Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.
Mashimba Ndaki akizungumza na viongozi na wataalam kutoka wizarani
upande wa sekta ya Mifugo, sekretarieti ya mkoa wa Kagera na Wilaya ya
Muleba kuhusu migogoro iliyopo kwenye Ranchi ya Kagoma na Mwesa ambapo
ameagiza upimaji ufanyike katika eneo hilo ili kutatua migogoro iliyopo
sasa ili wawekezaji waweze kuyatumia maeneo hayo kwa ajili ya kufugia
mifugo na wananchi waendeleze shughuli zao za kiuchumi. Kikao hicho
kimefanyika kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Muleba.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.
Mashimba Ndaki akizungumza na wananchi na wawekezaji waliopo kwenye
Ranchi ya Kagoma kuhusu mgogoro wa ardhi ambapo ameagiza maeneo
yaliyovamiwa na wananchi yapimwe ili wawekezaji waweze kubakiwa na eneo
ambalo halitakuwa na mgogoro na kwamba baada ya kupimwa atakae vamia
eneo la mtu atachukuliwa hatua.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi
(Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akifafanua jambo kuhusu
upandaji wa malisho kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki
na Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mhe. Toba Nguvila (katikati) wakati
walipokua wanakagua baadhi ya maeneo kwenye Ranchi ya Kagoma iliyopo
wilayani Muleba Mkoa wa Kagera.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi
(Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akizungumza jambo Katibu
Tawala Mkoa wa Kagera, Prof. Faustine Kamuzora (katikati) wakati wa
mkutano wa kutatua mgogoro kati ya wananchi na wawekezaji kwenye Ranchi
ya Kagoma. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ranchi za Taifa
(NARCO), Prof. Peter Msoffe.
Wananchi na wawekezaji katika Ranchi
ya Kagoma wakifuatilia maelekezo yaliyokuwa yakitolewa na Waziri wa
Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (hayupo pichani) wakati alipofanya
mkutano kwa ajili ya kutatua migogoro ya ardhi katika ranchi hiyo.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.
Mashimba Ndaki akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi na wataalam
kutoka wizarani upande wa sekta ya Mifugo, sekretarieti ya mkoa wa
Kagera, Wilaya ya Muleba, Chama cha Mapinduzi na wananchi wa Kijiji cha
Rutoro mara baada ya kumalizika kwa kikao kilichojadili hali ya migogoro
kwenye Ranchi za Kagoma.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.
Mashimba Ndaki akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi na wataalam
kutoka wizarani upande wa sekta ya Mifugo, sekretarieti ya mkoa wa
Kagera, Wilaya ya Muleba, Chama cha Mapinduzi na wawekezaji katika
Ranchi ya Kagoma mara baada ya kumalizika kwa kikao kilichojadili hali
ya migogoro kwenye Ranchi hiyo.
………………………………………………..
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.
Mashimba Mashauri Ndaki ameumaliza mgogoro wa ardhi kati ya wananchi
waliovamia kwenye vitalu katika Ranchi ya Kagoma na wawekezaji ambao
wanamiliki vitalu hivyo.
Waziri Ndaki ameumaliza mgogoro huo
leo (10.07.2021) baada ya kuwasikiliza wananchi na wawekezaji kwenye
mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kijiji cha Rutoro wilayani Muleba
Mkoa wa Kagera.
Akizungimzia kuhusu mgogoro huo,
Waziri Ndaki aliwaeleza wananchi kuwa maeneo hayo waliyoyavamia ni mali
ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ambayo tayari yalikuwa
yameshakodishwa kwa wawekezaji wanaofanya shughuli za ufugaji hivyo
walipaswa kuondolewa. Lakini kutokana na busara za Mhe. Rais Samia
ameridhia eneo hilo lipimwe na wananchi wabakizwe kwenye vijiji vinne
vilivyopo ambavyo ni Kijiji cha Rutoro, Byengeregere, Chobuheke na
Mishambya vilivopo katika Kata ya Rutoro.
“Ninyi wananchi mnatakiwa kumshukuru
sana Rais Samia kwa maamuzi yake ya kuwabakiza katika maeneo haya.
Lakini niwasihi kuwa watulivu wakati wa zoezi la upimaji wa maeneo na
kutoa ushirikiano kwa wataalam watakao kuja kutekeleza zoezi hilo,”
alisema Waziri Ndaki.
Vilevile amewataka wananchi
kutoendelea kuvamia maeneo mengine katika ranchi hiyo kwani wakifanya
hivyo kwa sasa watachukuliwa hatua. Waziri Ndaki pia ametoa onyo kwa
wananchi wenye tabia ya kuuza maeneo hayo wakati wao wenyewe
hawajamilikishwa.
Pia kwa upande wa wawekezaji hao
amewahakikishi kuwa zoezi hilo la upimaji wa maeneo halitaathiri
shughuli zao za ufugaji kwa kuwa utawekwa utaratibu mzuri. Vilevile
amewaeleza kuwa maamuzi hayo ya kupima maeneo na kuweka alama za mipaka
yatasaidia sana kupunguza migogoro ya ardhi na kufanya pande zote kuishi
kwa amani.
Katika mkutano huo yalitolewa
malalamiko kuwa wafugaji wanalisha mifugo kwenye mashamba yao na
kuwasababishia hasara. Kutokana na hilo Waziri Ndaki aliwaagiza wafugaji
hao kuacha tabia hiyo kwani ni moja ya vitu vinavyosababisha tatizo la
njaa kwa wananchi na kuleta migogoro baina ya pande zote mbili.
Vilevile wawekezaji wametakiwa
kuhakikisha wanayatumia maeneo waliyopewa kwa malengo yaliyokusudiwa na
si vinginevyo. Aidha, uongozi wa wilaya ya Muleba umetakiwa kuweka
utaratibu utakaotumika kuwaondoa wavamizi kwenye vitalu ambao wameingiza
mifugo yao wakati hawajamilikishwa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mhe.
Toba Nguvila amemuhakikishia Waziri kuwa maelekezo aliyoyatoa watakwenda
kuyasimamia kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa wa Kagera na uongozi wa
Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO).
Kutokana na uamuzi uliochukuliwa wa
kupima maeneo hayo kwenye ranchi ya Kagoma, wawekezaji na wananchi wote
wameonesha mtazamo chanya kwani hata wao wenyewe hilo ndio wameliona
ndio suluhisho.