Breaking news: rais magufuli aagiza wizara ya fedha kutoa shilingi bilioni 40 kulipa madeni ya korosho yaliyobaki

Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza
Wizara ya Fedha na Mipango kutoa shilingi Bilioni 40 kwa ajili ya
kumalizia madeni yote ya wakulima wa korosho yaliyobaki baada ya
Serikali kununua korosho za wakulima katika msimu wa mwaka 2018/19.


Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo Ikulu Jijini DSM alipokutana na
viongozi wa Wizara, Mikoa, Wilaya na Taasisi za Serikali ambazo
zinahusika katika uzalishaji na mauzo ya zao la Korosho.

Mkutano huo umehudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa.

Pamoja na kuagiza Wizara ya Fedha na Mipango itoe fedha hizo kesho
tarehe 02 Novemba, 2019 Rais Magufuli amewaagiza viongozi wa Mikoa na
Wilaya kuhakikisha fedha hizo zinawafikia wakulima na sio vinginevyo, na
pia kuhakikisha wanalipwa wakulima wanaostahili kupata malipo hayo.
Rais Magufuli ameelezea kutoridhishwa kwake na utendaji kazi wa Wizara
ya Kilimo na viongozi wa Mikoa na Wilaya ambao katika maeneo yao
kumetokea wizi mkubwa wa fedha za wakulima kupitia vyama vya msingi vya
ushirika (AMCOS) hali iliyosababisha wakulima wengi kuishi maisha duni.
Rais Magufuli amesema amesikitishwa kuona viongozi wa Wizara, Mikoa na
Wilaya hawajachukua hatua madhubuti dhidi ya watu wanaowaibia wakulima
mpaka alipoamua kumtuma Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Brig. Jenerali John Mbungo ambaye kwa
muda mfupi amebaini kuwepo wizi wa shilingi Bilioni 1.23 na tayari
amefanikisha kurejeshwa kwa shilingi Bilioni 375 katika Mkoa wa Lindi
pekee.
Amewataka viongozi wa Wizara ya Kilimo, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa
Wilaya kubadilika na kuhakikisha haki za wakulima zinalindwa ipasavyo
kwa kurejesha fedha zilizoibwa na kuzuia mianya yote ya wizi.
“Nataka mfanye kazi, hakuna mtu wa kuwanyanyasa, nendeni mkashughulikie
kero za wakulima, mna vyombo vya ulinzi na usalama nendeni mkavisimamie,
kinyume na hapo nitakuona hutoshi kwenye nafasi hiyo” Rais Magufuli.