Andengenye kutoa ushirikiano ajira za wapanda mlima kilimanjaro

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (CGF) Thobias Andengenye akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Sogwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela (hayupo pichani).
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (CGF) Thobias
Andengenye akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Sogwe Brig. Jen. Nicodemus
Mwangela mapema leo wakati wa ziara yake Mkoa wa Songwe.
Mkuu wa Mkoa wa Sogwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela akimsikiliza Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (CGF) Thobias Andengenye (aliyesimama) mapema leo ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe.
…………………..
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (CGF) Thobias
Andengenye ameahidi kutoa ushirikiano katika kutekeleza agizo la Rais
wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli la kutoa
ajira kwa vijana wazalendo waliopanda Mlima Kilimanjaro.
Andengenye ametoa ahadi hiyo
mapema leo kwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela
alipofika ofisini kwake ikiwa ni sehemu ya ziara yake Mkoani Songwe
kukagua utendaji wa jeshi hilo Mkoani hapa.
 “Suala la ajira za vijana
wazalendo waliopanda Mlima Kilimanjaro ili kumuenzi Baba wa Taifa Hayati
JK Nyerere kwa sasa linashughulikiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,
Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu na watakaponiletea majina niko
tayari kutoa ushirikiano.”, amesema Andengenye.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig.
Jen. Nicodemus Mwangela amesema wakati wa kilele cha Mbio za Mwenge wa
uhuru kilichofanyika Mkoani Lindi Oktoba 14, 2019 Mhe Rais aliagiza
Vijana wazalendo ambao walipanda mlima Kilimanjaro na hawana ajira
waangalie namna ya kuajiriwa.
“Tutashukuru sana endapo
vijana wetu hawa wazalendo watafanikiwa kupata Ajira, Nchi nzima
walipanda vijana 84 kwetu Songwe tulitoa vijana 21 kati yao vijana ambao
hawana ajira ni vijana sita kutoka Songwe.”, amesema Brig. Jen.
Mwangela.
Wakati huo huo Andengenye
amesema kuna mikakati ya kitaifa ya kuboresha utendaji wa jeshi la
Zimamoto na Uokoaji na katika Mikakati hiyo Mikoa mipya kama Songwe
itapewa kipaumbele hasa katika kuongezewa vifaa na watendaji.