Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Mkurugenzi wa Halimashauri ya Manispaa ya Shinyanga Jomaari Satura amesema serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya Elimu ili kuweka mazingira wezeshi kwa walimu kufundisha na wanafunzi kujifunzia lengo likiwa ni kuinua kiwango cha ufaulu.
Ameyasema hayo wakati akitoa salamu za pongezi kwenye hafla ya kuipongeza shule ya Msingi Ujamaa iliyopo katika Kata ya Mwamalili Manispaa ya Shinyanga kwa kupata ufaulu mzuri katika mtihani wa darasa la saba mwaka huu 2021.
Mkurugenzi Satura ameeleza kuwa kwakuwa serikali imetoa pesa kwa Manispaa ya Shinyanga kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu hivyo ni vyema viongozi wa Manispaa kuhakikisha kuwa fedha hizo zinaleta matokeo chanya kama ilivyokusudiwa.
“Serikali imejipanga kuhakikisha `watoto wanapata elimu bila malipo hivyo inaendelea kuboresha ustawi wa maisha ya kila mtu ili kupunguza hali ya kutokujua kusoma na kuandika”.
“Serikali imetoa kiasi cha fedha Milioni mia nane na themanini katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kwa lengo la kuboresha sekta ya elimu niwaombe tuendelee kuunga mkono jitihada zote zinazotolewa na serikali ili kufikia malengo yaliyokusudiwa”.
Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Shinyanga Elias Masumbuko amewataka wazazi kuwatia moyo watoto wao ili wapende elimu na kuweza kutimiza ndoto zao ikiwa ni pamoja na kushirikiana na walimu ili kuwezesha ufaulu mzuri kwa watoto hao.
Meya huyo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo ya kuwapongeza walimu na wanafunzi waliofanya vizuri matokeo ya darasa la saba na kuiwezesha Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kuwa ya kwanza kimkoa.
Sherehe hiyo ilifanyika katika shule ya msingi Ujamaa iliyopo kata ya Mwamalili Manispaa ya Shinyanga ambayo shule hiyo imeshika nafasi ya kwanza matokeo ya mitihani ya darasa la saba mara mbili mfililizo katika shule za serikali na kuiweka Manispaa hiyo kuwa ya kwanza kimkoa huku mwaka jana matokeo ya darasa la saba Shinyanga ilishika nasafi ya 17 kitaifa.
Amesema watumishi sekta ya elimu katika Manispaa ya Shinyanga wametakiwa kujenga mahusiano mazuri kwa kushirikiana, kupendana na kuwajibika katika nafasi zao ili kuendelea kuleta matokeo chanya kwa wanafunzi katika shule zote.
Masumbuko amesema njia pekee inayoweza kuleta matokeo chanya katika sekta ya elimu ni kufanya kazi kwa bidii, kuwajibika kila mtu katika nafasi yake kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza miongozo ya ufundishaji shuleni hasa walimu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa kimkoa na Taifa kwa ujumla.
Amewataka maafisa elimu kata kuwajibika na kuhakikisha kwamba wanafunzi wanapata elimu sahihi inayostahili ili kutengeneza Taifa imara.
Aidha Masumbuko amewaomba wazazi kutowakatisha tamaa watoto amabapo amesema baadhi ya wazazi hawapendi maendeleo ya watoto wao hasa watoto wa kike ambao wengi wanashidwa kufikia malengo kwa kukatishwa tamaa kuwa hawajui kusoma ili wasiendelee na masomo hivyo amewataka wazazi kutoa ushirikiano mzuri kwa watoto wao bila kuangalia matokeo hasi.
Akizungumza katika hafla hiyo afisa elimu taaluma Manispaa ya Shinyanga Essau Ezekiel Nyeringa ameyataja baadhi ya malengo yaliyochangia ufaulu huo katika Manispaa ya Shinyanga ikiwemo ufaulu kwa wanafunzi kuongezeka mwaka hadi mwaka, kuhakikisha wanafunzi wote waliosajiliwa kufanya mtihani wa darasa la saba na la nne wanafaulu kwa asilimia mia pamoja na kuhakikisha wanafunzi wote waliosajiliwa kwa darasa la pili na la kwanza wanamudu stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu.
Aidha Nyeringa amesema ipo mikakati ya pamoja waliyojiwekea ili kuipeleka Halmashauri ya Manispaa hiyo katika ufaulu wa shule kumi bora kitaifa ambapo amesema wamejiwekea utaratibu wa kuhakikisha wanadhibiti utoro kwa walimu na wanafunzi, shule zote kutoa huduma ya chakula pamoja na kila shule kupangiwa asilimia za ufaulu kulingana na mazingira kwa kila mwaka na kujaza fomu za mkataba.
Katika hafla hiyo Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imezipongeza shule zote zilizopata matokeo mazuri katika mtihani wa darasa la saba mwaka jana 2020 na kuiweka Manispaa hiyo kushika nafasi ya 17 kitaifa baadhi ya shule hizo ni shule ya msingi Lubaga, Mwenge, Jomu, Little Treasures, Samuu na Hope ambapo shule zilizofaulisha vizuri ni shule ya msingi Ujamaa, Town school, Kolandoto, Wame, Mapinduzi A, Mwasele, Mapinduzi B, Kom, Ibadhi, Balina, St. Anne pamoja na Shinyanga Modern huku baadhi ya shule zilizofanya vibaya mtihani huo ni shule ya msingi Mwamapalala, Bugwandege, Lyandu, Negezi, Bushola na Chibe.
Uongozi wa Halmashauri hiyo pia umempongeza mkuu wa idara ya elimu msingi wa Manispaa ya Shinyanga Neema Mkanga kwa usimamizi mzuri wa shughuli zilizopelekea shule hizo kupata ufaulu mzuri wa matokeo ya darasa la saba.
Naye mkuu wa shule ya msingi Ujamaa Japhet John Jasson akieleza historia fupi ya shule hiyo amesema shule imekuwa ikifanya vizuri kwenye matokeo ya darasa la saba kitaifa kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
“Shule ya msingi Ujamaa iliyopo katika Manispaa ya Shinyanga ni miongoni mwa shule za zamani ambazo zimekuwepo baada ya uhuru wa Tanganyika tarehe 9 mwezi Disemba mwaka 1961 ilianzishwa mnamo mwaka 1972 Shule ya awali ya msingi Ujamaa imekuwa ikifanya vizuri kwenye matokeo ya mtihani wa kitaifa kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita”
“Mwaka 2018 wanafunzi waliosajiliwa ni 40 waliofanya mtihani 40 waliofaulu 40 asilimia mia moja (100) wastani wa daraja A, Mwaka 2019 waliosajiliwa 55 waliofanya mtihani 55 waliofaulu 53 waliofeli 2 asilimia 96 wastani wa daraja A, Mwaka 2020 waliosajiliwa 40 waliofanya mtihani 40 waliofaulu 40 asilimia 100 wastani wa daraja A, Mwaka 2021 waliosajiliwa 56 walifanya mtihani 56 waliofaulu 56 asilimia 100 wastani daraja A.