Bilioni 23.5 zaokolewa na tanesco kila mwaka

Na  mwandishi wetu – Dodoma
Shilingi
Bilioni 23.5 zinaokolewa kila mwaka baada ya Serikali kupitia Shirika
la umeme Tanzania (TANESCO) kuzima mitambo ya kuzalisha umeme kwa
kutumia mafuta mazito.


Akizungumza
na waandishi wa habari leo, Jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya Shirika
hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya tano,
Mkurugenzi mtendaji wa Shirika hilo Dkt. Tito Mwinuka amesema kuwa
Shirika hilo limefanikiwa kujiendesha bila kupokea ruzuku  kufuatia
hatua zilizochukuliwa na Serikali ikiwemo kuzimwa kwa mitambo ya
kuzalisha umeme kwa kutumia mafuta.

“Tumezima
mitambo ya kuzalisha umeme kwa mafuta mazito katika maeneo ya 
Makambako, Tunduru, Liwale, Namtumbo, Ludewa, Madaba  na kuyaunganisha
na gridi ya Taifa hali inayochangia kuongeza kasi ya maendeleo katika
maeneo hayo na kupunguza gharama za uendeshaji ;” Alisisitiza Dkt.
Mwinuka

Akitaja
baadhi ya mitambo iliyozimwa Dkt. Mwinuka amesema kuwa ni  ile ya IPTL,
AGRECO, Syimbion na mingine  katika maeneo mbalimbali hapa nchini
iliyokuwa ikitumia mafuta katika uzalishaji wa umeme.

Akifafanua
amesema kuwa hali hiyo imechangia katika kuongeza mapato ya Shirika
hilo kutoka Shilingi takribani trilioni 1.2 mwaka 2012 hadi kufikia
zaidi ya trilioni 1.5 kwa mwaka kwa sasa hali inayoliwezesha Shirika
hilo kuendelea kuongeza tija katika utoaji wa huduma.

Kwa
upande wa wateja waliounganishiwa umeme wameongezeka kutoka milioni 1.6
waliokuwepo kufikia mwaka 2015 hadi zaidi ya milioni 2.7 kufikia mwaka
2019 sawa na ongezeko la wateja zaidi ya milioni 1.05 katika kipindi
hicho ambao ni asilimia 63.84.

Akizungumzia
miradi ya kimkakati Dkt. Mwinuka amesema kuwa ni pamoja na mradi wa
kufua umeme wa Mwalimu Nyerere katika Mto Rufiji megawati 2115
unaotekelezwa na Serikali kwa gharama ya shilingi trilioni 6.55, Rusumo
megawati 80, Kakono megawati 87, Mradi wa kuzalisha umeme kwa gesi
mkoani Mtwara megawati 300.

Akieleza
zaidi, Dkt. Mwinuka amesema kuwa miradi mingine inatekelezwa katika
maeneo mengine katika mikoa mbalimbali hapa nchini kwa lengo la
kuhakikisha kuwa kila mwananchi anafikiwa na huduma ya umeme.

Kwa
upande wa Vijiji vilivyounganishiwa umeme vimeongezeka kutoka 2018
mwaka 2015 hadi Vijiji 8236 kufikia Desemba 2019 ikiwa ni ongezeko la
asimia 67 hali inayotokana na jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano
kuhakikisha kuwa wananchi wote wanafikiwa na nishati ya umeme katika
maeneo yote.

Katika
kipindi cha miaka 4 umeme ulioongezwa kwenye gridi ya Taifa ni Megawati
400 zinazotokana na utekelezaji wa miradi ya kimkakati ikiwemo ya
Kinyerezi namba 1 na namba 2.

“Kwa upande wa wateja wa viwanda  wameongezeka kutoka 2571 mwaka 2015 hadi  3787 mwezi Desemba 2019;” Alisisitiza Dkt. Mwinuka

Shirika
la Umeme Tanzania (TANESCO) limetekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya
uzalishaji, usambazaji na uwekezaji katika sekta ya nishati ili kukuza
uchumi na ustawi wa wananchi.