Wahitimu Darasa la Saba Meccson wafundwa

Egidia Vedasto
Arusha

Wanafunzi waliomaliza masomo yao katika shule ya msingi ya MECSONS iliyopo Arusha Mjini wameaswa kutosahau maadili waliyofunzwa ya kutojiunga na makundi mabaya ili waweze kutimiza ndoto zao.

Akizungumza katika mahafali ya 13 ya shule hiyo, Mdhibiti Ubora Shule Mkoa Regina Kitanga amesema kwa hali ya sasa wazazi na walezi wasione aibu tena kuwaelewesha watoto juu ya ushoga, ulawiti na usagaji.

“Tafadhali mzazi ongea na mtoto wako usione aibu kumwambia kila sehemu ya mwili ina matumizi gani, maana ukinyamaza atakutana na wenzake watakaomfundisha na atajiunga nao” amefafanua Kitanga.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shule ya Awali na Msingi ya MECSONS Mecky Shirima ameiomba Serikali kupambana na wimbi la upoteaji wa watoto linaloendelea nchini, jambo linaloleta wasiwasi mkubwa katika jamii.

Aidha ameongeza kuwa, ni vema Serikali kuweka mikakati madhubuti juu ya wale wanaobainika wakijihusisha na vitendo vya utekaji na wizi wa watoto ili adhabu kali ichukuliwe na kuwa funzo kwa wengine.

“Imefikia wakati ukisikia mtoto hajafika shule au nyumbani moyo unalipuka, wasiwasi unatawala kiasi unaweza hata kuzimia, sababu unawaza labda ameuliwa na viungo vyake tayari vimechukuliwa”ameeleza Shirima.

Wakati huo huo Katika risala ya Shule iliyosomwa na Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Jadson Deoglas kwa Mgeni rasmi, ameeleza kuwa Shule hiyo imepata mafanikio makubwa kutoka 2006 ilipoanzishwa ikiwa na wanafunzi wawili awali na kufikia leo hii ikiwa na jumla ya Wanafunzi 664, Wasichana 344 na Wavulana 320.

Akieleza malengo ya Shule amesema, wanajipanga kupandisha wastani kutoka “A” Bora kufikia”A” Bora zaidi kwa mwaka huu wenye jumla ya wanafunzi 64 huku akiwaomba wazazi kulipa ada kwa wakati ili kutoathiri kiwango cha taaluma.

Mmoja wa wazazi wa shule hiyo Kitangenyi Misama amewakumbusha wazazi wenzie kuwa, kulea sio kulipa ada tu bali na kutenga muda wa kuzungumza na kuwasikiliza watoto.

“Ndugu zangu licha ya jukumu la kutafuta pesa lakini tusisahau kuwa kuna huduma na malezi, na tunatakiwa kumpa vyote mtoto ili aweze kutimiza ndoto zake” amesema Misami.

Mwanafunzi anayehitimu darasa la saba shuleni hapo Christina Rogate amewashukuru walimu wake waliompa maarifa ya darasani na kumfunza maadili ya jinsi gani anatakiwa kuishi.

“Ndoto zangu natamani kuwa Mhasibu, nachojivunia katika Shule yangu nimeweza kutumia kompyuta, lakini pia nimefundishwa Saikolojia, maadili na nidhamu ya hali ya juu na madhara ya kujiunga na makundi mabaya” ameeleza Christina.

Wanafunzi wa darasa la saba shule ya Msingi Meccson wanatarajia kuhitimu hivi karibuni