasafirisha washtakiwa na kwa mwananchi atakaekutwa akimhifadhi au
kumsafirisha mhamiaji haramu adhabu yake ni kifungo kisichozidi miaka
mitatu na faini isiyozidi laki tano au vyote kwa pamoja.

Akizungumza
katika kikao hicho Afisa Uhamiaji Mkoa wa Kigoma,Kamishna Msaidizi
Remigius Pesambili alisema katika kipindi cha mwezi Januari hadi
Disemba,2019 wamekamata wahamiaji haramu 3.992 na kuchukuliwa hatua
stahiki kwa mujibu wa sheria”

“Idara
ya Uhamiaji hapa Kigoma kwa kushirikiana na vyombo vingine  vya Ulinzi
na Usalama tumefanikiwa katika mwaka uliopita kuanzia Januari hadi
Disemba kukamata wahamiaji haramu kama ifuatavyo; raia wa Burundi 3,293,
Kongo 631, Kenya 12, Uganda 28, Rwanda 16, China 9, Somalia 2 na
Msumbiji , ambapo jumla yake ni wahamiaji haramu 3,992 na tayari
washachukuliwa hatua na wengine wako magerezani tayari wakitumikia
adhabu” alisema DCI Pesambili

Aliongeza
pia katika kipindi cha Januari hadi Disemba 2019 raia wa kigeni 1,544
waliondoshwa nchini,815 walipewa amri ya kuondoka,534 walifikishwa
mahakamani,231 waliachiwa huru baada ya kubainika kuwa hawana makosa ya
kuwafikisha mahakamani na 868 walikabidhiwa Idara ya Wakimbizi.

Kuwepo
kwa wahamiaji haramu nchini kunatajwa kushamiri sana katika mikoa
iliyopo mipakani huku upatikanaji wa nyenzo za kutosha ikiwemo
magari,elimu kwa wananchi juu ya kutoa taarifa za wahamiaji katika eneo
lao,utoaji wa vitambulisho vya taifa uelekezewe nguvu hasa zaidi katika
mikoa ya mipakani,vikao vya ujirani mwema baina ya Tanzania na nchi
tunazopakana nazo na utolewaji wa vibali vya wakimbizi ikiwemo kufanyika
upewaji wa uraia vikitajwa uenda vikawa suluhisho la kupunguza uhamiaji
haramu.