Michuano ya kufuzu ya BAL na NBL 2019.
Mashindano ya kutafuta Klabu bingwa ya Kikapu Tanzania Wanaume na wanawake (National Basketball League) NBL 2019 yamefika hatua ya robo fainali, mashindano haya yaliyoanza 3 Nov na yanatarajiwa kumalizika 9 Nov, yanafanyika uwanja wa ndani wa Taifa, Dar es Salaam.
Timu zilizoingia robo fainali Wanaume ni JKT, Savio, Oilers, Vijana, Pazi, ABC, Rukwa Stars na Ukonga Kings, kwa upande wa wanawake timu ni Don Bosco Lioness, Vijana Queens, Deap Sea Queens na Ukonga Queens.
Bingwa wa NBL 2019 atashiriki mashindano ya BAL 2021 ambapo michuano ya awali ya kufuzu itaanza mwaka 2020 kwa wanaume na kwa wanawake bingwa atapata nafasi ya kushiriki mashindano ya klabu bingwa ya kikapu ya Afrika kanda ya tano 2020.
Mashindano haya na mengine yote yajayo ya kikapu Tanzania yanarushwa mubashara, tembelea mitandao ya kijamii ya kikapu kama inavyoonekana hapo chini kupata taarifa zaidi namna ya kuangalia mubashara na kupata matokeo kadri michezo inavyoendelea.
Mzunguko kwanza ya Basketball Africa League (BAL) umemalizika rasmi tarehe 3 Nov, 2019 ambapo timu 12 zimepata nafasi ya kushiriki mzunguko wa pili ambao utashirikisha timu 16.
Jiji la Yaounde la Cameroon litakuwa mwenyeji wa kanda ya magharibi (kundi G) na jiji la Kigali la Rwanda litakuwa mwenyeji wa kanda ya Mashariki (kundi H).
Kila kanda itakuwa na timu 8 ambazo zitagawanywa katika makundi 2 ya timu 4 kila kundi, ambapo kila timu itacheza na mwenzake na timu 2 za juu zitacheza nusu fainali ambapo timu 3 za juu zitafuzu kwenda katika ligi ya BAL itakayoanza mwezi machi mwaka 2020.
Kundi G watacheza mashindano yao Nov 26 hadi Dec1 na kundi H itakuwa ni Dec 17-22, 2019.
Kundi G litashirikisha timu za Force Armees Police ya Cameroon, Abidjan Basketball Club ya Ivory Coast, AS Police ya Mali, AS Nigelec ya Niger, GSP ya Algeria na Manga ya Gabon.
Kundi H litakuwa na timu za Patriots ya Rwanda, City Oilers ya Uganda, Ferroviario de Maputo ya Msumbiji, GNBC ya Madagascar, Kenya Ports Authority ya Kenya na UNZA Pacers ya Zambia.
Timu 4 zaidi zilizofanya vizuri katika mzunguko wa kwanza pia zitapata nafasi ya kushiriki mzunguko wa pili wa kufuzu BAL 2020 ili kukamilisha timu 16 kwa mzunguko huu.
Tuna matumaini makubwa JKT ya Tanzania itapata nafasi ya kuwa miongoni mwa timu 4 zitakazopata nafasi ya kushiriki mzunguko wa pili katika kanda ya Mashariki kituo cha Kigali.
JKT ilishika nafasi ya tatu katika mzunguko wa kwanza katika michuano ya awali ya kufuzu BAL ya kundi D katika mashindano yaliyofanyika uwanja wa ndani wa Taifa, Dar es Salaam 16 hadi 20, Oct, 2019, taarifa zaidi itatolewa muda wowote kuanzia sasa hivi.
Uzinduzi rasmi wa BAL 2020 utafanyika tarehe 4 hadi 5, Dec, 2019 Brooklyn, New York, Marekani ambapo Viongozi wa Mashirikisho ya kikapu, viongozi wa timu za kikapu, Wachezaji, Wasaka Vipaji na wadau mbalimbali wa kikapu wamealikwa kuhudhuria tukio hilo.
Wadau na wapenzi wa kikapu karibuni sana uwanja wa ndani wa Taifa leo katika robo fainali na kila siku kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 4 usiku kuangalia mashindano haya ya NBL 2019 Wanawake na Wanaume, nusu fainali ni Ijumaa tarehe 8 Nov na fainali itakuwa ni Jumamosi tarehe 9 Nov, 2019.
We Are Basketball.
Phares Magesa
Rais,
Shirikisho la mpira wa kikapu Tanzania (TBF)
7 Nov, 2019