Waziri mwakyembe: radio, kumbi za starehe na vyombo vya usafiri kulipia sanaa tanzania

Na Mwandishi Wetu

Kauli ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini Tanzania, Dk. Harrison Mwakyembe ya kusema kwamba kuanzia tarehe 28 Agosti 2019 ndio itakuwa mwisho wa kutumia kazi za wasanii nchini humo bila kulipia, imezua utata mtandaoni na huku watu wakihoji kama utatekelezeka.

Dkt Harrison Mwakyembe, Waziri wa Habari, Sanaa, michezo na utamaduni

“Ni mwisho wa kazi ya sanaa kutumika bila kulipwa, kwenye kumbi zote za starehe iwe harusi au kitchen party watachangia, Inakuwaje Mshehereshaji (MC) anapiga muziki katika sherehe bila kulipia muziki anaotumia wakati yeye analipwa.

Ukiwa hotelini au kwenye daladala/Basi yenye mfumo wa burudani ya muziki au filamu lazima hiyo burudani iwe imelipiwa, kila mtu anapaswa kulipia” waziri Mwakyembe alisisitiza.

Waziri huyo aliongeza kuwa jambo hilo la kulipia sanaa sio jipya kwani duniani kote wasanii wanalipwa kwa kazi zao.

“Nchi zilizoendelea walianza zamani kuwalipa wasanii wao na sasa ili tuendelee lazima tulipe”.

“Tanzania tulichelewa sana kukubali kuwa sanaa ni kazi , kwa sababu utamaduni wetu kwa muda mrefu kuona sanaa sio biashara bali ni urithi wa jamii fulani, burudani isiyo rasmi na historia ya ujamaa ilichangia sana”.

Na katika kufanikisha hilo serikali imeamua kufanya jitihada ya kukaa na wasanii ili kuwashirikisha na kutaka kujua ni nini ambacho wanakitaka kwa sababu, imeeleza kwamba ‘haiwezekani msanii anayetengeneza wimbo wake lakini lazima msanii huyo ndio alipe ili wimbo wake uweze kupigwa kwenye redio’.