Waziri mkuu: rc fuatilia utendaji kazi ofisi ya dc kilolo


WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Happi
afuatilie utendaji kazi kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya ya Kilolo
kufuatia watumishi 14 wa ofisi hiyo wakiwemo madereva 10 kuhamishwa
baada ya Mkuu wa Wilaya hiyo Asia Abdallah kudai kuwa hawafanyi kazi
ipasavyo.


Hata
hivyo, Waziri Mkuu amesema ni mhuimu kwa viongozi wakatambua dhamana
zao katika utekelezaji wa shughuli zao pamoja na kuwatambua, kuwajali na
kuwathamini watumishi wa kada zote wakiwemo madereva, hivyo ni vizuri
wawaandae kwa kuwapa maelekezo kwa wakati kwa kuwa nao ni binadamu na
wanafamilia.

Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Septemba 27, 2019) wakati
akizungumza na watumishi wa wilaya ya Kilolo, Halmashauri ya wilaya ya
Kilolo pamoja na Madiwani wa Halmashauri hiyo akiwa katika siku ya nne
ya ziara yake ya kikazi mkoani Iringa. Amesisitiza umuhimu wa watumishi
hao kushirikiana.

Waziri
Mkuu amesema pamoja na shughuli za maendeleo wanazofanya katika wilaya
hiyo lakini hawana mshikamano, hivyo amemtaka Mkuu wa Wilaya ahakikishe
anashirikiana vizuri na wenzake kwa sababu watumishi wengi wamehamishwa
tangu aingie katika ofisi hiyo na hata wanaoletwa wanalalamika na
wanaomba wahamishwe.

Amesema
watumishi wengi katika ofisi hiyo anawaona hawana uwezo wakiwemo
wasaidizi wake kama madereva, watunza kumbukumbu na makatibu muhtasi.
“Hata aliyekuwa Katibu Tawala wa wilaya hii alihamishwa kwa sababu na
kutoelewana na DC, na hata huyu Katibu Tawala wa Wilaya aliyepo sasa
hana raha anataka kuhama kwa sababu hizo hizo.”

“Lazima
tuwatambue wasaidizi wetu na majukumu yao. Ofisi ya Mkuu wa Wilaya
haiwezekani ikawa hivi, lazima kuna shida kuwaondoa watumishi wote, Mkuu
wa Mkoa fuatilia hii ni mpya. Hapa tujue mbovu ni nani Mkuu wa Mkoa
tunataka tujue DC wako anataka dereva wa aina gani, tangu amefika hapa
madereva 10 wote hawafai?

Waziri
Mkuu ameongeza kuwa “ili mfanye kazi vizuri mnatakiwa mshikamane mfanye
kazi kama timu moja kwani pamoja na shughuli mnazofanya hamna
ushirikiano. DC (mkuu wa wilaya) sasa utabaki peke yako utakuwa
unaandika mwenyewe, unaendesha gari mwenyewe maana wote hawafai. Mkuu
Mkoa nakukabidhi majina ya watumishi hao ushughulikie suala hili. Na
Katibu Tawala wa Mkoa usilete watumishi wengine hapa mpaka suala hili
litakapopatiwa ufumbuzi”

Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu ameziagiza halmashauri zote nchini
zihakikishe zinatenga kiasi cha fedha katika makusanyo yao ya ndani kwa
ajili ya kutekeleza ujenzi wa miradi ya kimkakati kwenye maeneo yao kama
ujenzi wa vituo vya afya, barabara za halmashauri na masoko badala ya
kutegemea fedha kutoka Serikali Kuu pekee.

Amesema
wilaya ya Kilolo ambayo haina kituo cha mabasi inatakiwa itenge fedha
kutoka kwenye makusanyo yao na kuanzisha mradi wa kituo hicho ambao
utekelezaji wake utaboresha huduma kwa wananchi pia, mradi huo utasaidia
katika kuongeza mapato ya halmashauri. Halmashauri ya wilaya ya Kilolo
inakusanya sh. bilioni nne kwa mwaka.

Waziri
Mkuu amesema watumishi wanapaswa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwani
wananchi wanahitaji waone matokeo ya uwepo wao kutokana na dhamana
waliyotewa na Serikali katika wilaya hiyo. “Madiwani nanyi simamieni
halmashauri yenu vizuri kwa sababu nyie ndiyo wenye dhamana ya
kuhakikisha wananchi wanahudumiwa vizuri.”

Awali,
Mbunge wa jimbo la Kilolo, Venance Mwamoto aliishukuru Serikali ya
Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa kutoa fedha za
utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika wilaya yao ikiwemo
ya umeme, ambapo kati ya vijiji 94 vilivyoko vijiji 54 vimeunganishiwa
huduma hiyo na vilivyosalia vitakuwa viunganishiwa umeme ifikapo Desemba
mwaka huu.

Akizungumzia
kuhusu miradi ya maji mbunge huyo alisema kati ya vijiji 94 vya wilaya
hiyo vijiji 15 tu ndio bado havina maji ya uhakika lakini wanaendelea na
mchakato wa ufuatiliaji ili kuhakikisha navyo vipata maji safi na
salama.”Kuhusu sekta ya elimu tatizo tulilonalo ni madai ya walimu
waliohama na waliopandishwa madaraja.” Waziri Mkuu amesema suala hilo
linafanyiwa kazi.

Mapema,
Waziri Mkuu alikagua mradi wa ujenzi wa hospitali ya wilaya na kupokea
taarifa ya ujenzi wa hospitali hiyo ambapo alisema ameridhishwa na
ujenzi huo uliogharimu sh. bilioni nne na alitumia fursa hiyo
kuwapongeza viongozi wa wilaya hiyo akiwemo Mkurugenzi pamoja na
mkandarasi anayenga.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU