Wwananchi sasa kujipima virusi vya ukimwi – waziri ummy

*****************************
Na Rayson Mwaisemba, WAMJW- Katavi.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu leo amesema kuwa bunge
la Tanzania limerasimisha sheria ya Wananchi kuweza kujipima wenyewe
maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).
Waziri Ummy amesema hayo leo
Disemba 20 katika ziara ya kukagua hali ya utoaji wa huduma za Afya na
ujenzi wa miundombinu ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi, ikiwa ni
jitihada za Serikali za kuboresha huduma za Afya nchini.
“Napenda kuwapa Habari njema kuwa
Bunge la Mwezi wa 11 limepitisha Sheria, kwahiyo sasa ni rasmi Tanzania
mtu kujipima maambukizi ya VVU mwenyewe, kwahiyo hivi vitendanishi
(vifaa) vitakuwa vinauzwa kwenye maduka, pia kugawa bure baadhi ya
maeneo kwa sababu wakati mwingine watu wanaona unyanyapaa kwenda kupima
wenyewe,” Amesema Waziri Ummy.
Ameendelea kusema kuwa, Serikali
imeweka angalizo kuwa, kujipima mwenyewe sio majibu ya mwisho, hivyo
kuwataka wananchi kuwa, baada ya kujipima wanatakiwa kwenda katika vituo
vya kutolea huduma za Afya kwa ajili ya kuthibitisha na ushauri zaidi
wa jinsi ya kuishi.
Aidha, Waziri Ummy ameagiza
kuendelea kutoa elimu ya Afya kwa wananchi, hususan watu wanaoishi na
virusi vya Ukimwi kutumia dawa kwa usahihi kulingana na maelekezo ya
Watoa huduma za Afya katika vituo vya kutolea huduma za Afya nchini.
“Tuendelee kuhakikisha watu wote
waliobainika na ugonjwa wa Ukimwi, waendelee kutumia dawa kwa usahihi
kama walivyoelekezwa na Wataalamu wetu katika vituo vya kutolea huduma
za Afya nchini”. amesema Waziri Ummy.
Mbali na hayo, amesema kuwa kuna
changamoto ya maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi kwa vijana wenye
umri kati ya miaka 15 mpaka 24, huku akiweka wazi kuwa kitaifa hali ya
maambukizi mapya kwa vijana hao ni asilimia 40%, huku vijana wa kike
ikiwa ni asilimia 80 na wakiume ikiwa ni asilimia 20.
Kwa upande mwingine Waziri Ummy
amewatia moyo wanaoishi na maambukizi ya VVU kwa kuwakumbusha kuwa,
kuhudhuria katika vituo vya Afya na kufuata maelekezo kama walivyopewa
na Watoa huduma, pia kuishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi sio
mwisho wa maisha.
“Niendelee kuwatia moyo kuwa na
maambukizi ya Ukimwi sio mwisho wa Dunia, sio sentensi ya kifo, sikuhizi
watu Wanaishi vizuri, kwahiyo nawahimiza kwenda kwenye vituo vya
kutolea huduma za Afya, kupima na kuanza kutumia dawa”. Amesema Waziri
Ummy.
Nae Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Katavi,
ambae pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Bi Lilian Matinga amesema kuwa,
hali ya upatikanaji wa dawa ipo vizuri Mkoani hapo, huku akidai kuwa kwa
mwaka 2017/2018 bajeti ya dawa na vitendanishi ilikuwa Bilioni 2.9 na
kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Mkoa umetengewa jumla ya shilingi Bilioni
3.97 ikiwa ni ongezeko la shilingi Milioni 460.07.
Aliendelea kusema kuwa, kwa sasa
hali ya upatikanaji wa dawa muhimu ni zaidi ya asilimia 90% katika vituo
vyote vya kutolea huduma za Afya nchini. alisisitiza.