Waziri wa Viwanda na Biashara
Mhe.Prof.Kitila Mkumbo,akizungumza bungeni leo Mei 22,2021 wakati
akiwasilisha hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa
Mwaka 2021/2022.
Na.Alex Sonna, Dodoma.
Wizara ya Viwanda na Biashara
imewasilisha bungeni makadirio ya matumizi kwa Wizara hiyo kwa mwaka
2021-2022 na kueleza kuwa katika makadirio hayo yamelenga katika kupanua
wigo wa upatikanaji wa viwanda hasa vya sukuari ili kupunguza uhaba wa
sukari ambapo hutokea mara kwa mara.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha
bajeti hiyo Bungeni leo Mei 22, 2021 Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.
Prof. Kitila Mkumbo amesema wamejipanga kukabiliana na upungufu wa
sukari kwa kuanzisha viwanda vipya na kupanua uwezo wa viwanda vilivyopo
kwa sasa.
“Serikali inaendelea kuchukua hatua
mbalimbali katika kuongeza uzalishaji wa sukari kwa kupanua na kuongeza
uwezo wa viwanda vikubwa vilivyopo, ikiwemo Kiwanda cha Sukari cha
Kilombero,pamoja na kuanzisha viwanda vikubwa vipya,
“Sambamba na hatua hizi, katika
jitihada za kuongeza uzalishaji wa sukari ili kukidhi mahitaji ya bidhaa
hii nchini, Serikali imeelekeza Taasisi ya TEMDO kufanya usanifu na
kuanza kutengeneza mitambo midogo kwa lengo la kuwawezesha wajasiriamali
wadogo waanze kuchakata miwa ili kupata sukari (Sugar Min –Processing
Plant)” amesema Mkumbo.
Amesema kuwa hatua hii itaweza
kuongeza uzalishaji wa sukari na kuhakikisha kuwa wakulima wadogo (out
growers) wanaweze kuchakata miwa yao bila kuwa tegemezi katika viwanda
vikubwa.
Pia amesema watakamilisha taratibu za
kuwapata wawekezaji wapya waviwanda vilivyobinafisishwa na baadaye
kurudishwa serikalini, kukamilisha kanzidata ya viwanda na biashara
nchini, kuimarisha mfumo wa usajili wa makampuni na leseni za biashara
kupitia Wakala wa Usajili na Leseni za Biashara (BRELA).
Vipaumbele vingine ni kuimarisha Mfuko
wa Taifa wa Kuendeleza wajasiriamali Wadogo(National Entrepreneurship
Development Fund-NEDF) kwa kupanua wigo wa mtaji wa mfuko huo, kuratibu
na kusimamia uanzishwaji wa maeneo maalum ya kibiashara (trading hubs).
Ameongeza kuwa “Vipaumbe vingine ni
kuimarisha na kukuza matumizi ya utafiti na maendeleo, teknolojia na
ubunifukatika sekta ya viwanda na biashara, kuendelea kusimamia viwango
vya ubora na kubuni viwango vipya kwa ajili ya bidhaa zinazozalishwa na
kuingizwa Tanzania kupitia TBS na Wakala wa Vipimo (WMA)” amesema.
Vipaumbele vingine ni kuhamasisha,
kuendeleza na kulinda viwanda vya kuzalisha chuma na bidhaa za chuma,
kuendeleza na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya ngozi, nguo na mavazi,
kuhamasisha, kuendeleza na kulinda viwanda vya kuzalisha chuma na bidhaa
za chuma.
Kuweka msukumo na mazingira mazuri kwa
ajili ya uwekezaji wa viwanda vya kuunganisha vifaa vya kielekroniki na
magari, kuhamasisha viwanda vinavyozalisha vifaa vya ujenzi.
Pia amebainisha kuwa Serikali
imejipanga katika kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya kutengeneza betri na
umeme wa magari kwa kutumia rasilimali asili za nchi kama vile madini
ya Lithium, Vanadium na Titanium, ambayo pia yanapatikana hapa nchi.
Vile vile tutajikita kuweka mazingira
wezeshi kisera na kisheria ya kufanya biashara, kujiunga au kuimarisha
ushiriki wa Tanzania katika jumuiya za kiuchumi na kimasoko za kikanda
kwa ajili ya kupanua fursa za kibiashara kwa bidhaa za Tanzania ambazo
zitazalishwa hapa nchini.
Waziri Mkumbo ameongeza kuwa “Pia
tutajikita katika kuimarisha upatikanaji wa mitaji kwa wajasiriamali na
wafanya biashara wadogo ili wapanue mitaji yao ili kuendesha biashara
zao, tutaweka mazingira bora kisera, kisheria na kiutendaji kwa ajili ya
kuchochea na kulinda ukuaji wa sekta binafsi kama injini na msingi wa
ujenzi wa uchumi wa viwanda na shindani kuweza kushindana na mataifa
mengine” amesema.
Ameongeza kuwa “Lengo kuu la ilani ya
Chama Cha Mapinduzi kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ni kuleta
mapinduzi ya uchumi kwa maendeleo ya watu, moja ya nyenzo ya kuleta
mapinduzi ya uchumi iliyoanishwa katika ilani hiyo ni kujenga Tanzania
ya uchumi wa viwanda na kukuza biashara” amesema.
Wizara ya Viwanda na Biashara imeomba
kuidhinishiwa jumla ya shilingi Shilingi bilioni, 105,670,459,000, kati
ya fedha hizo, Shilingi bilioni, 52,582,573,000, ni za Matumizi ya
kawaida na Shilingi bilioni 53,087,886,000, ni za Matumizi ya Maendeleo.