Wananchi watakiwa kuchangia sekta ya elimu kahama

Mwalimu Bukuru Robert wa shule ya Msingi
Mtakuja akiwafundisha wanafunzi wa darasa la pili somo la Kiswahili
katika darasa ambalo linawanafunzi zaidi ya 50 huku wengine wakiwa
wamekaa chini kwa kukosa madawati.
Na Salvatory Ntandu – Kahama
Katika jitihada za kukabiliana na tatizo la uhaba wa vyumba vya
madarasa, matundu ya vyoo na madawati katika shule za msingi na
sekondari katika halmashauri ya Mji wa Kahama mkoani Shinyanga, jamii
imetakiwa kuchangia shughuli za maendeleo hususani sekta ya elimu ili
kutatua kero hiyo inayosababisha wanafunzi kukosa masomo.
Wito huo umetolewa Febuari 3,2020 na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi
(CCM) Thomas Myonga katika ziara ya siku mmoja ya kukagua miradi ya
maendeleo iliyotekelezwa na halmashauri hiyo katika kipindi cha miaka
mine ya serikali ya awamu ya Tano.
Alisema tatizo la wanafunzi kukosa vyumba vya madarasa na madawati
linachangiwa na wananchi kutochangia shughuli za maendeleo ikiwemo
ujenzi wa madarasa, vyoo na madawati jambo ambali linasababisha
wanafunzi kushindwa kusoma vizuri.
“Nimetembelea shule ya msingi mtakuja yenye wanafunzi 2467 yenye vyumba
vya madarasa 12 ambayo hayatoshi na baadhi ya wanafunzi wanasomea wakiwa
wamekaa chini nimebaini wazazi na wananchi wa eneo hili hawajachangia
ujenzi wa madarasa”,alisema Myonga.
Myonga aliwataka wakazi wa mtaa wa mtakuja na kata ya Nyahanga kuchangia
ujenzi wa madarasa pamoja na madawati ili kuondoa tatizo la wanafunzi
kusomea wakiwa wamekaa chini sambamba na kusoma kwa awamu jambo ambalo
linasababisha washindwe kufanya vizuri katika masomo yao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Kahama
Anderson Msumba  aliwataka watendaji wa kata mitaa na vijiji
kuwahamsisha wananchi kujenga maboma ya madarasa katika maeneo ambayo
yanachangamoto ili halmashauri iweze kuyakamilisha na kuondoa tatizo
hilo.
“Viongozi wa serikali za mitaa na vijiji shirikianeni na wataalamu wangu
kuhamasisha wananchi kuchangia katika sekta ya elimu ili kuondoa
changamoto zinazowakabili wanafunzi wetu kwa kukosa vyumba vya
madarasa,madawati na matundu ya vyoo”,alisema Msumba.
Alisema mwitikio wa wazazi kupeleka wanafunzi shule umekuwa mkubwa baada
ya serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli
kutoa elimu bure kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne na
kusababisha shule nyingi kukabiliwa na changamoto hizo.
Kamati ya siasa ya wilaya ya Kahama inaendelea na ziara ya siku mbili
katika halmashauri ya Mji wa kahama katika utekelezaji ilani ya CCM
sambamba na Maadhimisho ya miaka 43 ya CCM yanakwenda na kauli mbiu
isemayo “tumeahidi,tumetekeleza na tunaahidi tena kuchapa kazi kwa
juhudi,ubunifu na maarifa zaidi”.