Na Seif Mangwangi, Arusha
Hatimaye Mkuu wa Wilaya ya Arusha Said Mtanda amefanikiwa kuzuia zoezi la kubomoa nyumba zaidi ya 200 za wakazi wa mtaa wa Olasiti kati kwa kile kilichokuwa kinaelezwa kuwa ni amri ya mahakama.
Kabla ya tishio la bomoa bomoa hiyo msimamizi wa zoezi hilo dalali aliyetambulika kwa jina la mojaa alitumia silaha yake ndogo ( bastola), kujaribu kutishia wananchi waliokuwa wakihoji uhalali wa amri hiyo ya mahakama kwa kurusha hewani zaidi ya risasi tatu jambo ambalo limelalamikiwa vikali na viongozi wa mtaa na wananchi.
Akizungumza mbele ya mkuu wa wilaya, Mwenyekiti wa mtaa wa Olasiti kati Bruno Mbole amesema kubwa eneo linalotaka kubomolewa kwa madai kuwa ni mali ya kanisa la SDA wasabato ni mali ya wananchi familia ya mzee kisiongoni tangu enzi hizo.
Amesema viongozi wasiokuwa waaminifu waliokuwa wakiongoza mtaa huo wa Olasiti kati walipora ardhi ya wananchi hao kinyemela na kuiuza kwa kanisa la SDA lakini hata hivyo wananchi hao walifikisha malalamiko yao baraza la ardhi la kata na baadae mkoa dhidi ya kijiji na kushinda kesi hizo.
“Tunashangaa sana hawa wanaojiita madalali kuja kutishia wananchi tena kwa risasi kutaka kubomoa nyumba zao, huu sio sawa kabisa, sisi kama serikali tutamshtaki huyu mojaa kwa hiki kitendo chake, kwanza hatujui kama anamiliki kweli hiyo silaha kihalali,”amesema.
Amesema utaratibu wa kutekeleza hukumu ya mahakama ni madalali kufika ofisi ya mtaa na kutoa notisi ya siku 14 lakini madalali hao hawakuweza kutekeleza taratibu hizo na badala yake waliamua kufanya uhuni.
kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Arusha Said Mtanda amewataka mawakili wa pande zote kufika ofisini kwake kesho, Septemba30 na nyaraka zinazotoa uhalali wa umiliki wa eneo hilo.
” Naona pande zote hamueleweki, kesho saa3 mfike ofisini kwangu na nyaraka zenu zote, na mimi nitakuletea mwanasheria wangu asikilize, ndipo tutajua nani ana uhalali wa eneo hili,” amesema.
kwa mujibu wa wamiliki wa eneo hilo, hukumu ya mwisho ilishatolewa na mahakama kuu mwaka 2017 na kuwapatia wananchi hao haki ya kuendelea kumiliki ardhi yao na hawajui hukumu ambayo kanisa la SDA inataka kuitekeleza.
Kwa upande wake Mbunge wa Arusha Mjini Mrisho Gambo amelaani kitendo kilichofanywa na madalali hao na kusema kwa akili ya kawaida huwezi kukurupuka na kuanza kutaka kubomoa nyumba zenye wakazi zaidi ya 100.
” Huu ni uhuni ambao Serikali yetu tukufu inatakiwa kuuzuia kabisa, siku hizi kumeibuka madalali kuchukua sheria mkononi kubomoa bomoa nyumba za watu bila majadiliano yoyote, wanafanya haya mambo kana kwamba Serikali haipo, “amesema.
Amesema kitendo cha dalali huyo (Mojaa) kutishia wananchi kwa risasi hakiruhusiwi kisheria na kutoa wito kwa Serikali kuchunguza umiliki wa silaha hiyo lakini pia jeshi la Polisi kuangalia aina ya watu ambao imekuwa ikiwaruhusu kumiliki silaha.