Mahakama yamtia hatiani mchungaji mwenye wake watatu

Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam  imemuhukumu Mchungaji wa Kanisa
la The Early Church of Lord Yeshwah, David Chirhuza (33) kulipa faini ya
Sh2 milioni au kutumikia kifungo cha miaka miwili.

Wakati huohuo, mahakama hiyo imewahukumu Eather Sebuyange (27), Kendewa
Ruth (26) ambao ni wake wa mchungaji huyo na Samwel Samy (22) kulipa
faini ya Sh1 milioni au kwenda jela mwaka mmoja kila mmoja.

Akitoa Hukumu hiyo leo Jumanne Septemba 10, 2019 Hakimu Mkazi Mwandamizi
Augustina Mmbando amesema baada ya kulipa faini au kutumikia kifungo
hicho watuhumiwa hao wanatakiwa kurudishwa nchini kwao.


Wakili
wa Serikali kutoka Uhamiaji Godfley Ngwijo  akisaidiana na Sitta Shija,
wakisoma mashtaka kwa nyakati tofauti walidai kwamba, Septemba 2 mwaka
huu eneo la Salasala Kilimahewa, Dar es Salaam, mchungaji huyo na
wenzake walibainika kuingia nchini bila kibali.

Katika shtaka la pili, ilidaiwa mchungaji huyo pekee alibainika  kujihusisha na kazi za kanisa akiwa hana kibali cha makazi.

Baada
ya kusomewa mashtaka hayo, Mchungaji David alikiri shtaka la kwanza la
kuingia nchini bila kibali na kukiri shtaka la pili kufanya kazi ya
uchungaji huku akiwa hana kibali cha makazi.

Washtakiwa wengine walikiri shtaka la kuingia nchini bila kibali.