Wanaume zaidi ya milioni 4 wafanyiwa tohara nchini


Katibu Mkuu Dkt. Zainab Chaula akifafanua jambo wakati wa semina hiyo



Wabunge wa Kamati ya Bunge ya
masuala ya Ukimwi, Kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na Maendeleo ya
Jamii pamoja na kamati ya  Katiba na Sheria walioshiriki semina ya
kujengewa uelewa wa masuala ya mpango wa taifa wa kudhibiti UKIMWI


Wabunge walioshiriki semina hiyo iliyohusu masuala ya UKIMWI 




Na Catherine Sungura -Dodoma


JUMLA ya wanaume milioni 4,456,511
wamefanyiwa tohara kinga ya kitabibu tangu 2009 ilipoanza kutolewa hadi
kufikia Septemba, 2019.


Hayo yamesemwa na Afisa Mpango
kutoka Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (NACP), Dk. Sasan Mmbando
wakati wa semina ya kuwajengea uelewa wabunge wa Kamati ya Bunge ya
masuala ya Ukimwi, Kamati yabkudumu ya Bunge ya huduma na Maendeleo ya
Jamii pamoja na kamati ya Katiba na Sheria kuhusu mpango huo.


Dk. Mmbando alisema kuwa lengo la kwanza la afua hiyo lilikuwa kuwafikia wanaume na vijana milioni 2.8 kufikia Septemba, 2017.


“Hadi kufikia Septemba, 2017 tumeweza kuwafikia milioni 3,303,940 na kuwatahiri,” alisema.


Aidha, alisema katika lengo la pili kuanzia mwaka 2017 hadi 2022 wana mpango wa kuwafikia wanaume milioni 2.7.


Alisema hadi kufikia Septemba,
2019, tayari wameweza kuwatahiri jumla ya wanaume 1,681,070 ikiwa ni
sawa na asilimia 60 ya lengo.


Alisema afua hiyo inatekelezwa katika mikoa 17 yenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya HIV na kiwango kidogo cha utahiri nchini.


“Hata hivyo, Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ili kuwa na huduma endelevu
na kupunguza matatizo ya njia ya mkojo, mfano UTI, ilianza kutoa huduma
ya tohara kwa watoto wachanga wenye umri kuanzia siku moja hadi 60,
2013, kama utafiti wa kujifunzia (pilot study), katika mkoa wa Iringa
hadi sasa imefikia mikoa 15 nchini,” alibainisha.


Alisema hadi kufikia Septemba, 2019 jumla ya watoto wachanga 13,603 wametahiriwa.

“Tohara ya watoto wachanga
inafanyika katika mikoa 15, Iringa Njombe, Morogoro, Singida, Tabora,
Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita, Kagera, Rukwa, Katavi, Songwe, Mbeya
na Kigoma,” alisema.