Ahukumiwa adhabu ya kifo kwa kumuua mwenzake kisa kamnyima supu ya kuku


Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya
Mtwara, imemuhukumu adhabu ya kifo mkazi wa Kata ya Chikonji, Manispaa
ya Lindi, Mohamedi Hassani Omari (45), baada ya kukutwa na hatia ya
mauaji ya kukusudia dhidi ya Andrew Ndemba (Mtanzania) kisa alimnyima
supu ya kuku.

Hukumu hiyo imetolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Paul Ngwembe,
baada ya ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka kuthibitishwa bila
kuacha Shaka yeyote.
Jaji Ngwembe akitoa hukumu katika kesi hiyo namba 48/2016, kupitia
kifungu cha Sheria namba 196 kanuni ya adhabu sura ya 16/2002,
alimuhukumu Mohamedi Hassani Omari (45), adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
Mwanzoni ilidaiwa mahakamani hapo na Mwanasheria wa Serikali, Emmanuel
John, kuwa Mohamedi Hassani Omari alifanya mauaji hayo Aprili 07/2016
usiku,baada ya Andrew Ndemba maarufu (Mtanzania) kukataa kumnunulia Supu
ya kuku.
Alisema siku hiyo ya tukio, Mohamedi Hassani Omari akiwa ameongoza na
mpenzi wake, walifika nyumbani kwa rafiki yao na walikumkuta marehemu
akiwa anakunywa supu ya kuku, na kuomba amnunulie lakini alijibiwa hana
fedha.
Wakili John ameeleza kuwa majibu hayo, yalimchukiza mshitakiwa Mohamed
ndipo mzozo ulipoanza huku akimpa kauli za vitisho kuwa atamuonyesha,
ambapo marehemu alilipiga teke sufuria la supu, kisha kuondoka eneo lile
akiwa na rafiki yake Issa Abdallah.
Alisema wakiwa wanaelekea nyumbani kwao, mshitakiwa alichukuwa panga na
kwenda kuwavizia njia ambayo walikuwa wakiitumia kupita na walipokaribia
eneo alilosimama mshitakiwa aliwasimamisha, na kutekeleza azmio lake la
kuua.
Chanzo – EATV