Balozi sokoine amuwakilisha waziri simbachawene kuzindua mfumo wa ukusanyaji takwimu za gesijoto

Naibu
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Balozi Joseph Sokoine amezindua
Mfumo wa Kitaifa wa Ukusanyaji Takwimu za Gesijoto, Ufuatiliaji,
Uandaaji Taarifa na Uhakiki katika Ukumbi wa Kituo cha Kuratibu Hewa
Ukaa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) mkoani Morogoro.


Akizindua
mfumo huo kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa ais (Muungano
na Mazingira) Mhe. George Simbachawene, Balozi Sokoine alisema kuwa
utawezesha nchi kukusanya takwimu za gesijoto kutoka sekta mbalimbali
kwa ajili ya kuchukua hatua stahiki na maamuzi.

Pamoja
na mambo mengine alisema pia utasaidia kuandaa taarifa mbalimbali
ambazo nchi inatakiwa kuandaa kama Mwanachama wa Mkataba wa Umoja wa
Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi ambazo zinabainisha kiasi cha
uzalishaji wa gesijoto kutoka sekta mbalimbali husika na uondoshaji wake
kupitia misitu.

Balozi
Sokoine aklibainisha kuwa hadi sasa Tanzania imeandaa taarifa mara
mbili na kuwasilisha Sekretareti ya Mkataba mwaka 2003 na ya pili mwaka
2015 na kwa muda wote Tanzania kama ilivyokuwa kwa nchi nyingine.

Aliongeza
kuwa Tanzania imetumia wataalamu elekezi kufanya kazi hii chini ya
Mradi uliokuwa unatekelezwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa
(UNDP) kuratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais Idara ya Mazingira hivyo
kuleta ugumu katika kuthibiti ubora na kulinganisha takwimu za nchi
mbalimbali kwani hakukuwa na mfumo au njia iliyokubalika kimataifa
kufanya kazi na haikujenga uwezo wa sekta husika.
“Mfumo
wa Kitaifa wa ukusanyaji na usimamizi wa Takwimu za gesijoto,
unaozinduliwa leo utawezesha nchi kutoa  takwimu sahihi na za
kutosheleza kuhusu uzalishaji wa gesijoto kutoka sekta mbalimbali husika
na uondoshaji kwa njia ya misitu, kwa hatua sahihi za uamuzi na kutoa
taarifa,” alisema.

Aidha
Balozi Sokoine alisema kuwa uzinduzi wa Mfumo huu umekuja wakati
muafaka ambapo tunajipanga kuanza utekelezaji wa Makubaliano ya Paris
ambayo yalipitishwa na Mkutano wa 21 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa
Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabinchi na Tanzania kuridhia Mei
2018.

Aliongeza
kuwa kwa sasa Tanzania inakamilisha maandalizi ya Mchango wake katika
juhudi za kupambana na Mabadiliko ya Tabianchi hivyo Mfumo huo utasadia
katika upatikanaji wa takwimu na taarifa kuhusu utekelezaji wa NDCs na
uandaaji wa Taarifa ya Tatu ya Mawasiliano.


Utekelezaji wa Mfumo huu utahitaji kila mdau kubaini majukumu yake na
kuyatekeleza na hivyo kila mdau anatakiwa kubaini majukumu yake kama
yalivyobainishwa katika Mfumo ili  kuhakikisha kuwa Mfumo huu
unatekelezwa na hivyo kutuwezesha kufikia malengo tarajiwa,” alisisitiza
Balozi Sokoine.

Naibu
Katibu Mkuu aliagiza Kituo Cha Kitaifa cha Kuratibu Hewa Ukaa (NCMC)
kuratibu na kusimamia mfumo wa Kitaifa wa Ukusanyaji Takwimu za
Gesijoto, Ufuatiliaji, Uandaaji Taarifa na Uhakiki.

Aliagiza
Wizara za Kisekta ziteue Wataalamu watakaohusika na usimamizi na
uandaaji wa takwimu za uzalishaji wa gesijoto katika sekta zao na
kuwasilisha kwenye Kituo cha Kitaifa cha Kuratibu Hewa Ukaa.

Pia
aliagiza Wizara za Kisekta kwa kushirikiana na Kituo cha Kitaifa cha
Kuratibu Hewa Ukaa ziweke Utaratibu wa kuwasilisha taarifa katika Kituo
cha Kitaifa cha Kuratibu Hewa Ukaa kila mwaka.na kubainisha watoaji
takwimu chini ya sekta zao za uzalishaji wa gesijoto na kuweka utaratibu
wa kupata takwimu hizo.