#Kigogo asiyejulikama awatumia kama fursa ya kujipatia kipato
#Awapatia viti mwendo, msukumaji, wazazi waridhia
Egidia Vedasto APC Media.
Haki za watoto wenye ulemavu katika jiji la Arusha zimeendelea kuvunjwa kwa kutumika katika biashara ya kuomba mitaani huku ikidaiwa kuwepo mtu nyuma yao anayewafadhili.
Inadaiwa mfadhili huyo huwatoa mikoani na kuwaleta mjini na kisha kuwapatia malazi, viti mwendo na kuwatumia wazazi wa watoto hao mshahara kila mwisho wa mwezi.
Ulemavu ni hali inayotokana na dosari mwilini au akili ambayo
inasababisha mtu kushindwa kutenda mambo ambayo kwa kawaida
angetegemewa kuyaweza, hivyo kumletea mtu huyo kizuizi katika
utekelezaji wa majukumu yake katika jamii.
Licha ya ulemavu wa aina yoyote kwa mtoto lakini bado anastahili
kupata huduma maalum ya matibabu, nafasi sawa ya elimu na mazoezi pale
inapowezekana ili kumsaidia kufikia malengo yake ya maisha.
Katika mahojiano kwa nyakati tofauti baadhi yao wamesema wanatokea mikoa ya kanda ya ziwa Simiyu, Shinyanga pamoja na Mwanza, huku wakionyesha kufurahia maisha ya mjini yanayowapatia pesa bila kufanya kazi ngumu tofauti na maisha ya kijijini yaliyotegemea zaidi kilimo.
APC Media imefanya uchunguzi wa kina na kubaini kuwa watoto hao licha ya kufanya kazi hiyo katika mazingira magumu ya jua na mvua, lakini anayefaidi zaidi ni mtu anayewafadhili pamoja na msaidizi wake kwa maana anayemsukuma kwenye kiti mwendo.
Hata hivyo bado kuna dhana potofu katika jamii ikiaminiwa kuwa mtoto mwenye ulemavu ni kikwazo na mkosi katika, lakini ifahamike kuwa, mtoto huyo akipewa haki sawa na watoto wengine anaweza kufikia ndoto zake na kufurahia maisha.
Kijana Antony (17) siyo jina lake halisi anayefanya kazi ya kutoa msaada wa kumsukuma Mtoto wa miaka (6) mwenye ulemavu wa kutoongea wala kusimama anaeleza alikotokea na namna anavyoishi mjini kwa sasa.
“Nimetokea Simiyu, huyu ni mdogo wangu hawezi kuongea wala kusimama, mama yetu anaishi Lamadi mkoa wa Simiyu, tunaishi hapa mjini kati, hiyo sehemu tunapoishi wapo wengi tu wenye ulemavu” amesema Antony.
Katika maelezo ya kijana huyo yalitawaliwa na wasiwasi mwingi kwani hakutaka kujulikana anaishi eneo gani, licha ya kwamba inasemekana wengi wanaosaida kuwasukuma watoto hao siyo ndugu zao wa damu, hatua ambayo pia inaleta mashaka juu ya usalama wao dhidi ya ukatili wa kingono.
Malengo ya Maendeleo Endelevu yanahimiza kuwa hakuna mtoto anayepaswa kuachwa nyuma, lakini utafiti uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) unaonesha kuwa kati ya watoto milioni 240 wenye ulemavu duniani, nusu hawajawahi kuhudhuria shule, takriban theluthi moja hawapati chakula bora na cha kutosha, na wanawakilishwa kwa njia isiyo sawa na wengi wao wanaachwa nyuma.
UNICEF inadhamiria kuhakikishia kuna ujumuishaji wa watoto wote wenye ulemavu katika elimu, afya, majibu ya dharura, ulinzi wa kijamii, familia na maisha ya jamii.
Hii imetokana na dhamira hiyo, katika Mkutano wa Kimataifa wa Watu wenye Ulemavu 2022, UNICEF inajitolea kutoa ushahidi mpya kupitia utafiti, kuanzisha ajenda ya utafiti wa kimataifa na jukwaa kwa watoto wenye ulemavu ili kuhakikisha wanajumuisha ulemavu katika tafiti zote na kuongeza uwekezaji katika ujumuishaji kwa watoto.
Mashuhuda wazungumza
Mmoja wa watu wenye ulemavu ambaye hakutaka kutaja jina lake aliyekutwa maeneo ya soko la Kilombero jijini Arusha, amesema, “Mimi nimeolewa nina watoto (2) kabla ya kuja hapa Arusha nilikuwa nikiishi na mume wangu, lakini jamii yetu ilinidhihaki na kunibeza, kila wakati walimwambia mume wangu kuwa ameoaje mwanamke wa aina hii” amesema na kuongeza.
“Tangu nimekuja hapa mjini nashukuru maana hakuna mtu anamuangalia mwenzake, hapa kila mmoja anafanya shughuli zake na ninafurahia maisha kwani nakula vizuri, nalea watoto wangu, na kutuma pesa za shamba kwa mume wangu”
Amesema kwa upande wao watu wazima wenye ulemavu hakuna changamoto kwa sababu wanajitambua, lakini watoto wadogo changamoto kubwa ni kudhulumiwa fedha zao, kukosa watu wa kuwahudumia chakula na usafi pamoja na kukosa uangalizi.
Ameongeza kuwa, wengi wa watoto hao huchukuliwa kutoka vijijini kwa wazazi wao na kuja mjini kutumikishwa kuombaomba ili kuingiza kipato kwa familia.
“Siwezi kujua nani anawachukua kutoka kwa wazazi wao lakini nasikia watoto wengi wenye ulemavu wanatokea Kanda ya Ziwa, wazazi wao hulipwa shilingi 50,000 hadi 100,000 kila mwezi kama mshahara na watoto hao wakihifadhiwa katika nyumba za kulala wageni (guest) na wengine kupangishiwa vyumba na kupewa viti mwendo” amebainisha.
“Si unajua shughuli za wasukuma ni kilimo, sasa mzazi anaangalia mtoto hatembei na hajiwezi kwa chochote, inakuwa ni usumbufu maana hawezi kufanya kazi zake za kilimo kwa uhuru, hivyo anaona bora mtoto aende awe huru na apate huo mshahara kupitia huyo mtoto” amesema na kuongeza,
“Sasa wewe jiulize, unamuona yule mtoto pale miaka yake haifiki minne cha kushangaza wazazi wake hawapo hapa Arusha, wapo kijijini wanasubiri mwisho wa mwezi walipwe kupitia huyu mtoto, hii ni hatari zaidi kwa sababu akifanyiwa vitendo vibaya hana wa kumsaidia, bora yetu sisi watu wazima tunaweza kujipambania kusema ndiyo au hapana” ameeleza
Uchunguzi wa APC Media umengudua idadi kubwa ya ombaomba hao wanaishi Kata ya Ungalimited huku ikisemekana kuwepo na mfadhili nyuma yao, siri ambayo serikali inatakiwa kuhakikisha inaifichua na kukomesha uovu huo mkubwa.
Ni mwaka mmoja sasa tangu gazeti la Jamhuri lilipoti utumikishwaji wa kingono kwa watoto ombaomba Jijini Arusha, lakini hadi leo hii vitendo vinazidi kuongezeka maradufu hali inayochafua taswira ya jiji la kitalii la Arusha.
Hata hivyo baadhi ya watoto waliohojiwa kuhusiana na uwepo wa vitendo vya ukatili wa kingono wamekana na kudai hata kama vipo basi vinafanyika kwa makubaliano.
Mwanasheria Richard Manyota amesema kwa mujibu wa sheria ya mtoto kifungu na.16 ya mwaka 2014 wazazi kwa maana ya baba, mama au mlezi ni kosa la kisheria kutelekeza na kutomlea mtoto.
Ameendelea kufafanua kuwa mtoto anaangaliwa kwa mujibu wa sheria, na kwa maslahi mapana bila kujali uwezo wa kifedha.
Amemtaja Afisa ustawi wa jamiii kuwa ndiye mwenye uwezo wa kwenda mahakama ya watoto na kufungua maombi maalum ya kuomba mahakama imuamrishe aidha mzazi au mlezi kufanya jukumu la kumlea mtoto na iwapo hatawajibika, Afisa ustawi wa jamii ataomba amri mahakamani ili kumuondoa mtoto mikononi mwa mzazi au mlezi na kumpeleka katika taasisi maalum ya malezi.
“Ni kweli kwa sasa kuna wimbi kubwa la watoto wenye ulemavu wenye umri kati ya miaka 4-10 wanaokaa kando ya barabara au wakitembea katikatika ya barabara wakifanya shughuli za kuombaomba, baadhi wakitembezwa kwenye vitimwendo na wengine wakiwatembeza watu wazima.
“Sheria ipo wazi, ni kosa la jinai la sheria ya usalama barabarani, maana sheria inamtambua askari wa usalama barabarani pekee, kuwa ndiye anayeweza kukaa katikati ya barabara akiongoza magari, hivyo watoto hao wanapaswa kuondolewa kwa sababu ya kukaa katikati ya barabara ni kosa na hatari Kwa usalama wao”
“Ni ngumu kumshitaki mtoto kwa kosa la kusimama na kuomba pesa barabarani, kuna taarifa kwamba kuna watu wanaowatumia watoto kuomba ili wajinufaishe, inasadikiwa kwamba wanahifadhiwa Kata za Sekei, Ngarenaro, Ungalimited na maeneo mengine ya jiji la Arusha”
“Mwaka huu mwezi Juni kulikuwa na kesi Mahakama Kuu, Mahakama iliwafunga watu watatu, wanawake wawili na mwanaume mmoja kila mmoja kifungo cha miaka saba jela pamoja na faini ya shilingi milioni tano kwa kila mmoja pale watakapomaliza kutumikia kifungo, watuhumiwa wawili kati yao walitokea Mwanza na mwanamke mmoja alitokea Arusha ambaye alifanya kazi ya kuwatafutia vyumba vya kuishi watoto ombaomba”
“Watu hao walikuwa wanawalaghai watoto kwamba watawapeleka shule, lakini baada ya kuwafikisha mjini waliwambia wajifanye walemavu na kuanza kazi ya ombaomba ili wajinufaishe, watoto waliotoa ushahidi na kuwafichua waharifu walionekana wasioona na wengine walemavu kumbe siyo” ameeleza Wakili Manyota.
Pia amefafanua kwamba, sheria ya mtoto inamtaja askari polisi, wazazi na afisa ustawi wa jamii kuangalia suala la mtoto kwa mustakabali wa maisha yao, na iwapo watoto watakamatwa na kupelekwa polisi bila kufikishwa mahakamani kunakosekana nguvu ya sheria kwa afisa ustawi wa jamii kufanya kazi yake kwa usahihi.
Naomi Kimaro anayefanya kazi katika shirika la kuokoa watoto wanaoishi mazingira magumu la Amani Centre linalofanya kazi zake katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Singida, amesema watoto wenye ulemavu wanaofanya shughuli za ombaomba wanaongezeka kila kukicha hususan katika barabara kuu za jiji la Arusha.
“Hii naiona kama sababu ya kuchangia kudorora kwa elimu kwa mtoto, kwa mfano suala jingine ni pale mtoto akitoka na mzazi au mlezi ambaye ni mlemavu, mzazi anamtumia mtoto kama kiongozi wake wakiwa barabarani, hivyo ni lazima ashinde naye kutwa nzima, hivyo ni ngumu mtoto huyo kupata haki yake ya elimu”,
“Sisi shirika letu tuna maafisa ustawi wa jamii, wanaofuatilia mitaani usiku na mchana kubaini watoto wanaoishi mazingira magumu, ambapo wakipatikana tunatafuta familia zao ili kujua shida ipo wapi, baada ya hapo tunahakikisha kama mtoto ameacha shule anarudishwa au kuanza masomo ya elimu ya watu wazima kama hajawahi kwenda shule” amesema Naomi.
Ameshauri kuwa, serikali iweke sera mahususi za namna ya kukomesha utumikishwaji wa watoto wenye ulemavu, jamii kutumia njia za uzazi wa mpango ili kupanga idadi ya watoto watakaoweza kuwalea.
Pia amewashauri wazazi kuzungumza na watoto na kuwalea katika misingi bora bila kujali hali ya mtoto wake, pia serikali kuziunganisha kaya zenye watoto wenye ulemavu na TASAF ili kuwasaidia wazazi hao kuhudumia familia zao.
“Mwaka jana tuliletewa mabinti wawili wenye ulemavu, baada ya kuwapokea tuliwasiliana na afisa ustawi wa jamii ili awasiliane na afisa ustawi wa jamii wa huko walipotokea, walieleza wametokea Kanda ya Ziwa, baada ya kuwajulisha kuwa kituo chetu hakihudumii watoto wenye ulemavu, walianza kufanya mazoezi ya kutembea na hatimaye walitembea vizuri, ndipo tukagundua kuwa hawana ulemavu licha ya kwamba walifikishwa ofisini kwetu wakiwa na viti mwendo, hii ilitupa picha kuwa, wengi wanajifanya walemavu ili wapate pesa lakini sio walemavu” amebainisha Naomi.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju amesema utumikishwaji wa watoto wenye ulemavu haukubaliki, ni kinyume cha sheria namba 9 ya mwaka 2010, pia kitendo hicho kinakinzana na sheria za nchi.
“Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakataza utumikishwaji wa namna yoyote ile ambao unalenga kumbagua au kumnyanyapaa, na sheria ya mtoto inazuia utumikishwaji kwa lengo la mtu kujiingizia kipato na ni kosa la jinai, mtoto akiwa na ulemavu isiwe sababu ya kugeuzwa kitega uchumi” amefafanua Mpanju.
Hata hivyo Mpanju amesema kuwa, suala hilo ni vema lizungumziwe na ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuwa ndiyo wenye ufafanuzi na mikakati ya kupambana na suala hilo, amesema amelizungumzia kidogo kwa sababu limehusisha watoto.
Kizunguzungu kuwapata viongozi ngazi ya Mkoa na Halmashauri
Mwandishi wa chombo hiki alifanya jitihada za kumpata Mkurugenzi wa watu wenye ulemavu Ofisi ya Waziri Mkuu, ambapo baada ya kupatikana ametoa maelekezo atafutwe afisa ustawi wa jamii mkoa wa Arusha.
Afisa Ustawi wa Jamii ngazi ya mkoa alitoa maelekezo kwa afisa ustawi wilaya kuzungumzia suala hilo kwa takwimu na mikakati iliyopo na namna ya kulikabili suala hilo, lakini simu yake haijapokelewa kwa siku mbili mfulizo.
Diwani wa Kata ya Ungalimited Mahmoud Said Omary ambaye idadi kubwa ya watu wenye ulemavu wanaoomba wanakaa katika kata yake, amesema Baraza la Madiwani limeweka mikakati ya kuzitaka idara zinazohusika na ustawi wa jamii kushughulikia suala hilo.
Ameongeza kwamba, watu wenye ulemavu wanaofanya shughuli za kuomba jijini humo wanaishi mazingira magumu hasa kipindi cha mvua kutokana na tishio la kupata magonjwa ya kifua na yale ya kuambukiza.
“Ni kweli kuwa kuna mtu nyuma ya kundi la watoto na watu wazima wenye ulemavu wanaofanya shughuli za kuombaomba, lakini naamini kwa mkakati huu uliowekwa tatizo hili litapata ufumbuzi, na ninashauri jitihada zisifanywe na wilaya wala mkoa, bali ziwe za kitaifa, ili tuweze kuondokana na vitendo hivyo”
“Ukweli watoto wenye ulemavu wanatumikishwa na wanateseka sana, kwa mfano kipindi hiki cha mvua mtoto anaamshwa usiku kuwahi magari ya kwenda Moshi mjini au soko la Sadala lililopo wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro ili wakaombe, unakuta mvua na baridi vinamuishia mwilini, wakati huo mzazi yupo mkoani anasubiri ujira kupitia kwa huyo mtoto, matokeo yake anayenufaika ni mtu aliyepo nyuma ya mtoto kwa maana aliyemchukua kutoka kijijini” ameeleza Mahmoud.
Aidha ameelezea mazingira wanayoishi katika nyumba zao, kwamba watoto huwekwa kati ya wanne hadi watano kwenye chumba kimoja, huku wakilalia na kujifunika turubai na wanaolalia godoro hulala watu wanane hadi kumi kwenye godoro moja hali inayohatarisha usalama wa afya zao na hatua hiyo kuchangia vitendo vya ukatili ikiwemo ubakaji na ulawiti.
“Ikumbukwe watu wanaotumikisha watu wenye ulemavu wana pesa sana, kwa sababu ya mtandao mkubwa uliopo, ukienda Zanzibar wamejaa, na sasa wamefika Mombasa, hali hii inachafua taswira ya nchi yetu, nashauri uwekwe mkakati wa kitaifa wa kumaliza ombaomba mitaani ambayo kwa hapa Arusha imeshamiri” amefafanua Diwani Mahmoud.
kikao cha Ushauri cha Mkoa (RCC) kimekiri kuwa tatizo hilo ni la muda mrefu na kuweka mikakati ya kuwafuatilia ili kuweza kubaini wanakotoka na kisha kuwaondoa.
Mkuu wa Wilaya ya Karatu Dadi Kolimba akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda, katika kikao hicho amesema suala hilo limewekewa mkakati kwa maafisa ustawi wa jamii na maafisa maendeleo ya jamii kuhakikisha wanatumia mbinu zao kuwafuatilia walemavu hao ili kujua uhalisia kwa lengo la kumaliza tatizo hilo.
*****************