Sheria ya habari kujadiliwa januari na bunge

Waziri wa habari na teknolojia ya mawasiliano Nape Nnauye akimkabidhi tuzo mwandishi Bakari Chijuba katika kongamano la wanahabari lililokuwa likifanyika Jijini Dar es salaam Leo Disemba17,2022

 

Na Mwandishi Wetu, Dar es salaam

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Moses Nnauye (mwandishi), amewahakikishia wanahabari kuwa kikao kijacho cha bunge kitapeleka marekebisho ya sheria ya huduma za habari ya mwaka 2016.

Alieleza hayo wakati akifungua kongamano la maendeleo ya sekta ya habari mwaka 2022, lenye kauli mbiu ‘habari kwa maendeleo endelevu’, lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es salaam

Alisema katika bunge litakaloanza Januari mwakani, wizara hiyo inatarajia kupeleka marekebisho ya sheria hiyo ili ifanyiwe marekebisho katika baadhi ya vifungu, hali ambayo itakuza uhuru wa habari.

Nape alieleza kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, itashirikiana na vyombo vya habari na kwamba itawezesha kuweka mazingira mazuri na kuondosha vikwazo kwa wanahabri.

Mkurugenzi wa UTPC Keneth Simbaya wa kwanza mstari wa mbele akifuatilia mjadala katika kongamano hilo

Nape aliwashauri wadau wa habari waone ipo haja ya kuzioanisha sheria ya habari na sheria ya utangazaji, ili tasnia hiyo ifanye kazi vizuri, kwa weledi na ufanisi mkubwa kwa vile wote ni wanajukumu la habari.

Aliongeza kuwa sekta ya habari inaendelea vizuri na uhuru wa habari umeimarika, kwani hakuna hakuna mwandishi aliyepotea, hakuna anayefinywa, ambapo Rais Samia amefanya mabadiliko makubwa katika kukuza uhuru wa habari nchini.

Katika Waziri Nape alitoa maagizo matano kwa wadau hao kuwa sekta ya habari ni muhimu hivyo wizara itaendelea kushirikiana na kutatua changamoto mbali mbali zinazowakabili zitafanyiwa kazi.

Alisema mwaka unafuata nguvu zaidi zitawekwa kwa ajili ya maslahi ya waandishi wa habari ikiwemo masuala ya bima, ambapo alimtolea mfano mwandishi wa TBC aliyefariki baada ya kupanda mlima Kilimanjaro Kapembe ambae ameacha familia itaangaliwaje.

Alieleza kuimarishwa kwa uchumi wa vyombo vya habari, mikataba ya ajira na taasisi kulipa madeni wanaodaiwa na media.

Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari Arusha Claud Gwandu kushoto na Makamu Mwenyekiti Mussa Kuna pamoja na mwanahabari Zanura Mollel wakiwa katika picha ya pamoja katika kongamano hilo.

Sanjari na kuvihimiza vyombo vya habari kufanya kazi kwa kuzingatia miiko, maadili na utamaduni wa nchi na wajibu wa kulinda rasilimali za nchi ili zisitumike vibaya na kusababisha mvurugano.

Alisema kongamano hilo litakuwa endelevu na litafanyika kila mwishoni mwa mwaka ambalo litaboreshwa na liwe la Kongamano la kimataifa naaendeleo ya sekta ya Habari.

Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Jim Yonazi alisema jukumu la Wizara wakati wa matumizi ya Tehama kuleta mabadiliko ya kiuchumi kupitia Teknolojia ya Mawasiliano nchini.