Wazazi walia na wamiliki wa shule singida, watoto wao kuchelewa kurejea nyumbani

Na Abby Nkungu, Singida.

WAZAZI wa watoto wanaosoma shule za awali za mchepuo wa Kiingereza
katika Manispaa ya Singida, maarufu “English Medium” wameiomba Serikali
kuwalazimisha wamiliki wa shule za Maasai,Abeti, Maemack na Malaika wa
Matumaini kuwa na magari ya kutosha kwa ajili ya kuwapeleka shuleni na
kuwarejesha majumbani watoto wao kwa muda muafaka.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wazazi wamesema kuwa watoto
wao wanaosoma kutwa katika shule hizo hulazimika kuamka majira ya saa
11:00 alfajiri kila siku za masomo kwa ajili ya kujiandaa kwenda shule
na huchelewa kurejea majumbani hadi saa 11 jioni.
“Hebu fikiria, kwa mtoto wa shule ya awali mwenye umri wa chini ya miaka
sita kulazimika kuamka kila siku saa 11 alfajiri na kurejea nyumbani
saa 11 jioni, kesho yake vivyo hivyo; hakika mtoto anachoka na kumfanya
achukie shule kwa kuona kama vile anapewa adhabu” alisema Sakilu Ntandu,
mmoja wa wazazi.
Sakilu anaeleza kuwa, moja ya sababu kubwa inayochangia watoto wao
kuamka mapema ni uhaba wa mabasi ya shule hizo, hivyo gari moja
hulazimika kuanza mzunguko wa kukusanya watoto mapema kuwapeleka shule
ili kurudi kuchukua wengine. Vivyo hivyo, wakati wa kuwarejesha nyumbani
jioni.
“Kuna wakati mtoto anachoka kupitiliza, unamwamsha hiyo saa 11 alfajiri,
unamnawisha, unamvisha nguo na kumpakia kwenye gari ukidhani yuko macho
kumbe bado anachapa usingizi” alisema mzazi huyo na kuongeza kuwa kuna
baadhi ya shule hizo hazina hata sehemu ya watoto kupumzika baada ya
kupata chakula cha mchana hivyo mtoto huendelea kuteseka mchana kutwa.
Mzazi mwingine, Kidoho Kidimanda alieleza kuwa licha ya kumuamsha
mtoto wake alfajiri, wakati mwingine dereva wa shule haendi kumpitia
kwenye Kituo kilichokubaliwa hali inayomlazimu aingie gharama nyingine
ya kumpeleka shule yeye mwenyewe au huamua kurudi naye nyumbani; hivyo
kumkosesha masomo siku hiyo.
Kutokana na hali hiyo, wazazi hao wameiomba Serikali kuangalia
uwezekano wa kuwalazimisha wamiliki wa shule hizo kuwa na idadi ya
magari kulingana na wingi wa wanafunzi ili kukidhi mahitaji ya
kuwapeleka shule na kuwarejesha nyumbani kwa wakati ikiwa ni njia
mojawapo ya kuboresha mazingira ya mtoto kupenda kwenda shule na
kujifunza katika hatua za awali.
Uchunguzi zaidi wa Mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa uhaba wa
magari katika shule hizo umezaa tatizo lingine la wanafunzi kujazana
kupita kiasi kwenye gari moja.
Changamoto hiyo ni watoto kujazana kupindukia hadi wengine hukaliana
mapajani hali ambayo ni hatari kiafya na ni kinyume na Sheria za Usalama
barabarani; isitoshe, hawajifungi mikanda kutokana na magari hayo
kukosa viti maalum kwa ajili ya watoto, jambo ambalo ni hatari iwapo
ajali itatokea.
Akiongea kwa niaba ya Ofisa Elimu Taaluma shule za Msingi Manispaa ya
Singida, Ofisa elimu Vielelezo Fatina Kipingu alikiri kuwa na taarifa
juu ya baadhi ya shule hizo ambazo wanafunzi wake husoma kutwa hazina
mabasi ya kutosha hivyo wameanza kulifanyia kazi suala hilo.
 
Wataalam wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto wanasema mtoto
anapaswa kupumzika angalau kwa saa moja hadi mbili awapo shuleni na
kwa shule zinazokaa na watoto kwa saa nyingi lazima ziwe na ratiba yenye
huduma ya mapumziko; ikiwemo kulala kwa muda kwa kuwa kupumzika ni afya
kwa mtoto kwani ubongo wake bado unakua kwa kasi