Waziri mkuu atoa maagizo kwa wizara ya kilimo sakata la malipo ya korosho

WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo ihakikishe asilimia
tatu ya wakulima wa zao la korosho waliosalia wanahakikiwa na kulipwa.


Hadi sasa zaidi ya asilimia 96 ya wakulima wa korosho waliouza korosho zao katika msimu wa 2018/2019 wameshahakikiwa na kulipwa.

Ameyasema
hayo jana (Ijumaa, Januari 3, 2020) wakati alipokutana na baadhi ya
wakulima wa korosho kutoka wilaya za Ruangwa, Masasi na Tandahimba.

Baada
ya kupokea malalamiko kutoka kwa wakulima hao, Waziri Mkuu amewataka
waendelee kuwa na subira na kwamba haki yao itapatikana.

 “Serikali
ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli ipo
makini, hivyo hakuna Mtanzania yeyote atakayepoteza haki yake.”

Kadhalika,
Waziri Mkuu ametoa wito kwa wanachama wa vyama vya ushirika pale
watakapoona ushirika wao hauendi vizuri wasisite kutoa taarifa
Serikalini.

Amewaagiza
wakuu wa mikoa na wilaya wawachukulie hatua viongozi wote wa vyama vya
ushirika watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Kwa
upande wao, wakulima wameishukuru Serikali kwa kusikiliza kero zao na
kuzipatia ufumbuzi na kwamba wanaimani ya kulipwa madai yao.

Mmoja
wa wakulima hao Bi. Mariamu Mganda amesema anamshukuru Waziri Mkuu kwa
kukubali kuwasikiliza kwani wamepata tumaini la kulipwa fedha zao.
Mkulima
Mwingine Bw. Abdulkareem Said amesema ameridhishwa na utendaji kazi wa
Serikali hususan baada ya Waziri Mkuu kukubali kusikiliza kero zao.

(mwisho)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU