Katibu Mkuu CCM: Uchaguzi sio Namba, Ni Maamuzi ya Umma

Katibu
Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally amewakumbusha
baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa nchini maana halisi ya uchaguzi ni
maamuzi ya Umma si kama ambavyo wamekuwa wakieleza kwa kupotosha kuwa,
uchaguzi ni namba.

Ameyasema hayo tarehe 13 Januari, 2020 alipokuwa akihutubia viongozi wa
mashina,matawi, Kata na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya wilaya za Handeni
na Kilindi Mkoani Tanga.

“Nimewasikia baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa, wanasema uchaguzi ni
namba. Uchaguzi sio namba, uchaguzi ni uamuzi wa umma, namba ni kitu
cha baadae, waambieni wanaosema uchaguzi ni namba waache kugeuza
uchaguzi kama mchezo wa kamari au bingo, uchaguzi ni uamuzi wa wananchi
juu ya mustakabali wao.”

Amesisitiza zaidi kuwa, wananchi hufanya hivyo kabla ya siku ya kupiga
kura, siku ya kupiga kura ndio siku ya kudhihirisha uamuzi wao, lakini
uamuzi wao huanza kufanyika tangu uchaguzi ulipoisha.

Hivyo Katibu Mkuu ameeeleza kuwa, CCM inauona uchaguzi kama zoezi muhimu
sana linalohusu uamuzi wa wananchi juu ya mustakabali wa taifa lao,
uamuzi wa wananchi juu ya wananchi wenzao wanaofaa kuwaongoza kwa
maendeleo yao, uamuzi wa wananchi juu ya chama chenye sifa,
kinachoaminika, kinachoweza, chenye rekodi ya kuongoza nchi na sio
vinginevyo.

Wakati huo huo Dkt. Bashiru amewahakikishia wananchi msimamo wa CCM
kuendelea kuisimamia serikali kutekeleza kila kilichoahidiwa na
kisichotekelezwa huelezwa ni kwa nini hakijatekelezwa, hivyo mwaka huu
ni mwaka wa wanaCCM wote kuueleza umma yote yalioahidiwa yametekelezwa
kwa kiasi gani, yepi yametekelezwa vizuri, yepi yametekelezwa kwa
wastani na yepi ambayo Chama kitaongeza nguvu zaidi.

Aidha Katibu Mkuu ametumia mkutano huo wa ndani kuwataka wenyeviti wa
Vijiji na Mitaa, watendaji wa mitaa na Halmashauri, kuwa wabunifu na
kung’amua fursa za maendeleo, na kwa wakuu wa mikoa na wilaya kusimamia
ubunifu kwa watendaji ili kuwawezesha wananchi kupiga hatua kwa haraka.

Viongozi mbalimbali wakizungumza kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu,
wameonesha kuridhishwa na kasi kubwa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM
licha ya changamoto mbalimbali ambazo wanaendelea kuzishughulikia na
kuzitafutia majawabu ikiwa ni pamoja na kasi ya usambazaji wa umeme
vijijini.

Mkutano huo umehudhuriwa na wanachama, viongozi wa Chama na Serikali
wakiongozwa na Kaimu Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga Ndg. Mohamed Salim
Ratco (MNEC), Mkuu wa Mkoa wa Tanga Ndg. Martin Shigela, wajumbe wengine
wa Halmashauri Kuu Bi. Mwantumu Zodo, na Bi. Catherine Kitandura na
wabunge wa Mkoa wa Tanga.

Katibu Mkuu yupo Mkoani Tanga kwa ziara ya kikazi ya siku nne, ambapo
ziara hiyo imelenga kuimarisha na kuhuisha uhai wa Chama katika ngazi za
Mashina na Matawi.