Washushwa vyeo kwa kujiandikia posho

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga Sporah Liana akiwa na Meya wa Jiji la Tanga Abdulrahaman Shiloow kwenye mkutano wa Baraza la Madiwani.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga Spora Liana amewaondoa Waganga wafawidhi katika Vituo vya Afya katika Halmashauri ya Jiji la Tanga baada ya kuweka maslahi yao binafsi na kujiandikia posho kwenye matumizi ya fedha za Hosptali na kuacha kununua vifaa tiba na Dawa.


Hatua hiyo imezifanya Vituo hivyo vya Afya kushindwa kujinunulia Dawa na Vifaa tiba mbalimbali ambayo vingewasaidia Wananchi pindi wanapokwenda kufuata huduma kwenye vitu hivyo.


Hayo yamejiri leo kwenye kikao cha robo ya tatu ya baraza la Madiwani iliyofanyika katika Halmashauri hiyo,baada ya Diwani wa Majengo Salimu Perembo kuuliza swali kuhusu Umeme wa ziada kwenye vituo vya Afya,wakati wa kufanya upasuaji kama Umeme ukikatika. 


Akijibu swali hilo mkurugenzi wa Jiji Spora Liana amesema kuwa ameshachukua hatua kwa ajili ya kumaliza kero hizo kwa kuwaondoa waganga wafawidhi wote waliokuwepo na kuwaweka wengine na wameshawapa mikakati.


“Utaona hivi karibuni kwenye hivi vituo kuna watumishi tumewaondoa baaada ya kuona matumizi makubwa ambayo ni poshoposho tu,baada ya wao kununua dawa wao wanaweka posho zao,hivyo tumewaondoa wale waganga wafawidhi na tumewaweka wengine,kwa hiyo tunawasimamia na tumewapa mikakati wahakikishe wananunua jenereta,hata kama jenereta ni kuanzia millioni hamsini na kuendelea hawawezi kushindwa kwa sababu kuna vituo vinapata mpaka millioni Mia na zaidi hivyo hawatashindwa kununua”alisema Liana 


“Unajua hivi vituo vya afya na zahanati wanapokea pesa za papo kwa papo nyingi sana,Makorora tumenunua Jenereta kwa zaidi ya millioni sitini,vituo vya Afya vinaweza kukusanya hela na kununua Jenereta,Bajeti tumeshapitisha na hatukuweka na tumeanza kusimamia hivi vituo vianze kukusanya fedha,tumeanza kusimamia vituo na kuondoa matumizi yote ya hovyohovyo kwenye vituo,matumizi ni kununua Dawa,Vifaa na vifaa ikiwemo Jenereta”alisema Liana

Waganga wafawidhi hao wamekumbwa na majanga hayo baada ya kushindwa kufanya manunuzi ya Dawa,huku vituo hivyo vikiwa na changamoto za Jenereta,na zikiwa zinaingiza mapato yanayoweza kuleta mabadiliko katika sekta ya Afya kwa kununua vitu muhimu.