Mwanamke amuua shemeji yake aliyemzaba kofi kwenye makalio yake

Polisi eneo la Suna Magharibi, kaunti ya
Migori nchini Kenya wanamsaka mwanamke mwenye umri wa makamo
aliyetoweka baada ya kumdunga kisu shemeji yake. 

Eunice Adhiambo alitekeleza kisa hicho baada ya mabishano makali kuzuka baina yake na shemejiye mnamo Jumanne, Disemba 24,2019. 

 Kulingana na chifu wa eneo hilo Yogo
Tumbo, marehemu alikuwa amemtembelea mshukiwa ambaye alimkuta akimenya
mihogo kulingana na ripoti ya Citizen TV.

 Inadaiwa, jamaa aliyejaribu kujadiliana
kuhusu jambo fulani ambalo bado halijajulikana alimzaba kofi Eunice
katika makalio yake baada ya kuhisi mshukiwa alikuwa akimpuuza.

 Punde si punde, mshukiwa anadaiwa
kumrukia marehemu na kumdunga kisu mara kadhaa kifuani akitumia kisu
alichokuwa nacho mkononi.

 Chifu huyo alidokeza kwamba, marehemu
alifariki papo hapo na mwili wake umehifadhiwa katika makafani ya
hospitali ya Migori Level Four ukisubiri upasuaji.