Wizara yathibitisha mgonjwa wa kwanza wa corona nchini

Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, akizungumza na Waandishi
wa Habari(hawapo pichani), kuhusu kugundulika kwa Mgonjwa wa Corona nchini,
mkutano ambao ulifanyika Jijini Dar es Salaam, kulia ni Mwakilishi wa Shirika
la Afya Duniani (WHO), Dkt. Tigest Katsela Mangestu na kushoto ni Naibu Waziri
wa Afya  Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, akizungumza na Waandishi wa Habari(hawapo pichani), kuhusu kugundulika
kwa Mgonjwa wa Corona nchini, mkutano ambao ulifanyika Jijini Dar es Salaam,
kushoto ni Naibu Waziri wa Afya 
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile

Na.Mwandishi
Wetu- MAELEZO.
Serikali kupitia Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia Wazee na Watoto, Mhe.Ummy Mwalimu imethibitisha kuwepo ka mgonjwa mmoja
wa Corona ambapo amewasisitiza  wananchi
kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam,
Waziri Ummy alisema  kuwa Machi 15, 2020
aligundulika mgonjwa mmoja mwanamke mwenye umri wa miaka 46 ambaye aliwasili na
ndege ya Rwandair akitokea nchini Ubelgiji.
“Mwanamke huyu aliondoka nchini Machi 5, 2020 na
alitembelea nchi za Sweden na Denmark machi 5-13 na baada ya hapo alirudi
Ubelgiji na kurejea nchini machi 15, 2020, mgonjwa huyu alipita katika uwanja
wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, KIA na alipimwa na kuonekana hana ugonjwa
huo baadae akiwa hotelini alianza kujihisi vibaya na alikwenda katika hospitali
ya Rufaa Mt.Meru na sampuli ilichukuliwa na kupelekwa maabara ya Taifa ya Afya
ya Jamii ambapo majibu yemekuja amegundulika kuwa na Corona”, Alisema Waziri
Ummy.
Alisema kuwa serikali inaendelea kuchukua tahadhari,
pia aliwataka wanachi kuendelea kujikinga kwa kufuata ushauri unaotolewa na
wataalamu wa Afya  wakishirikiana na
Shirika la Afya duniani  WHO ili kuepuka
kusambaa zaidi kwa virusi hivyo.
Aidha Waziri Ummy alisema kuwa katika Taasisi zote
ambazo mikusanyiko ni mikubwa na watu kukutana mara kwa mara zikiwemo, Shule,
hoteli, maduka ya biashara, nyumba za kulala wageni, makanisa, misikiti, Ofisi
za Umma na Binafsi na sehemu za kutolea huduma za Afya pamoja na sehemu
nyingine za mikusanyiko mbalimbali kuweka vifaa vya kunawia zikiwa na maji safi
yanayotiririka na yenye Klorini.
Hatua nyingine za kujikinga ni pamoja na  kuweka maji dawa ya Klorini au vitakasa
mikono, kuweka maji yenye Klorini katika vituo vya mabasi ya abiria, kuepuka
kusalimiana kwa mikono, kukumbatiana, kugusa pua, mdomo pamoja na macho kadri
inavyowezekana.
Waziri huyo wa Afya amezitaka hospitali zote kuhakikisha
kuwa ndugu na jamaa wanaoenda kuona wagonjwa angalau wawe wawili na kutoa
taarifa kituo cha Afya endepo atapatikana mtu mwenye dalili za Corona.