Breaking: mahakama yatupilia mbali maombi ya tundu lissu kupinga kuvuliwa ubunge



Mahakama Kuu Kanda ya Dar, imetupilia mbali maombi ya Tundu Lissu kupinga uamuzi wa Spika wa Bunge, Job Ndugai kumvua ubunge kwa maelezo kuwa alipaswa kuweka pingamizi dhidi ya uchaguzi na si kuomba mahakama ibatilishe uamuzi wa Spika.

Imedaiwa maombi hayo yangesikilizwa hadi mwisho na Lissu kushinda, Jimbo la Singida Mashariki lingekuwa na wabunge wawili ambapo ni kinyume cha Katiba. Pia maombi hayo yemechelewa kuletwa mahakamani.

Akitoa uamuzi huo Jaji Sirilius Matupa leo Jumatatu Septemba 9, amesema maombi ya Lissu hayatekelezeki kwa sababu mleta maombi alitakiwa kufungua kesi ya kupinga uchaguzi mahakamani badala yake wameleta maombi ya kutaka kupinga uamuzi wa spika.

“Mahakama imepata wakati mgumu sana katika kupitia maombi haya kwa sababu kilichotakiwa ni kupinga uchaguzi na lakini hakuna mahali walikofungua kesi mahakamani.

“Tungeruhusu maombi haya hadi mwisho, maana yake Singida Mashariki ingekuwa na wabunge wawili kitu ambacho ni kinyume na Katiba,” amesema Jaji Matupa.