Waziri mkumbo awataka wanachama wa cti kujadili maendeleo ya viwanda nchini

 

Waziri wa Viwanda
na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo ,akizungumza na wanachama wa
Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) Jijini Dar es Salaam uliofadhiliwa
na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ).

Waziri wa Viwanda na Biashara,
Profesa Kitila Mkumbo akiwa katika picha ya pamoja  na wanachama wa
Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) Jijini Dar es Salaam uliofadhiliwa
na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ).

…………………………………………………………………………..

Waziri wa Viwanda
na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo amewataka wanachama wa Shirikisho la
Viwanda Tanzania (CTI) kujadili maendeleo ya viwanda zaidi kuliko
changamoto zinazokabili viwanda nchini ambazo Serikali imeahidi
kuzitatua.

Prof Mkumbo
alisema hayo alipokutana na wanachama wa Shirikisho la Viwanda Tanzania
(CTI) Jijini Dar es Salaam uliofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la
Ujerumani (GIZ).

Aidha aliwataka
wanachama wa CTI kujadili ni jinsi gani wanaendeleza Viwanda nchini
ikiwa ni pamoja na kuendeleza na kuwekeza katika maeneo yote ya Mamlaka
ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) ambayo ni ajenda
ya kitaifa.

Serikali
inatambua mchango mkubwa wa mapato ya nchi unatokana na sekta binafsi
hivyo inaweka mazingira wezeshi na rafiki kwa wawekezaji na
itashirikiana na wadau kutatua changamoto zinazokabili viwanda nchini
ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira wezeshi kwenye biashara. Alisema
Prof. Mkumbo.

Prof. Mkumbo,
aliahidi kutoa ushirikiano kwa sekta binafsi ili kujenga mazingira bora
na kuaminiana baina ya Serikali na sekta binafsi.

“Serikali haina
mpango wa kukwamisha sekta binafsi bali itaendelea kuwawekea mazingira
mazuri na bora ya kufanyia biashara,” alisema.

Naye Mwenyekiti
wa CTI, Paul Makanza alisema katika mkutano huo walijadili kuhusu hali
ya viwanda nchini ikiwa ni pamoja na kuonyesha changamoto
wanazokabiliana nazo na jinsi ya kuzitatua.

“Tumejadili ni
namna gani tunaweza kuongeza tija katika uzalishaji, namna gani tunaweza
kutatua tatizo la ujuzi, ni mapendekezo gani tunaweza kupeleka kwa
serikali ili kuhakikisha mazingira ya biashara yanaweza kuwa mazuri,”
alisema.

Kwa upande wake
mdau wa viwanda, Shabbir Khataw alisema amefurahi kwa kuwa Serikali
imeahidi kuwa pamoja nao kwani inatambua mchango mkubwa wa mapato ya
nchi yanatokana na sekta binafsi.

Veronika
Mbazingwa kutoka kiwanda cha Chemi Cotex alisema baada ya Waziri Mkumbo
kuzungumza nao ni dhahiri kuwa Serikali ipo tayari kushirikiana nao
katika changamoto mbalimbali wanazokutana nazo.

“Hii inatupa
mwanga kwamba kwenye viwanda kutakuwa na mazingira ambayo yatasaidia
katika ushindani wa bidhaa zetu katika masoko ya ndani hata nje ya nchi.

“Kwa upande wa
viwanda tunaona kuna haja ya Serikali kuangalia upande wa nguvu kazi
inayotumika kiwandani tungependa kuona ni namna gani ambavyo tunapata
wafanyakazi wenye ujuzi tuwe na malengo madhubuti ya kupata watu
wanaoweza kusimamia viwanda, tunaongelea wale wahandisi watakaoenda
kwenye mashine na kufanya kazi,” alisema.

Alisema anaamini miaka mitano ijayo watakuwa wamepata nguvu itakayoleta ushindani mkubwa katika viwanda vyao.

“Tunaamini mazingira wezeshi, mazingira mazuri ya biashara yataendelea kuboreshwa,” alisema.

Tanzania imedhamiria kujenga
uchumi wa viwanda, imepiga hatua miaka mitano iliyopita hivyo inatarajia
kuendeleza kasi hiyo katika miaka mingine mitano.