Wauzaji na wanunuzi wa madini ya vito Mirerani wahakikishiwa usalama

Seif Mangwangi, APC Media,

Manyara

Waziri wa madini Antony Mavunde amewahakikishia wauzaji na wanunuzi usalama wa madini na pesa zao, wakati akizindua minada ya ndani ya vito iliyofanyika leo katika eneo la madini Mererani Manyara, iliyowakutanisha wadau wa madini kutoka ndani na nje nchi.

Mavunde amewatoa hofu na hisia mbaya wananchi juu serikali, kwamba haitaingilia biashara hiyo, kwa maana ya kuchukua mdini yatakayobaki baada ya mnada, na kuahidi kuwarudishia wafanyabiashara madini yaliyobaki katika mnada wa 2017 na kupelekwa benki kuu, ili wamiliki wa madini hayo waweze kuendelea na biashara zao.

Waziri wa Madini Anthony Mavunde akizungumza wakati wa uzinduzi wa mnada wa madini ya vito Mirerani wilayani Simanjiro, Manyara

Aidha amesema, mnada huo ni chachu ya kukuza maendeleo na kukuza pato la taifa, sambamba na serikali kujipanga kudhibiti na kuzuia utoroshaji wa madini kwa ushirikiano wa tume ya madini na soko la bidhaa Tanzania (TMX) kupitia mfumo wa mauzo wa kielekitroniki ili kuweka uwazi kwa wadau wote wa madini.

“Niwahakikishie kuwa serikali inaendelea kuchukua hatua kuhakikisha tunarudisha hadhi ya Tanzanite na kushindana kimataifa, sifa ya madini vito ni uadimu, tutahakikisha thamani yake inalindwa ili wafanyabiashara wadogo kwa wakubwa pamoja na wachimbaji wananufaika” amefafanua Mavunde.

Mavunde ameongeza kuwa, sekta ya madini inaendelea kukua na kuongeza fedha katika mfuko mkuu wa serikali, kutoka shilingi bilioni 161katika mwaka wa fedha 2015/2016 hadi kufikia shilingi bilioni 753, huku ikitazamiwa kufikia lengo la kukusanya trilioni 1 kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Waziri wa Madini Anthony Mavunde na Viongozi wengine katika uzinduzi wa minada ya Madini Mererani Mkoani Manyara

Mwenyekiti wa tume ya Madini Janeth Reuben Lyakashingo, amesema wizara ya madini kupitia tume ya madini inalenga kuboresha mfumo wa usimamizi wa biashara ya madini ya vito, kwa kuanzisha minada ya ndani na kimataifa ya madini ya vito.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa Manyara Queen Sendiga ameiomba serikali kukamilisha soko la madini ambapo kiasi cha bilioni 5.4 zimetolewa, amesema jengo hilo likikamiika shughuli zote zitafanyikia huko, kuchakata na kuhakikisha madini hayo yanakuwa tayari kutumika.

Ameongeza kwa kuiomba serikali kukamilisha zahanati yenye ukubwa wa hadhi ya kituo cha afya, itakayogharimu kiasi cha shilingi milioni 250.

Vilevile amewataka baadhi ya watu wanaoingia katika geti la mgodi wa Mererani, kuacha ubadhirifu na uhujumu uchumi kwa kuiba madini, hatua inayorudisha nyuma maendeleo taifa, hatua hiyo imekuwa ikichangia ukaguzi mkali katika geti la kutokea na kuchukua muda mwingi wa ukaguzi.

“Kurudi kwa mnada huu ni wazi kuwa taifa na watu wake wanaenda kuongeza pato na kukuza uchumi, kuongezeka kwa ajira, kuboreshwa kwa huduma za afya, elimu, miundombinu na mengine mengi, kitu kingine ni namna ya kuwaangalia wafanyabiashara wadogo wa madini ili na muda wao wa kuuza madini kwa lengo la kunufaika kama ilivyo kwa wafanyabiashara wakubwa”amesema Sendiga.

Pia Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya madini Msafiri Mbibo amesema madini yenye gramu 184.06 yenye thamani ya shilingi bilioni 3 yatauzwa kwenye mnada huo uliowakutanisha wauzaji wapatao 195.

“Mnada huo ulioanzishwa rasmi mwaka 1992 ulisitishwa mwaka 2017 ili serikali iangalie namna bora ya uendeshaji ili kuhakikisha taifa na wafanyabiashara wananufaika” ameongeza Mbibo.

Vilevile kwa niaba ya Mwenyekiti wa kamati ya bunge ya kudumu ya nishati na madini Kirumbe Ng’enda amesema serikali itaendelea kuboresha bajeti ya wizara ya madini, ili kufikia hatua wachimbaji kuweza kuchimba madini eneo lenye uhakika wa upatikanaji wa madini, kwani hadi sasa ni asilimia 16 tu ya eneo lenye uhakika wa upatikanaji madini nchini.

Mbunge wa wilaya ya Simanjiro Christopher Ole Sendeka ametoa dukuduku lake la ukaguzi ambao kwa wiki sasa limezua gumzo na kupelekea wachimbaji na wafanyabiashara kutoka usiku wa manane katika eneo hilo kwa sababu ya ukaguzi unaochukua muda mrefu.

“Nawakumbusha kwamba asiwepo yeyote mwenye mawazo kwamba mnada huu utahamia kwingine, mwenye mawazo hayo atakuwa anapingana na kauli aliyoitoa Rais wa nchi kwamba mnada utasalia Mererani” ameeleza Ole Sendeka.

Wachimbaji na wafanyabiashara wakubwa na wadogo wa madini, wakiwa katika uzinduzi wa minada ya ndani katika eneo la kimadini Mererani Mkoani Manyara