Waziri simbachawene ahimiza matumizi ya nishati mbadala kupikia ili kuhifadhi mazingira

Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. George
Simbachawene amehimiza matumizi ya nishati mbadala kupikia ili
kukabiliana na uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji miti kwa
ajili ya kuni na mkaa.

Mhe. Simbachawene ametoa rai hiyo wakati akihutubia wanafunzi na
wananchi katika mahafali ya kumaliza kidato cha nne katika Shule ya
Sekondari Pwaga wilayani Mpwapwa.

Aliwataka wananchi kuacha mara moja kukata miti kwa ajili ya kuni au
mkaa na kusema kuwa vitendo hivyo huchangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko
ya tabianchi.

Mhe. Simbachawene ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Kibakwe alisema kuwa
wakati umefika sasa kwa wananchi kuanza kutumia gesi katika shughuli za
kupika hivyo kuepuka matumizi ya mkaa au kuni ambayo huchangiwa kwa
kiasi kikubwa na ukaaji wa miti.

“Tukiyachezea mazingira tunachezea uhai wetu na ukataji hovyo wa miti
kwa ajili ya kuni na mkaa unaishia kusababisha kumalizika kwa maeneo
yenye miti mikubwa na wengine wanakata miti kwa kiwango kikubwa hata
tukae miaka mingi hatutakuja kupata tena miti kama hiyo,” alisisitiza.

Aidha, Waziri Simbachawene ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kibakwe
wilayani humo aliwapongeza wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani
yao na kuwatia moyo.

Pia alikemea tabia ya baadhi ya wanafunzi wa kike kuanza kushiriki
katika vitendo vya ngono kabla ya umri na kuwataka kuzingatia masomo na
hivyo kufikia malengo yao na kuwaonya wazazi wanaoficha wahusika wa
mimba hizo.

Alionya tabia ya baadhi ya wanaume wanaowarubuni wanafunzi wa kike na
kushiriki nao ngono vitendo vinavyosababisha kuwapa mimba na hivyo
kukatisha masomo yao.

Kwa upande wake Afisa Elimu wa Sekondari Halmashauri ya Wilaya ya
Mpwapwa Nelson Milanzi alitoa mwito kwa wanafunzi na wananchi kwa ujumla
kutunza mazingira.

Afisa Elimu huyo aliwataka kuunga mkono juhudi za Ofisi ya Makamu wa
Rais na Serikali kwa ujumla kutunza mazingira na kupanda miti kwa wingi.