Bunge lapitisha sheria kuwabana wanaotuma au kusambaza picha za maiti au waathirika wa ajali.

Bunge
limepitisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 6
wa Mwaka 2019, ambao pamoja na mambo mengine, upendekeza kuifuta
Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA).


Muswada huo pia unapendekeza kuweka adhabu kali dhidi ya watu wanaotumia au kusambaza picha za maiti au waathirika wa ajali.

Akiwasilisha
muswada huo unaopendekeza marekebisho katika sheria tisa, Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Prof. Adelardus Kilangi, alisema mabadiliko hayo
yanahusisha Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16 iliyotungwa mwaka
1930 kwa lengo la  kuainisha adhabu kwa makosa mbalimbali.

Alisema
tangu kutungwa kwa sheria hiyo, imerekebishwa mara 67 kupitia sheria
mbalimbali na marekebisho ya sasa yanalenga kuongeza adhabu ya faini kwa
makosa chini ya kifungu cha 29 ili kuondoa adhabu zilizopitwa na wakati
kutokana na hali ilivyo sasa.

“Kifungu
kipya cha 162 kinapendekezwa kuongezwa ili kutoa adhabu kwa watu
wanaotumia na kusambaza picha au video za maiti, waathirika wa majanga
na matukio ya kutisha yanayohatarisha amani au kuingilia utu wa mtu,”
alisema.

Alisema
katika muswada aliouwasilisha jana, marekebisho yanalenga kuifuta SSRA
na kuhamisha jukumu la usimamizi wa sekta ya hifadhi ya jamii kwenda
kwenye divisheni inayowajibika kwa masuala ya hifadhi ya jamii.

“Muundo
wa kitaasisi uliopo sasa kwenye Sheria ya SSRA, Sura ya 135
unapendekezwa kufutwa na badala yake majukumu ya usimamizi wa sekta ya
hifadhi ya jamii kuhamishiwa kwenye divisheni hiyo,” alisema.

Prof.
Kilangi alisema eneo la usimamizi wa masuala ya fedha na uwekezaji wa
mifuko litaendelea chini ya uangalizi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT)
kama ilivyo sasa.