Watoa huduma za afya washauriwa kutumia vipimo vya viwango vya kitaifa na kimataifa kulinda afya za watanzania

 

Kaimu
Katibu tawala wa Mkoa wa Mbeya Bi. Mwajabu Nyamkomora akifungua semina
ya umuhimu wa vipimo katika sekta ya afya iliyofanyika katika ukumbi wa
Dr. Shein jijini Mbeya mapema leo.

Nyamkomora alitoa wito kwa watoa huduma za afya,madaktari,wauguzi
na watu wa maabara kulinda afya za Watanzania kwa kuzingatia upimaji
sahihi, kufuata miongozo pamoja na viwango vya kitaifa na kimataifa .

Mkuu wa Maabara ya Ugezi Bw.James
Mahilla akizungumza na washiriki wa semina ya umuhimu wa vipimo katika
sekta ya afya iliyofanyika katika ukumbi wa Dk. Shein jijini Mbeya.

Mahilla alisema ili kuenzi siku ya vipimo duniani,TBS imeandaa
semina kwa lengo la kutoa uelewa kwenye masuala ya sayansi ya Vipimo
hususani katika sekta ya Afya

Meneja wa Kanda Nyanda za juu
kusini Bw.Abel Mwakasonda akizungumza na washiriki wa semina ya Umuhimu
wa Vipimo katika sekta ya afya iliyofanyika katika ukumbi wa Dk. Shein
Jijini Mbeya mapema leo.

Mwakasonda alisema TBS kwa kushirikiana na taasisi zingine zenye
dhamana ya kushughulika na vipimo zimejipanga kuhakikisha kila mtoa
huduma katika sekta ya afya anapata uwezo wa kutoa huduma kwa kuzingatia
vipimo sahihi.

Washiriki wakiwa katika semina ya
Umuhimu wa Vipimo katika sekta ya afya iliyofanyika katika ukumbi wa Dk.
Shein Jijini Mbeya mapema leo.

Watoa huduma katika sekta ya afya
na wadau wote kila mmoja kwa nafasi yake wametakiwa kuchukua hatua
stahiki kwa pamoja kuhakikisha wanalinda afya za Watanzania kwa
kuzingatia upimaji sahihi, kufuata miongozo na viwango vya kitaifa na
kimataifa.

Wito huo umetolewa leo Mei 27 2021
na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Mwajabu Nyamkomora, katika
semina iliyoandaliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa lengo la
kutoa uelewa kwenye masuala ya Sayansi ya Vipimo hususani katika sekta
ya afya kwa wadau.

Semina hiyo ni sehemu ya mwendelezo
wa maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani yaliyofanyika Mei 20, mwaka
huu kitaifa mkoani Dodoma, kauli mbiu ikiwa na ujumbe usemao; “Umuhimu
wa Vipimo Katika Sekta ya Afya.”

Nyamkomora alisema vipimo ni huduma
muhimu sana katika utoaji wa huduma za afya na uzalishaji wa dawa
katika viwanda vyetu, kwani Taifa ambalo watu wake hawana afya, haliwezi
kuzalisha.

Aliongeza pia ni muhimu watoa
huduma za afya, madaktari, wauguzi na watu wa maabara, watoe huduma kwa
kuzingatia viwango, miongozo ya Serikali, weledi, kujituma na kufanya
kazi kwa bidii na kwa kukumbuka viapo vyao.

“Lakini pia tutambue kuwa uhai na
ustawi wa taifa letu upo katika mikono yenu (watumishi wa afya) hivyo
wafanye kazi kwa bidii,” alisema, Nyamkomora.

Mgeni huyo rasmi, Nyamkomora
aliwataka watoa huduma katika sekta ya afya kujitathmini kama wanatoa
huduma ya vipimo inayokidhi viwango.

“Tujikague kwa kujiuliza maswali.
Je, una elimu, ujuzi na maarifa ya kutosha kutumia vifaa unavyotumia
katika upimaji, je, hali ya vifaa unavyovitumia inaruhusu kufanya
vipimo? Je, tunafuata ushauri wa kitaalamu kuhusu matumizi, utunzaji,
matengenzo ya muda na yale ya baada ya hitilafu kwa vifaa tunavyotumia?”
Alihoji, Nyamkomora na kuongeza;

“Mtoa huduma anatakiwa kujiuliza
kama kifaa chako kimehakikiwa kwa usahihi wake wa kutoa majibu sahihi?
Je, umefanya ugezi (Calibration) kwenye vifaa vyako?

Unatumia cheti cha ugezi kutoka kwa
aliyekupa huduma hiyo? je,aliyekupa huduma ya ugezi ana weledi wa kazi
anayofanya na je mfumo wa kuhakiki majibu yanayotoka ni sahihi?”

Alisema ni muhimu kila mmoja kwa
nafasi yake akachukua hatua stahiki ili wote kwa pamoja tuhakikishe
wanalinda afya za Watanzania kwa kuzingatia upimaji sahihi, kufuata
miongozo na viwango vya kitaifa na kimataifa.

Alisema ni matumaini yake kuwa baada ya semina hiyo kila mmoja kwa
nafasi yake atachukua hatua stahiki ili wote kwa pamoja tuhakikishe
tunalinda afya za Watanzania.

Kwa upande wa Meneja wa TBS Kanda
ya Nyanda za Juu Kusini, Abel Mwakasonda, alisema vifaa vinavyotumika
katika uchunguzi wa afya vina mchango mkubwa katika kuhakikisha ugonjwa
ambao mtu anaugua.

Aliwataka wamiliki na waendeshaji
wa hospitali, maabara za afya, viwanda vya kuzalisha dawa na taasisi
zinazosimamia sekta ya afya kutambua kuwa huduma bora za afya
zinawezekana tukizingatia ubora wa vipimo vyetu.

Alisema mtoa huduma katika sekta ya afya anapata uwezo wa kutoa huduma kwa kuzingatia vipimo sahihi.

“Vipimo sahihi ni huduma muhimu
sana katika utoaji wa huduma bora za afya, nawashauri wamiliki wa
viwanda, hospitali, vituo vya afya, maabara za uchunguzi na watoa huduma
wote wa sekta ya afya mtumie vipimo sahihi kwa wakati sahihi na kupata
huduma ya ugezi wa vifaa (mashine zinazotumika kupimia ama kutunzia
sampuli zenu kutoka katika Taasisi zinazofanya vipimo kwa usahihi ili
muweze kutoa huduma bora kwa Watanzania,” alisema Mwakasonda na
kuongeza;

“Vipimo sahihi ni kiwezeshi cha utoaji wa huduma bora na salama. IIi kuenzi siku ya Vipimo Duniani.”

Kwa upande wa Mkuu wa maabara ya
ugezi Bw.James Mahilla alisema TBS kupitia Maabara ya Vipimo
(Metrolojia) ndiyo watunzaji wa Viwango vya Taifa vya Vipimo.