Na Seif Mangwangi, Arusha
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa
Arusha imekubali kuwapatia dhamana aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dkt
John Pima na wenzake wawili, Mariam Mshana aliyekuwa Mwekahazina wa Jiji la Arusha na Innocent Maduhu aliyekuwa mkuu wa idara ya Mipango, Utafiti na Takwimu wa Jiji hilo kufuatia mashtaka
mawili yaliyokuwa yakiwakabili kuwa na dhamana kisheria.
Hata hivyo washtakiwa hao
wameshindwa kurejea uraiani na kulazimika kurejeshwa mahabusu katika gereza kuu
la Kisongo, kufuatia kushindwa kukamilisha masharti ya dhamana katika shauri namba nne linalowakabili.
Awali Mshtakiwa namba moja, Dkt John Pima na Mshtakiwa namba tatu, Innocent Maduhu walikamilisha nyaraka za dhamana kwa shauri namba 3 linalowakabili huku Mshtakiwa namba tatu, Mariam Mshana akikwama kufuatia hati ya dhamana iliyowasilishwa kwa upande wake kutokidhi vigezo na hivyo kutakiwa kukamilisha.
Kesi hiyo ambayo Februari 28 , 2024
itaanza kutajwa katika mahakama hiyo kwa shauri namba3 na 4, leo Februari 20, 2024 ilifikishwa katika
mahakama hiyo kwaajili ya watuhumiwa kupewa dhamana kufuatia maombi ya upande wa utetezi na taratibu hizo zilipaswa
kuanza mapema lakini upande wa waendesha mashtaka walichelewa kufika
mahakamani.
Ilipofika majira ya saa 7 mchana Hakimu
Mkazi Fadhil Mbelwa aliitisha jalada la Dkt Pima na wenzake kwaajili ya kusikiliza
maombi ya dhamana upande wa utetezi lakini upande wa Jamhuri ulikosa wawakilishi hali
ambayo ilimlazimu Hakimu kumwamuru wakili wa Dkt Pima na wenzake Mosses Mahuna kuwasiliana na
waendesha mashtaka ili Mahakama ijue cha kufanya.
“Hapa naona upande wa
utetezi tu, upande wa Jamhuri uko wapi? Wewe Mheshimiwa wakili najua huwa
mnawasiliana embu toka nje wasiliana na waendesha mashtaka tujue wamefikia wapi
ili tuanze kusikiliza shauri hili, “aliagiza Hakimu Mbelwa.
“Mheshimu Hakimu shauri hili
lilipaswa kuanza kusikilizwa saa6 mchana na mawakili wa Serikali Wana taarifa lakini wakati naingia hapa sikuona
wawakilishi wa Jamhuri na nilijaribu kuwapigia sikuwapata lakini kwa maagizo
yako ngoja nitoke nje niendelee kuwatafuta,”alisema Wakili Mosses Mahuna na
kutoka nje.
Baada ya Wakili Mahuna kufanya mawasiliano, nusu saa baadae mawakili wa Serikali waliweza kufika mahakamani hapo na hivyo upande wa Jamhuri
uliwakilishwa na wakili Safari Mshana na Godfrey Nugu, huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na Mosses Mahuna Pamoja na Sabato Ngogo.
Hakimu mfawidhi mkazi wa mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Fadhili Mbelwa aliwataka mawakili wa utetezi kuwasilisha nyaraka za dhamana kama walivyoomba kwa kuwa shauri hilo Lina dhamana kisheria na kwamba tayari mahakama hiyo 17.06.2022 ilishatoa dhamana na Mshtakiwa namba nne alishapewa dhamana.
Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Godfrey Nugu uliiomba mahakama kutoendelea na dhamana hiyo mpaka watakapo jiridhisha na nyaraka za dhamana zitakazowasilishwa jambo ambalo Hakimu Mbelwa alilikataa kwa hoja kuwa jambo hilo tayari liko mahakamani na mwenye dhamana ya kujiridhisha na uhalali wa nyaraka hizo ni Mahakama.
Kufuatia msimamo huo wa Mahakama, Mwendesha mashtaka wa Serikali Godfrey Nugu alionyesha kutoridhika na maamuzi hayo na kuitaka mahakama kuendelea kwa kuwa imewanyima kuwapatia nyaraka hizo na hata pale Hakimu Mbelwa alipomtaka Nugu kupitia nyaraka hizo mahakamani hapo aligoma na kusema ‘mheshimiwa endelea tu kwa kuwa umeshatugomea ombi letu’.
Mabishano yaliibuka kati ya Hakimu na Mwendesha mashtaka aliieleza mahakama kuwa lengo la kutaka kupitia nyaraka hizo ni kuona kama washtakiwa watakapokuwa nje kama wanaweza kuharibu kesi nyingine ambayo inaendelea kutayarishwa ambayo unaweza isiwe na dhamana dhidi ya washtakiwa hao.
“Mheshimiwa ni kweli dhamana ni haki ya mshtakiwa na sisi tunataka tujiridhishe endapo wakiwa nje hawataweza kuharibu kesi mpya ambayo tunakusudia kuifungua dhidi ya washtakiwa,”amesema.
Hata hivyo Wakili Mahuna aliieleza mahakama kuwa mahakama haijawahi kufanyia kazi shauri ambalo halijafikishwa mahakamani kama ambavyo wakili wa Jamhuri alivyoieleza mahakama na hivyo kumuombea Hakimu kutokubaliana na hoja hiyo.
Baada ya kukamilika kwa dhamana, Hakimu Mbelwa alisoma maamuzi ya mahakama kwamba washtakiwa namba Moja na tatu dhamana yao katika shauri namba tatu imekamilika lakini Mshtakiwa namba tatu Mariam Mshana ataendelea kukaa mahabusu hadi nyaraka zake zitakapokamilika, hata hivyo aliieleza mahakama kuwa washtakiwa wote wataendelea kukaa mahabusu Hadi watakapokamilisha dhamana kwa shauri namba nne linalowakabili.
Nje ya Mahakama
Nje ya Mahakama kuu upande wa Jamhuri ulidaiwa kuonyesha nia ya kukatia rufaa hukumu iliyowafutia mashtaka ya kifungo Cha miaka 20 jela, Dkt Pima na wenzake na wakati huo huo ikitaka kusajili kesi mpya ya utakatishaji wa fedha ili watuhumiwa waweze kukosa dhamana.
Hata hivyo nia zote mbili zilionekana kugonga mwamba na mahakama kuamuru washtakiwa waendelee na mchakato wa kupewa dhamana kwakuwa ni haki yao kisheria.
Wakili wa washtakiwa Sabato Ngogo anasema kilichokuwa kikitaka kufanywa na Jamhuri ni ukiukwaji wa Sheria kwa kuwa dhamana ni haki ya mshtakiwa kikatiba lakini pia kutaka kuwafungulia mashtaka mapya ya utakatishaji wa fedha ni kutaka kuwaumiza watuhumiwa bila sababu za msingi.
“Upande wa Jamhuri ulionyesha nia ya kukatia rufaa hukumu iliyofuta kifungo Cha miaka20 jela lakini haukufanya hivyo, Leo wamekuja wanaiambia mahakama kuwa Wana Nia ya kufungua kesi nyingine ambayo itawanyima dhamana washtakiwa, huu sio utaratibu na huko ni kubaka katiba, kinachofanyika hapa ni kutaka tu kuonea washtakiwa lakini Sheria Iko wazi kabisa,”amesema Wakili Ngogo.