Tra yavunja rekodi nyingine kwa kukusanya trilioni 1.987 desemba 2019

Na Veronica Kazimoto-Dar es Salaam.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa mara nyingine, imevunja rekodi kwa
kukusanya jumla ya kiasi cha sh. trilioni 1.987 kwa mwezi Desemba 2019
ambayo ni rekodi ya kwanza kufikiwa tangu kuanzishwa kwake
ikilinganishwa na rekodi ya mwezi Septemba, 2019 iliyokuwa sh. trilioni
1.767.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kamishna
Mkuu wa Mamlaka hiyo Dkt. Edwin Mhede amesema kuwa, makusanyo hayo ya
mwezi Desemba 2019 ni sawa na ufanisi wa asilimia 100.20 kutoka katika
lengo la kukusanya kiasi cha sh. trilioni 1.983 kwa mwezi huo.

“Ni kweli kwamba, kitaalam, miezi tofauti hailinganishiki moja kwa moja.
Hata hivyo, kwa makusanyo haya ya sh. trilioni 1.987 kwa mwezi Desemba
2019, TRA imevunja rekodi yake yenyewe iliyoiandika mwezi Septemba 2019
ambapo ilikusanya jumla ya sh. trilioni 1.767 ikiwa ni sawa na asilimia
97.20 ya lengo la kukusanya sh. trilioni 1.817 katika kipindi hicho,”
alisema Dkt. Mhede.

Akizungumzia makusanyo ya kipindi cha Robo ya Pili ya mwaka 2019/20
inayohusisha mwezi Oktoba, Novemba, na Desemba yenyewe, Kamishna Mkuu
Mhede amesema kuwa, TRA imefanikiwa kukusanya jumla ya sh. trilioni
4.972 sawa na ufanisi wa asilimia 97.49 ya lengo la kukusanya jumla ya
sh. trilioni 5.100.

“Makusanyo haya ya robo ya pili ya mwaka 2019/20 ni sawa na ukuaji wa
asilimia 19.78 ikilinganishwa na kipindi kama hiki cha Robo ya Pili ya
mwaka 2018/19 ambapo Mamlaka ilikusanya sh. trilioni 4.151 ikiwa ni sawa
na ufanisi wa asilimia 87.59 kutokana na lengo la kukusanya mapato
kiasi cha sh. trilioni 4.739 katika kipindi hicho,” alifanunua Kamishna
Mkuu Mhede.

Ameeleza kuwa, kwa upande wa makusanyo ya mapato ya Serikali kwa mwezi
Oktoba 2019, TRA ilikusanya kiasi cha sh. trilioni 1.484 na Novemba
2019, Mamlaka ilikusanya sh. trilioni 1.501 sawa na ufanisi wa asilimia
93.98 na asilimia 97.59 kutoka katika malengo ya kukusanya sh. trilioni
1.579 na sh. trilioni 1.538 kwa mwezi Oktoba na Novemba 2019.

Kamishna Mkuu Mhede ameongeza kuwa, makusanyo hayo ni muendelezo wa
kiashiria cha wazi kwamba Walipakodi na Watanzania walio wengi
wameendelea kuelewa, kukubali, na kuitikia wito wa Serikali ya Awamu ya
Tano wa kuongeza mapato ya ndani kwa ajili ya maendeleo ya Taifa zima.

“Kwa kuwa Walipakodi wengi wameitikia wito wa kulipa kodi kwa mujibu wa
Sheria, ni rai yangu kwamba asiwepo mlipakodi hata mmoja ambaye
atathubutu kubaki nyuma. Ni busara wafanyabiashara wote wakaungana na
kundi kubwa la Washindi, yaani, kundi kubwa la wanaolipa kodi kwa hiari,
kwa ukamilifu, na kwa wakati, alisisitiza Dkt. Mhede.

Pia, amewashukuru walipakodi waliolipa kodi kwa wakati na hivyo
kupelekea kuongezeka kwa makusanyo ambayo yatapelekea utekelezaji wa
miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.

“Kwa namna ya kipekee, napenda kuwashukuru Walipakodi wote waliolipa
kodi ya Serikali na kupelekea Mamlaka kufikia makusanyo haya ya
kihistoria kwa mwezi Desemba 2019. Pia, tunaishukuru sana Serikali ikiwa
ni pamoja na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bodi ya
Wakurugenzi ya TRA, Taasisi za Maendeleo, na Sekta Binafsi kwa kuendelea
kuipatia TRA ushirikiano stahiki katika kutekeleza majukumu yake ya
kukadiria, kukusanya, na kuhasibu mapato ya Serikali,” Alisema Kamishna
Mkuu Mhede.

Aidha, ametoa wito kwa wamiliki wote wa majengo nchini kujitokeza
kulipia kodi za majengo ili kuepuka usumbufu wa kulipa mwishoni mwa
mwaka wa fedha 2019/2020 ambapo amesema kuwa, kwa sasa viwango ni rafiki
na vinalipika kwa urahisi.

Amevitaja viwango hivyo kwa mwaka kuwa ni sh. 10,000 kwa nyumba ya
kawaida, sh. 50,000 kwa kila sakafu ya nyumba ya ghorofa katika Majiji,
Manispaa, na Halmashauri za Miji, na sh. 20,000 kwa jengo la ghorofa
katika maeneo ya Halmashauri za Wilaya.

MWISHO.