Kamanda muliro aanika kanuni inayotumika kufanya uhalifu, dc jokate ataka ulinzishi shirikishi temeke

Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Jumanne Muliro (aliyesimama) akizungumza wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha viongozi wa Wilaya ya Temeke, maofisa wa Jeshi la Polisi pamoja na Wenyeviti wa Serikali za mitaa ndani ya wilaya hiyo.Kikao hicho kililenga kuweka mikakati ya kukabiliana na matukio ya uhalifu katika mitaa mbalimbali ambapo Kamanda Muliro amesisitiza ulinzi ni jukumu la kila mwananchi.Wa pili kushoto katika picha ni Mkuu wa Wilaya hiyo Jokate Mwegelo na wakwanza kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Temeke Elihuruma Mabelya.


Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo(aliyesimama) akitoa maelekezo kwa wenye viti wa Serikali za mitaa katika wilaya hiyo kuhakikisha ndani ya siku saba mitaa yote ambayo haina ulinzi shirikishi wawe wameanzisha sambamba na kuwakumbusha wajibu wao katika kusimamia ulinzi na usalama katika mitaa yao.


 

Baadhi ya maofisa wapya wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ambao wamepangwa kutekeleza majukumu yao katika baadhi ya Mitaa ya Halmashauri ya Wilaya ya Temeke wakiandika maelezo ya maelekezo yaliyokuwa yakitolewa kwenye kikao kazi hicho ambacho kilihusisha wenyeviti wote wa Serikali za mitaa katika wilaya hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo(katikati) akijadiliana jambo na Mwenyekiti wa Wenyeviti katika Wilaya hiyo wakati wa kikao hicho.Kushoto ni moja ya maofisa wa jeshi hilo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam Elihuruma Mabelya akizungumza wakati wa kikao hicho kilichowakutanisha wadau wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wenyeviti wa Serikali za mitaa pamoja na watendaji wa halmashauri hiyo  kujadili namna ya kuimarisha ulinzi na usalama .


Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam akielezea kwa kina namna ambavyo wameendeelea kuchukua hatua katika mitaa yao kukabiliana na vitendo vya uhalifu pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama
Washirki wa kikao hicho wakiwemo maofisa wa jeshi la Polisi Mkoa wa Temeke pamoja na Wenyeviti wa Serikali za mitaa katika wilaya hiyo wakiwa wamesimama baada ya kumalizika kwa kikao kazi ambacho kiliitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo (hayuko pichani) ambapo pia walimualika Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Jumanne Muliro.

Na Said Mwishehe, Michuzi TV

KAMANDA wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Jumanne Muliro ameweka hadharani kanuni  inayotumiwa na watu wanaojihusisha na matukio ya uhalifu kwenye maeneo mbalimbali.

Wakati Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo akitoa siku saba kuhakikisha mitaa yote ya Wilaya hiyo inakuwa na polisi jamii (ulinzishi shiriki) kwa lengo la kukabiliana na vitendo vya kihalifu.

 

Hayo wameeleza leo Aprili 29,2022 katika kikao kazi kilichowakutanisha viongozi wa Wilaya ya Temeke, Jeshi la Polisi pamoja na wenyeviti wote wa Serikali za mitaa katika wilaya hiyo ambapo kwa sehemu kubwa wamehimizwa kuanzisha polisi jamii.

Akizungumza katika kikao hicho, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Jumanne Muriro amesema masuala ya usalama wa nchi kwa ujumla hayawezi kuelekezwa na kuachiwa vyombo vya ulinzi na usalama pekee  bali ni jukumu la kila mwananchi.

Hivyo amesema kuna kila sababu ya kuangalia mfumo wa kuimarisha mfumo wa usalama katika maeneo mbalimbali na kila mwananchi anatakiwa kushiriki.

”Katiba ya nchi ibara ya 28 inaelezea umuhimu wa kila mmoja wetu kuwa mlinzi wa Taifa hili, lakini pia Sheria ndogo ya halmashauri ya Wilaya ya Temeke inazungumzia suala la usalama,”amesema Kamanda Murilo.

 Amefafanua kuna baadhi ya watu wanatoa hoja kuwa kazi ya usalama ni ya jeshi la polisi kwani ndio wanaolipwa mshahara kwa kazi hiyo lakini ukweli jukumu la kulinda usalama wan chi ni la kila mwananchi.

” Ndugu zangu wa serikali za mtaa ninyi mnafahamu idadi ya askari tulionao na hali halisi.Hakuna mfumo unaowezesha kila mtaa kuwa na Polisi.Fikra za kwamba polisi ndio wenye jukumu la kulinda usalama linatoa fursa kwa wahalifu kufanya uhalifu.

“Maeneo yaliyoitikia mwito wa kufanya ulinzi shirikishi yameendelea kuwa salama na yale yenye fikra usalama ni kazi ya Polisi yamekuwa na uhalifu, kwasababu yanakuwa rahisi kufanyika uhalifu,”amesema.

Aidha amesema kuna hoja zinazotolewa na wanaoshiriki ulinzi shirikishi kuwa wahalifu wanakwenda na dhana ya kivita kama bunduki au mapanga , hivyo watawezaje kukabiliana nao.

“Ili mhalifu afanye tukio kihalifu kuna kanuni  wanayoitumia ambayo ina vitu vitatu , kwanza awepo  mhalifu, awepo anatendewa uhalifu na tatu fursa ya kufanya uhalifu.

 “Muunganiko huo ukiwepo ndio tukio la  kihalifu linafanyika.Tunachokifanya sasa ni kuziba fursa ya mtu kufanya uhalifu kwa kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi.

“Ukishakuwa na kikundi cha ulinzi shirikishi, mhalifu atakuwepo na mtendewa uhalifu atakuwepo lakini fursa ya kufanya uhalifu haitakuwepo, hivyo uhalifu hautafanyika.

“Mkiwa na ulinzi shirikishi hamuwezi kupambana kwasababu mhalifu ili afanye vitendo vya uhalifu lazima afanye uchunguzi kujua kama kuna fursa ya kufanya uhalifu? Akigundua ipo ndio anafanya,”amefafanua.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo ametoa maelekezo kwa wenyeviti wote wa Serikali za mitaa ndani ya wilaya hiyo katika kipindi cha siku saba wawe wameanzisha ulinzis shirikishi.

 “Wenyeviti wa serikali za mitaa mlioko kwenye kikao hiki hamko hapa kwa mbaya bali mmetajwa kwenye Katiba, mmetajwa kwenye Ilani ya CCM, mmetajwa katika sheria ndogo ya manispaa ya temeke na mmetajwa katika Sheria ya serikali za mitaa.Hivyo ni wajibu wetu kushiriki katika ulinzi katika meneo tunayotoka,”amesema Jokate.

Amesema kwa mujibu wa Sheria ndogo ya Halmashauri ya Wilaya ya Temeke ulinzi shirikishi ni jambo la lazima na sio utashi wa kiongozi. “Utekelezaji wa sheria hii namba 216 sheria ndogo iliyotungwa na Temeke kuhusu ulinzi shirikishi.

“Sio utashi wa kiongozi kuamua tuwe nao au  tusiwe nao, ulinzishi shirikishi lazima uwepo.Hivyo natoa siku saba mitaa isiyokuwa na ulinzi shirikishi kuitisha vikao vya dharura vya usalama na ulinzi wa mtaa waweke mkakati wa kuwa na ulinzi shirikishi.

“Pia natoa wiki moja  maeneo yenye ulinzi shirikishi lakini unasuasua lazima wachukue ya kujitathimini,”amesema Jokate na kuongeza maelekezo kwa wenyeviti wote kuhakikisha wanashiriki katika ulinzi na usalama.

Amesema wale ambao hawawajibiki katika suala la  ulinzi katika mitaa yao wanatia shaka.”Sasa kwa wale wasioshiriki katika kusimamia ulienzi kwenye mitaa yao wajitathimini.”

Amesisitiza kuwa vitendo vya uhalifu huwa vinaanza kidogo kidogo na visipodhibitiwa mapema yanafanyika matukio makubwa ya uhalifu, hivyo jamii ikishikiriki kikamilifu matukio hayo yatatoweka na Wilaya kubaki salama.

“Nadhani mmesikia maeneo mengine huko kuna panya road, hapa kwetu Temeke lazima tuseme hapana na tutafanikiwa kwa kila mmoja wetu kuchukua hatua kwa kushiriki katika ulinzi.”amesema.