Na Mapuli Kitina Misalaba
Baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutangaza Uchaguzi ngazi ya Kanda, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Shinyanga Emmanuel Ntobi amejitosa kuwania Uenyekiti wa Chadema Kanda ya Serengeti ambayo inaundwa na Mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mara.
Mapema leo Jumatatu Aprili 22,2024 Ntobi akiwa ameambatama na baadhi ya wafuasi wake wamefika katika ofisi za Chadema Kanda ya Serengeti zilizopo Ngokolo – Shinyanga mjini, ambapo amerejesha fomu yake ya kugombea nafasi hiyo.
Ntobi anasema kwamba ana nia ya dhati ya kuleta mageuzi ya kiuongozi Katika kanda hiyo ya Serengeti ambayo ni moja kati ya maeneo ya kimkakati ya Chadema.
Anaamini kwa uzoefu wake pamoja na kushirikiana na Viongozi wenzake wataweza kuifanya Chadema izidi kuwa na nguvu na watahakikisha Chadema inashinda Uchaguzi Mkuu na Uchaguzi wa Serikali za mitaa ambao unatarajia kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.
“Mimi kabla sijaingia rasmi kwenye Siasa za mageuzi, nilikuwa afisa msimamizi wa mikopo katika benki ya NBC pale Makao makuu Dar es Salaam, ambapo nilifanyakazi kwa muda wa zaidi ya miaka mitano.
Mwaka 2015 nilichaguliwa kuwa Diwani wa Chadema kata ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga, na baadae kuchaguliwa na Madiwani wenzangu wa CHADEMA katika Kanda hii na kuwa; Mwenyekiti wa Umoja wa Madiwani CHADEMA Kanda ya Serengeti, katika uchaguzi uliofanyika Mkoani Mara Augusti 2017.
Na mwaka 2019 nilichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Shinyanga, nafasi ambayo naitumikia mpaka sasa”, anaeleza Ntobi
Ntobi anasema kwamba anatambua kuwa kwa hatua ya sasa bado Chama chake hakijaruhusu wagombea kufanya kampeni ila muda ukifika anaomba wajumbe wote wa Baraza la Uongozi la Kanda wamuunge mkono.