Wizara ya Maliasili na Utalii yaonya uvamizi eneo la mapito ya wanyama na mauwaji wanyama la Burunge
Mwandishi wetu
Babati.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Staslaus Kanyasu,ameonya serikali kuwachukulia hatua watu, wanaoanza kuvamia eneo la mapito ya wanyamapori wanaotoka hifadhi ya Taifa ya Tarangire kwenda hifadhi ya Manyara na kuanza kujenga makazi , kuingiza mifugo na kufungua mashamba.
Akizungumza jana baada ya kutembelea eneo hilo ambapo kumeundwa jumuiya ya hifadhi ya wanyamapori ya Burunge, Naibu waziri Kanyasu, alisema eneo hilo ni muhimu kwa uhifadhi kwani,lipo kati kati ya hifadhi za Taifa za Manyara na tarangire na ni lazima lilindwe.
Naibu Waziri Kanyasu alisema ni lazima shirika la hifadhi za taifa(TANAPA), Mamlaka ya usimamizi wanyamapori(TAWA) taasisi za utafiti wa wanyamapori(TAWIR) na Burunge WMA kukaa na kuanza mikakati ya kuweka mipaka ya mapito ya wanyamapori kulingana na sheria.
Naibu Waziri huyo, pia alionya kuanza kuibuka matukio ya baadhi ya watu, kuanza kuingiza mifugo katika maeneo hifadhi hiyo na kuuwa wanyama .
“kuna baadhi ya viongozi wa WMA wanatajwa kuhusikano na kuingiza mifugo eneo la hifadhi na kushindwa kudhibiti wahalifu tunaonya kuchukuwa hatua kali na wale ambao waliua pundamilia na Twiga tayari tumewakamata”alisema.
Mkuu wa wilaya ya Babati, Elizabeth Kitundu akizungumza katika ziara hiyo, alisema ni muhimu mapito ya wanyama kulindwa katika eneo hilo, hasa kutokana na tayari wizara ya maliasili kutoa sheria za kulinda mapito hayo.
Mwenyekiti wa Burunge WMA Marceli Yeno alisema jumuiya hiyo inakabiliwa na changamoto kadhaa licha mapato ya jumuiya hiyo kufikia sh 2 bilioni kutokana na mapato ya sekta ya Utalii.
Alisema hifadhi ya jamii ya wanyamapori(WMA) ya Burunge iliyoanzishwa tangu mwaka 2003 akiwa na eneo la kilomita za mraba 283 na inaundwa na vijiji 10.