Waziri mkuu azitaka azaki zihimize ulipaji kodi

Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akiwahutubia wananchi, kwenye ufunguzi wa
Maonesho ya Wiki ya Asasi Zisizo za Kiserikali 2019, yaliyofanyika
katika uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma, Novemba 4.2019. (Picha na Ofisi
ya Waziri Mkuu).

…………………………

*Ataka fedha wanazopata zitumike kujenga miradi mikubwa
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka Asasi za Kiraia ziendelee kuelimisha umma juu ya umuhimu wa kulipa kodi.
“Nitoe
rai kwenu wana AZAKI, muendelee kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa
kulipa kodi kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla ili
Serikali iweze kujenga miradi mikubwa ya kijamii,” amesema.
Ametoa
wito huo leo jioni (Jumatatu, Novemba 4, 2019) wakati akizungumza na
mamia ya wananchi na washiriki wa Maonesho ya Wiki ya Asasi za Kiraia
(AZAKI) nchini yaliyoanza leo kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Maonesho hayo yatafikia kilele chake Ijumaa, Novemba 8, mwaka huu.
Amesema
Serikali inatambua na kuthamini mchango wa mashirika yasiyo ya
Kiserikali katika kusukuma gurudumu la maendeleo nchini kama vile
kuwajengea uwezo viongozi wa Serikali za Mitaa wakiwemo Madiwani,
viongozi wa vijiji na mitaa ili watambue majukumu yao.
“Niwatoe
hofu tu kwamba Serikali inatambua mchango wenu wa kuhamasisha wananchi
kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo; kujiongezea kipato na kupata
ujuzi; utoaji wa huduma za kijamii hususan elimu, afya, upatikanaji wa
maji, huduma za kisheria na huduma za mikopo midogo.
“Pia
tunatambua mchango wa AZAKI wa kuleta teknolojia mpya na rahisi kwa
wananchi pale mnapoona kuna uhitaji. Pia mnaisaidia Serikali kupinga
mila potofu na kandamizi hasa kwa makundi yenye mahitaji maalum,”
amesema.
Wakati
huohuo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuzitaka AZAKI nchini
zizingatie sheria iliyofanyiwa marekebisho ya Mashirika Yasiyo ya
Kiserikali Na. 24/2002 na kanuni zake, ambayo ilipitishwa na Bunge
kupitia Sheria Na. 3/2019 na kusisitiza kwamba marekebisho hayo
yalilenga kuboresha sekta hiyo.
“Nipende
kuwahakikishia wana-AZAKI kuwa marekebisho hayo yalilenga kuboresha
sekta ya NGOs na siyo kuyabana mashirika yasiyo ya Kiserikali kama
ambavyo imekuwa ikipotoshwa na baadhi ya watu. Marekebisho hayo
yalizingatia misingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya
mwaka 1977,” amesema.
Kuhusu
mapato ya AZAKI, Waziri Mkuu amesema fedha wanazopata zinaweza kufanya
miradi mikubwa ambayo itawanufaisha wananchi na akawasihi wazitumie
kwenye ujenzi wa miradi mikubwa inayoonekana badala ya kuendesha semina
na warsha.

“Tunajua
fedha mnazopata zinaweza kusaidia kwenye miradi hii. Kwa mfano, kuanzia
Januari hadi Septemba, mwaka huu, tulifanya mapitio ya ufadhili wa
fedha mnazopata. Na katika upekuzi uliofanyika kwenye taasisi 92,
ilibainika kwamba zilipokea jumla ya sh. bilioni 261.059 ambazo
zimeingia kwenye AZAKI hizi.”
“Vilevile,
mwaka 2016 hadi 2017, tuliangalia mapato ya NGOs 51, tukagundua kuwa
katika kipindi cha miaka miwili, zimepokea jumla ya shilingi trilioni
2.5. Kama fedha hizi zote zingeratibiwa vizuri kwa kupunguza matumizi
yasiyo na umuhimu ni lazima tungefika mbali. Tutumie vizuri fedha hizi
za ufadhili kwa miradi inayoonekana,” amesisitiza.
Akizungumzia
kuhusu ajira kwa vijana, Waziri Mkuu amesema vijana ni kundi lenye
umuhimu mkubwa katika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo licha
ya kuwa wanakabiliwa na uhaba wa ajira.
Amesema
Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, inaonesha asilimia 35 ya
Watanzania wote ni vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35. Kwa mujibu wa
matokeo ya utafiti wa nguvukazi ya Taifa wa mwaka 2014, vijana
wamebainika kuwa ndio kundi kubwa la nguvukazi ya Taifa ambao ni
asilimia 56 ya nguvukazi yote nchini.
“Kila
mwaka, kumekuwa na ongezeko la vijana wanaoingia kwenye soko la ajira.
Kwa mfano, taarifa ya hali ya ajira ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa
mwaka 2019 inaonesha kuwa asilimia 11.8 ya nguvukazi ya vijana duniani
ambao ni takriban vijana million 59.1 hawana kazi,” amesema.
Mapema,
Waziri wa Nchi (OR-TAMISEMI), Bw. Suleiman Jafo alizishukuru asasi zote
za kiraia ambazo zinafanya kazi Tanzania kwa sababu zinawahudumia
wananchi kwa karibu zaidi. “Ninazishukuru NGOs zote kwa kusaidia kutoa
elimu kwa wananchi. GTunazishukuru kwa kazi kubwa mnayoifanya Tanzania
nzima kwa kushirikiana na Ofsi ya Rais TAMISEMI,”
Akimkaribisha
Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa maonesho hayo, Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bi. Ummy Mwalimu alisema
mwaka huu, wizara yake imesajili mashirika yasiyo ya Kiserikali 617
ikilinganishwa na mashirika 385 yaliyosajiliwa mwaka 2017.
“Kati
ya hayo mashirika 617, mashirika 44 ni ya ngazi ya kimataifa; 551 ni
ngazi ya kitaifa, saba ni katika ngazi ya mikoa na mashirika 15 ni
katika ngazi ya wilaya. Hadi kufikia Oktoba, 30, 2019, tumeshasajili
mashirika 19,318” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *