Watatu kizimbani kwa kukutwa na tausi wa ikulu

Watu
watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisitu wakikabiliwa
na mashtaka matano likiwemo la  kukutwa na ndege watatu aina ya tausi
waliokuwa Ikulu wenye thamani ya zaidi ya Sh3.4milioni.

Washtakiwa hao wanaokabiliwa na kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 116/2019 ni David Graha, Mohamed Hatibu na Mohamed Ally.


Mbele ya Hakimu Mkazi, Vick Mwaikambo, Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi alisema 
Juni Mosi 2015 na Oktoba 14, mwaka huu jijini Dar es Salaam, washtakiwa
walijihusisha na mtandao wa uhalifu ambapo wanadaiwa kuratibu genge la
uhalifu wakijihusisha na biashara ya ndege aina ya Tausi bila kibali cha
Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Katika
shitaka la pili, Nchimbi amedai katika tarehe hizo washitakiwa
walikutwa na ndege watatu aina ya tausi wenye thamani ya USD 1,500
ambazo ni sawa na Sh milioni 3.4 mali ya serikali bila kuwa na kibali.

Pia
Oktoba 14, mwaka huu maeneo ya Mikocheni jijini Dar es Salaam,
mshtakiwa Ally alikutwa na ndege watatu aina ya Tausi wanaopatikana
Ikulu, ambao aliwapata kwa njia zisizo halali huku katika shtaka la
tano, washtakiwa i Graha na Hatibu katika tarehe hizo hizo walijipatia
Sh 300,000 huku wakijua fedha hizo ni mazalia ya kosa la wizi.

Hata
hivyo, washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama
hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi.

Kwa
mujibu wa upande wa mashtaka, upelelezi wa shauri hilo bado
haujakamilika hivyo waliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na
kuzingatia kwamba mashitaka hayo hayana dhamana.

Kesi
hiyo imeahirishwa hadi Novemba 7 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na
washitakiwa walirudishwa rumande kwa sababu mashitaka hayo hayana
dhamana.