* Mawaziri wapongeza Global Education Link
*Abdulmalik Mollel asema wahitimu wameiva vya kutosha
*Jumanne Sagini asema Global Education Link ni ya viwango
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imepongeza mchango wa Global Education Link (GEL) kwa namna ambavyo imekuwa ikisaidia kuwaunganisha wanafunzi wa Tanzania kusoma taaluma mbalimbali vyuo vikuu vya nje ya nchi.
Pongezi hizo zilitolewa mwishoni mwa wiki na Naibu Waziri wa Elimu, Omary Juma Kipanga, wakati wa mahafali ya tatu ya wanafunzi waliosoma nje ya nchi yaliyoandaliwa na Global Education Link.
Mahafali hayo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City siku ya Jumapili yalihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Jumanne Sagini na mabalozi mbalimbali wanaowakilisha nchi zao.
Naibu Waziri alisema taasisi hiyo mbali na kuwaunganisha wanafunzi wa Tanzania na vyuo vikuu nje ya nchi pia imekuwa ikifuatilia kwa karibu maendeleo yao ya kitaaluma ili kuhakikisha wahitimu vyema masomo yao.
Alisema hata wakati wa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine Global Education Link ilisimamia mchakato mzima wa kuhakikisha wanafunzi wote wa Tanzania wanarejea nchini wakiwa salama kwa kushirikiana na serikali na wazazi.
” Hata vitabu vya dini vinatueleza kwamba asiyeweza kumshukuru binadamu hawezi kumshukuru Mungu. Mollel Serikali inakupongeza sana kwa jitihada na uzalendo wako kusaidia nchi yako umefanya mambo makubwa sana kwenye elimu,” alisema
“Kila mmoja wetu hapa anatambua namna vita vya Ukraine vilivyoleta taharuki hapa nchini lakini kwa namna ulivyosimama na wazazi kuhakikisha watoto wote wanarudi salama tunakupongeza sana kwa moyo wako wa uzalendo,” alisisitiza Naibu Waziri
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel aliomba apelekewe changamoto zinazowakabili wahitimu wa vyuo vikuu nje ya nchi ili azifanyie kazi na wataalam wake wizarani.
Alitoa agizo hilo kwa taasisi ya Global Education Link (GEL) kufuatia changamoto mbalimbali zilizotolewa na Mkurugenzi wa GEL Abdulmalik Mollel kwenye mahafali hayo.
“Mollel umetaja changamoto nyingi niandikie nileteee wizarani nitaitisha kikao na wataalamu wangu tutatue changamoto moja baada ya nyingine tunataka kuwasaidia wazazi ambao wamejitahidi sana kusomesha watoto wao, “ alisema Dk Mollel
Alisema serikali imewekeza kiasi kikubwa kwenye sekta ya afya zikiweno trilioni 1.3 zilizotolewa kupambana na UVIKO 19 hivyo wataalamu hao wanahitajika sana kwenye maeneo mbalimbali.
Alitaka wahitimu hao watembezwe kwenye Taasisi ya Moyo ya JKCI, Muhimbili na Mlonganzila kuona uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali ili wasiwe na ndoto za kufanyakazi nje ya nchi.
” Kuthibitisha hill juzi Waziri wa Afya wa Malawi alikuja nchini akaja JKCI kuangalia uwekezaji tulioufanya alishangaa mambo makubwa na tumekubaliana walete wagonjwa wao hapa badala ya kuwapeleka Ulaya na India,” alisema
Dk Mollel aliwataka wahitimu hao kubuni mambo yatakayowaingizia kipato kwa kujiajiri na kuajiri wengine badala ya kuwa na mawazo ya kuajiriwa pekee.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Jumanne Sagini aliipongeza GEL na Mkurugenzi wake Mollel kwa namna ambavyo wamekuwa wakifuatilia maendeleo ya wanafunzi nje ya nchi.
Alisema taasisi hiyo ndiyo inaongoza kwa ubora katika wakala wanaowaunganisha wanafunzi kwenda kusoma nje ya nchi kutokana na namna inavyowafuatilia kujua maendeleo yao.
Aliwataka wanafunzi wanaokwenda nje ya nchi kuzingatia sheria za nchi husika ili kuepuka misukosuko wanayoweza kuipata wanapovunja sheria
Mkurugenzi Mtendaji wa GEL Abdulmalik Mollel alisema asilimia 50 ya wahitimu hao wamesomea fani ya afya ikiwemo udaktari na ufamasia
Aliomba serikali itoe mikopo kwa wanafunzi wanaosoma nje ya nchi kwani nao watakuja kuijenga nchi mara wanapohitimu masomo yao
Alisema wazazi wengi wanaosomesha watoto wao nje ya nchi hawana kipato kikubwa isipokuwa wamekuwa wakijibana na kuachana na mambo mengine ili kufanikisha elimu kwa watoto wao
Alisema wahitimu hao wameiva vya kutosha kuweza kufanyakazi eneo lolote hivyo aliwaomba waajiri ikiwemo serikali kuwachukua kwenye nafasi hizo
Mheshimiwa Waziri nikuhakikshie hawa wahitimu ni bora na wamehitimu kutoka vyuo bora kabisa duniani wajaribu kwa kuwachukua na kuwapa nafasi mbalimbali mtaona kazi kubwa watakayofanya