Soko la Kilombero kama linavyoonekana kwa nje |
Na Mwandishi Wetu, Arusha
TANGU kulipoibuka kwa janga la
ugonjwa wa Corona nchini na kupelekea kufungwa kwa shule za Sekondari na msingi
nchini, idadi kubwa ya wanafunzi wamekimbilia katika masoko nchini wakifanya
biashara.
Kundi kubwa la wanafunzi
wanaokadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 10 hadi 15 wamekusanyika katika
masoko ya Kilombero na Soko Kuu jijini hapa wakifanya biashara ya kuuza mifuko
ya kubebea bidhaa mbalimbali za sokoni.
Mbali ya kuuza mifuko vijana
wengine wamekuwa wakitafuta ujira kwa kuelekeza maegesho ya magari ya wateja
wanaofika sokoni hapo kwaajili ya kupata mahitaji ambapo baada ya mteja kufanya
manunuzi humpatia kijana aliyemwelekeza kiasi ambacho atapendezwa nacho.
Aidha vijana hao pia wamekuwa
wakitumika kama vibega wa kubebea wateja wanaofika sokoni kwaajili ya kupata
mahitaji ya nyumbani, na kulipwa ujira wa kati ya Tsh500 hadi 2000 kwa kazi
hiyo.
Akizungumza na APC BLOG, mmoja wa
vijana hao aliyejitambulisha kwa jina la Edward Saitabau anayesoma darasa la
sita shule ya msingi Olmuringaringa anasema ameamua kufanya kazi hiyo baada ya
shule kufungwa na nyumbani kwao maisha ni magumu.
“Nyumbani maisha ni magumu, baba
hana kazi na mama pia, kwa hiyo nimeamua kuja sokoni kutafuta pesa baada ya
shule kufungwa ili nipate pesa kidogo ya kujikimu, baada ya shule kufunguliwa
lakini pia pesa nitakayoipata napeleka chakula kidogo nyumbani,”amesema.
Amesema Serikali kuamua kufunga
shule ni fursa kwake kama kijana kwa kuwa anapata nafasi ya kujitafutia fedha
ambazo zitamsaidia pindi shule zitakapofunguliwa kununulia mahitaji ya shule
kama daftari, viatu na sare za shule.