Cag kichere: nitafanya kazi kulinda matumizi ya kodi za watanzania maana naujua ugumu wa kukusanya kodi

Na.Mwandishi Wetu-MAELEZO

Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mpya, Bw. Charles Kichere
amesema kuwa ataendelea kutekeleza majukumu ambayo yameachwa na CAG
aliyemaliza muda wake Prof.Mussa Assad kwani Ofisi hiyo ni muhimu kwa
maendeleo ya watanzania.


Akizungumza
katika makabidhiano Kichere alisema kuwa Ofisi ya CAG ni nguzo muhimu
kwa watanzani kwani ndiyo ofisi inayolinda na kuangalia matumizi sahihi
ya kodi yao wanayolipa kila siku.

“Tutaendelea
kuifanyakazi ambayo imefanywa na Prof.Assad na timu yake, nitahakikisha
kushirikiana na wafanyakazi wa Ofisi hii kuifanya kazi hii ya kulinda
mapato ya kodi ya watanzania”, Alisema Kichere.

Kichere
alisema kuwa katika kutekeleza majukumu hayo mapya atahakikisha kuwa
atalinda Kodi ya watanzania wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara
na wafanyakazi ili fedha inayopataikana kwenye kodi iweze kuwanufaisha
wote.

Aliwahakikishia
watanzania kuwa hakuna kodi inayotolewa na watanzania ambayo itapotea
kwa hiyo ataangalia na kuilinda  kwaajili ya kuwaletea maendeleo.

“Nataka
kufanya kazi kulinda maslahi ya watanzania nimefanyakazi Mamlaka ya
Mapato Tanzania TRA najua ugumu wa kukusanya kodi na kupata mapato, kwa
hiyo nitahakikisha kuwa nailinda kodi ya wananchi kwa wivu mkubwa sana”,
Alisisitiza Kichere.