Wakuu wa wilaya za momba na nakonde waanza kusaka wanaobadilisha fedha mtaani

Na Joachim Nyambo,Momba.
WAKUU
wa wilaya za Momba mkoani Songwe,Juma Irando  na Nakonde nchini
Zambia,Field Simwinga wamesema sasa dawa ya wabadilishaji fedha kiholela
imewafikia na kilichobaki ni kuwatibu wasiotaka kutii agizo la
Serikali.
Mkuu
wa wilaya a Momba mkoani Songwe,Juma Irando(kushoto)  na Mkuu wa wilaya
ya Nakonde nchini Zambia,Field Simwinga wakizindua rasmi matumizi ya
Shilingi na Kwacha kwenye miji ya Tunduma na Nakonde .Nyuma yao ni Mkurugenzi wa BoT tawi la Mbeya,Ibrahim Malogoi
Mkurugenzi wa Huduma za Kifedha za Benki na Mifumo ya Malipo wa 
BOT,Kamanga Lazarous wakishuhudia uzinduzi huo uliofanyika katika eneo
la kituo cha Huduma cha pamoja Tunduma.(Picha na Joachim Nyambo)

Wakuu
hao wa wilaya wamesema baada ya Uzinduzi wa matumizi ya Shilingi na
Kwacha bila kubadili kwenye miji ya mpakani ya Tunduma na Nakonde iliyo
na mzunguko mkubwa wa kibiashara,wafanyabiashara wote waliokuwa
wakifanya shughuli za ubadilishaji fedha kiholela ni wakati kwao
kutafuta shughuli nyingine.
Walisema
kwa pamoja ni muda mrefu walikuwa wakisubiri uamuzi wa Serikali na sasa
kwakuwa makubaliano yamefikiwa kwa pande zote mbili ni wakati kwao
kutumia vyombo vya ulinzi na usalama walivyonavyo kufanya kazi.
“Sisi
tulichokuwa tunasubiri ni ruhusa tu maana ni mfumo uliokuwa na kasoro
nyingi.Wananchi walikuwa wakiibiwa wakati wa kubadilisha fedha.Lakini
wabadilishaji hawa hawa ndiyo waliokuwa wanatengeneza mazingira ya
kupandisha na kushusha thamani za pesa zetu ili wapate faida zaidi.”
“Sasa
tuna imani kuwa fedha zetu zitakuwa salama.Na kwakuwa matawi ya mabenki
kwa pande zote mbili yamekwishaanza kupokea Shilingi na Kwacha
tunaamini tutakuwa salama zaidi.Wafanyabiashara wetu pia sasa
tumewafungulia uwanja mpana hapa mpakani kufanya biashara pasi woga wa
sehemu gani sahihi atapata fedha halali na akiuza wapi
atazipeleka.”alisema Irando.
Kwa
upande wake Simwinga alisema“Sasa tutapita kwenye vichochoro vyote
walimokuwa wanajificha wabadilishaji.Hakuna tutakayemuacha na niseme tu
ni wakati kwa wananchi hasa wafanyabiashara wa pande zote mbili watupe
ushirikiano ili malengo ya BoT na BoZ yaweze kufikiwa kwenye mpaka
wetu.”
Naye
Mkuu wa wilaya ya Ileje mkoani Songwe,Jonas Mkude alisema kwakuwa
changamoto zilizokuwepo kwenye mpaka wa Tunduma hazitofautiani na
zilizopo kwenye mipaka ya wilaya yake na nchi jirani ikiwemo Zambia na
Malawi ni muhimu BoT pia ikaelekeza mazungumzo ya namna hiyo kwenye eneo
lake ili kuwaondolea usumbufu wananchi hasa wafanyabiashara.
Mkude
alisema wapo wafanyabiashara ambao pia wamekuwa wakitumia mwanya wa
ubadilishaji holela wa fedha mipakani kujinufaisha kwa kuwaibia wananchi
wasio na uelewa wa kutosha.
Akijibu
hoja hiyo Mkurugenzi wa BoT tawi la Mbeya,Ibrahim Malogoi aliahidi
kulifanyia kazi suala la matumizi ya Shilingi na Kwacha ya Malawi lengo
likiwa ni kuwezesha biashara rahisi mipakani.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Kifedha za Benki na Mifumo ya
Malipo wa  BoZ,Kamanga Lazarous alisema matumizi ya Kwacha na Shilingi
kwenye miji ya Tunduma na Nakonde itachoche uchumi wa wananchi wa maeneo
hayo mawili na Mataifa husika.